Ads (728x90)

VIBINTI HIVI VINADAIWA KUBAKWA KWA ZAMU NA MCHUNGAJI WA KANISA LA PENTEKOSTE
Baadhi ya walimu wa shule ya Msingi Maendeleo wakizungumza kwa hisia tukio hilo la ubakaji lililofanywa na Mchungaji
Kanisa linaloendeshwa na Mchungaji Bryson Mwaikambo
Shule ya Msingi Maendeleo ambako wanasoma wasichana wanaodaiwa kubakwa na Mchungaji kwa zamu
Wazazi wa watoto wanaodaiwa kubakwa na Mchungaji wakiwa katika sura ya huzuni
Nyumba anayoishi Mchungaji Mwaikambo ikiwa imepigwa kufuri huku mwenyewe akiwa ''amelala mbele!! baada ya kufanya unyama wake
Kufuri!!! Ngaaa!!!! mchungaji huyooo kasepa
Nyumba anayoishi Mchungaji Mwaikambo
Diwani wa Kata ya Nsalala Mashauri Mbembela akitoa msimamo wake juu ya vitendo vya kinyama walivyofanyiwa mabinti hao


Ripota Wetu
MCHUNGAJI wa kanisa la Pentekostal aliyefahamika kwa jina la Bryson Mwaikambo(55) anadaiwa kuwabaka na kuwaambukiza ugonjwa wa zinaa wanafunzi wawili wa kike wanaosoma katika shule ya msingi ya Maendeleo wa  kata ya Nsalala wilaya ya Mbeya vijiji mkoani Mbeya.
Wanafunzi hao (majina yanahifadhiwa) wenye umri kati ya miaka 11 na 13 wanaosoma darasa la nne na darasa la sita walifanyiwa unyama huo kuanzia mwaka 2012 ambapo alianza kujenga mazoea na watoto hao wadogo kwa kuwapa peremende  pamoja  na fedha.
Imeelezwa kuwa mchungaji huyo ambaye anaendesha ibada katika kanisa hilo dogo lenye waumini wachache lililopo kitongoji cha kanani kijiji cha ‘Tunduma Road’alikuwa akiwavizia watoto hao kwa muda mrefu kila walipokuwa wanapita kuelekea shuleni.
Katika jitihada zake za kuwanasa watoto hao wa kike alimdanganya mmoja wa wazazi wa watoto aliyefahamika kwa jina la Bw.John Mussa(38) na kumuomba binti yake awe anamsaidia kazi za nyumbani nyakati za jioni kutokana na kuwa  mke wa mchungaji kuwepo safarini.
Kwa kuamini kuwa mchungaji huyo alikuwa ni mtumishi wa Mungu, Bw. Mussa aliridhia mwanaye aende kuishi na Mtumishi huyo wa Mungu bila kujua hatima ya kile ambacho kimemtokea binti yake kwa sasa.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa wazazi na walimu wa shule ya Msingi Maendeleo ni kwamba mabinti hao walikuwa wakifanya ngono na mchungaji huyo kwa zamu na kwamba walianza kujua tatizo hilo baada ya kutokea mgongano baina ya wasichana hao wawili .
‘’Tumejua tukio hili baada ya kutokea ugomvi baina yao wa kugombania maji na hivyo kuanza kurushiana maneno, mmoja wa watoto hao alikuja ofisini kushitaki kuhusu ugomvi wao ndipo mmoja akasema kuwa mwenzie anatembea na Mchungaji Mwaikambo’’alisema Mwalimu mkuu msaidizi Bi. Lucy Kamongile.
Alifafanua kuwa, baada ya tukio hilo walimu kwa pamoja walilazimika kuwauliza zaidi ndipo walipoanza kujieleza kuwa wamekuwa wakilala na Mchungaji huyo kwa muda mrefu na kwamba mwanzo alikuwa akiwapa peremende na baadaye akaanza kuwapa fedha.
Alisema kuwa walilazimika kuitisha kikao cha dharura baina ya wazazi wa watoto hao na walimu ambapo walieleza tukio zima la kuingiliwa kimwili na Mchungaji huyo tangu mwaka jana.
