Ads (728x90)



Mkulima mwenye shamba bora la Chai nchini Bi. Josephine Njuwensi akiwa shambani kwake katika kijiji cha Bujesi wilayani Rungwe

Mtendaji Mkuu wa Wakulima wadogo wa Chai Lebby Gabriel akifafanua jambo katika shamba la chai.
Baadhi ya wakulima wa Chai wilayani Rungwe wakiwa katika kikao cha kamati ya chai kujadili mustakabali wa zao la chai.



WILAYA ya Rungwe ni kati ya wilaya 9 za Mkoa wa Mbeya ambayo ina ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha chakula na biashara, asilimia 80 ya wakazi wake zaidi ya 300,000 (sensa ya mwaka 2002) wanategemea kuendesha maisha yao kwa shughuli za kilimo.

Umaarufu wa wilaya ya Rungwe umeongeza ushindani katika Nyanja za kilimo husuani katika zao la Chai huku wakulima wakihitaji msaada zaidi kutoka serikalini ili upatikane uwezeshaji wa uwekezaji wenye tija kwa nia ya kuongeza pato la uchumi kwa mkulima mmoja mmoja, vikundi, wilaya, mkoa na hata Taifa.

Umuhimu huu huongezeka zaidi pale serikali inapomudu kuuza mazao yake nje ya nchi na kujiingizia fedha za kigeni kutokana na mazao ya kibiashara yanayozalishwa nchini.

Hali ya hewa rafiki ya wilaya hiyo inatoa fursa kuvutia wakulima wa mazao ya chakula na biashara na kuimarisha uchumi wa wakazi wake wanaotegemea kujiinua kiuchumi na kuondokana na utegemezi ambao unatishia umaskini wa kipato.