‘’Nililazimika kuwaita wazazi pamoja na wanafunzi tulikaa katika ofisi ya walimu, watoto walieleza tukio zima mbele ya wazazi wao juu ya vitendo walivyokuwa wakifanyiwa na Mchungaji huyo.
Alisema kuwa mara baada ya kikao hicho cha wazazi waliwapeleka watoto hao katika kituo kidogo cha Polisi kilichopo  katika mji  mdogo wa Mbalizi ambako walipewa Fomu ya Polisi Na. 3,(PF3) kwa ajili ya kuepelekwa hospitali ili wapatiwe matibabu.
Mwalimu Kamongile ambaye alikuwa na walimu wenzie katika ofisi ya Mwalimu mkuu wa shule hiyo wakati akitoa taarifa hizi mbele ya Ripota Wetu kuwa wanafunzi hao walipatiwa matibabu katika hospitali Teule ya Ifisi ambapo kwa mujibu wa taarifa za mganga aliyewachunguza  watoto hao ni kwamba mbali na kufanyiwa ubakaji wote wawili walikuwa wameambukizwa ugonjwa wa zinaa wa kaswende.
‘’Tukio hili limetufedhehesha sana tulikuwa tunatafakari wapi tutaenda,tunaomba kilio chetu kifike chama cha Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kitoe taarifa hizi kwa undani waone namna ambavyo jamii ya pembezoni inavyokosa msaada na haki za kisheria,’’alisema Mwalimu Kamongile. 
Mwalimu huyo alisema kuwa wanatambua juhudi za chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA ambazo wamekuwa wakizifanya hivyo wanaimani chama hicho kikisikia suala kitalifanyia kazi kwa kina zaidi kuisaidia jamii ambayo aina mahali pa kusemea.
Kwa upande wa watoto hao ambao walikuwa wakizungumza kwa kupokezana juu ya kadhia iliyowakuta walisema kuwa Mchungaji huyo alianza kufanya nao vitendo vya ngono tangu mwaka 2012 kwa kuwadanganya kwa fedha na peremende na baadaye wakazoea kwenda kwa Mchungaji huyo mara kwa mara.
Mwanafunzi anayesoma darasa la nne alisema kuwa alianza kutembea na Mchungaji huyo wakati akimpitia mwenzie aliyekuwa akiishi nyumbani kwa mchungaji ambapo siku hiyo alimuita chumbani kwake na kumlazimisha kulala kitandani ambapo alianza kumuingiza vidole katika sehemu zake za siri.
“Siku ya kwanza nililia sana wakati mwenzangu yupo pembeni akishuhudia mchungaji akinifanya na ndipo mwenzangu alisema jikaze rafiki yangu”alisema Mtoto huyo.
Alisema kuwa mara baada ya kumuingiza vidole alivua nguo zake na kumbaka huku akilia wakati msichana mwenzie (alimtaja jina) akiwa amekaa pembeni ya kitanda akimweleza kuwa aache kulia kwa kuwa baada ya kumaliza watapewa fedha za kutumia shuleni.
Binti huyo aliendelea kusema kuwa alipata maumivu makali wakati Mchungaji huyo akitekeleza ubakaji wake ambapo mara baada ya kumaliza` alimpa sh.500 na peremende na baadaye alimwita mwenzie kitandani na kufanya naye ngono huku akishuhudia kwa macho yake.
Alisema mara baada ya kumaliza kufanya na mwenzie Mchungaji Mwaikambo aliwaonya wasiseme kwa wazazi wao kisha akawapa fedha na kuwaonya wasiseme jambo hilo kwa mtu yoyote.
Akizungumza sababu za kutosema kwa walimu au wazazi wake binti mwingine anayesoma darasa la sita alisema kuwa Mchungaji huyo aliwatishia kuwachinja na kuwafukia kwenye shimo iwapo atasikia wamesema tukio hilo kwa wazazi ama walimu wao.
Alisema kuwa Mchungaji aliwaomba wazazi wake ili aende kuishi nyumbani kwake kumsaidia kazi kutokana na mama Mchungaji ‘’Mke wa Mchungaji’’ kuwa safarini na kwamba katika siku hizo ndipo Mchungaji huyo alipoanza kulala naye mahusiano taratibu.
Alisema kwa siku za mwanzo alikuwa akimuingiza vidole katika sehemu zake za siri na baadaye akaanza kumbaka ambapo alijisikia maumivu makali lakini alimbembeleza kwa kumpa sh.1000 ambayo alikuwa akitumia shuleni kwa kununua chipsi.
‘’Alikuwa akiniingiza vidole huku chini(akionyesha sehemu za siri) akanibaka, sikuweza kumwambia baba niliogopa atanichinja..mwenzangu alipokuwa anakuja kunipitia kwenda shuleni naye alianza kumuingiza vidole akambaka!!, alilia sana, nikamwambia asilie atatupa hela,’’alisema.
Alisema kuwa wamebakwa na Mchungaji huyo zaidi ya mara nne na kila alipokuwa akiwabaka alikuwa anawapa hela za kutumia shuleni.
Kwa upande wazazi wa watoto hao Bw.Suveli Harrison na Bw. John Mussa walikiri kuitwa shuleni na kupata taarifa za kubakwa kwa watoto wao walipoitwa shuleni ambapo watoto walijieleza walichokuwa wakifanyiwa na Mchungaji Mwaikambo mbele ya walimu.
‘’Jambo hili lilitushitua sana, machozi yalitulenga, hatukutegemea kusikia Mchungaji anaweza kuwabaka watoto ambao ni sawa na wajukuu zake, tulienda polisi walitupa karatasi tukaenda Hospitali ya Ifisi, watoto walikutwa na maambukizi ya ugonjwa wa zinaa,’’alisema Bw. John Mussa.
Alisema kuwa yeye aliridhia mwanaye kuishi na Mchungaji huyo baada ya kuombwa kutokana na mchungaji huyo kuishi na mtoto mdogo wakati mkewe akiwa safarini.
Bw. Mussa alisema kuwa hakujua kuwa kama kuna siku mwanaye atadhurika kwa kufanyiwa kitendo cha unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kama walivyofanyiwa watoto hao na kwamba hata hivyo hadi sasa hakuna jitihada zozote za jeshi la polisi zilizofanikisha kumnasa Mchungaji huyo.
Alisema kuwa kwa sasa watoto hao wamekuwa wakitishiwa na Mchungaji kutokana na kufahamika kuwa yeye aliwabaka na kwamba anaomba msaada wa kisheria kusimamia haki ili sheria iifuatwe dhidi ya mtuhumiwa wa ubakaji.
Naye mzazi mwingine Bw.Suvile Harrison alisema kuwa hakujua chochote juu ya vitendo alivyofanyiwa mwanaye na Mchungaji huyo na  kwamba alifahamu tukio hilo baada ya kuitwa shuleni ambako walimu waliwaita watoto wao na kueleza tukio zima walilokuwa wakifanyiwa na Mchungaji.
Alisema kuwa hakubaini mabadiliko yoyote kwa mwanaye juu ya vitendo alivyofanyiwa na wala hajawahi kuhisi lolote hadi hapo alipoitwa shuleni na walimu.
Baada ya taarifa hizo waandishi wa habari wa gazeti hili walifunga safari hadi katika nyumba ambayo inasadikiwa kuwa ndipo anapoishi Mchungaji huyo na kukuta mlango ukiwa umefungwa lakini alijitokeza jamaa ambaye alijitambulisha kuwa ni mmiliki wa nyumba hiyo Bw. Zacharia Gambi.
Bw.Gambi alisema kuwa anamfahamu mpangaji wake kwa jina moja la Mchungaji Mwaikambo na kwamba mbali ya kuwa ni Mchungaji wa Kanisa la Kipentekoste ni Balozi wa nyumba kumi wa mtaa wa Kanani.
Bw.Gambi alisema kuwa Mchungaji huyo hajaonekana muda mrefu na kwamba mkewe amekuwa na desturi ya kuondoka alfajiri kuelekea shambani na kurudi usiku.
Kadhalika imeelezwa na baadhi ya watu ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini kuwa  kitendo cha Mchungaji huyo kuwabaka mabinti wadogo kimetokana na imani za nguvu za giza kwamba kwa kufanya hivyo kitamuongezea waumini katika kanisa lake dogo lililopo katika mtaa wa Kanani.
Mama mzazi wa mmoja wa watoto waliobakwa aliyejitambulisha kwa jina la Jane John(35) alisema kuwa awali yeye alikuwa ni mmoja wa waumini katika kanisa hilo lakini baadaye walihamia kanisa jingine baada ya kuona mienendo ya mchungaji huyo kutofanana na kazi ya huduma za kiroho.
Alisema waumini wengi wamehama katika kanisa hilo wakiwemo watoto wake wakubwa wa kike ambao walieleza waziwazi tabia ya ukware ya Mchungaji huyo ya kuwafuatilia mabinti wadogo kwa ajili ya kufanya nao vitendo vya ngono.
Diwani wa Kata ya Nsalala iliyopo Mbeya vijijini Bw.Mashauri Mbembela alipozungumza na waandishi wa gazeti hili alisema kuwa anashangazwa tukio hilo kutoshughulikiwa kwa kipindi chote huku taarifa zikiwa zimefikishwa kituo cha polisi.
Alisema kuwa tukio hilo ni la unyanyasaji ambalo lilipaswa kushughulikiwa kwa nguvu zote na kwamba kuna haja ya kuweka sheria ngumu itakayokomesha vitendo vya ubakaji kwa watoto wa kike.
Bw.Mbembela alisema kuwa ili kukomesha tabia za ubakaji, itungwe sheria ya kuwahasi wabakaji badala ya kuwafunga jela miaka 30  ambako wanaenda kula chakula kinachotokana na kodi za wananchi.
‘’Wabakaji wanafungwa jela, wakimaliza vifungo vyao hurejea uraiani ambako wanaweza kuendeleza vitendo hivyo, njia pekee ya kukomesha ubakaji ni kuwahasi, wakirudi uraiani wataendeleza kujenga Taifa,’’alisema Bw. Mbembela.
Ripota wetu alifanya jitihada za kutafuta namba za simu za mchungaji huyo ambaye mara baada ya kupokea na kuulizwa juu ya tuhuma hizo alikanusha na kusema kuwa huu ni uzushi na uongo uliolenga kumpaka matope ili kuchafua huduma zake anazotoa kwa waumini .
Alidai kuwa kanisa lake la Pentecostal Holiness lenye  jumla waumini nane linatoa huduma za uhakika kijijini hapo hivyo baadhi ya wafuasi wa shetani wanalipiga vita ili lisiendelee kukua ili kuwafikia wanakondoo wengi.
“Wananipakazia tu unaweza kuingiwa na ibilisi na hivi ulivyonipigia nafikiria kuchukua maamuzi magumu na mwili wangu hamtauona kamwe bora uliwe na ndege  na wanyama wa porini  niende jehanamu kuliko kuchafuliwa huku”alisema Mchungaji huyo.
Alisema kuwa tuhuma hizo zimeelekezwa kwake baada ya kumdai fedha mmoja wa wazazi wa watoto hao ambaye alikuwa akifanya kibarua cha kujenga ofisi ya kata ambapo mama huyo alimkopesha fedha sh.5000 na alipoanza kudai ndipo akaanza kuzushiwa tuhuma hizo.
Hata hivyo alisema  Jumanne iliyopita alifuatwa na askari mgambo sita wenye virungu ambao walitaka kumkamata lakini kwa nguvu za yesu walishindwa na kuondoka zao.
“Mimi naishi kwa nguvu za Yesu mtu yeyote mwenye nia mbaya na mimi hawezi kunipata nataka niwe kama mfalme aliyejitoa mhanga nijiue mwili wangu usionekane duniani”alisisitiza na kukata simu.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Bw.Diwani Athumani alisema kuwa amepata taarifa hizo za ubakaji ambapo amemuagiza Ofisa Upelelezi wa Mkoa Bw.Mtatiro Nyamuhanga ambaye atalifuatilia kwa karibu tukio hilo na kwamba hata hivyo mtuhumiwa bado hajatiwa mbaroni.

Post a Comment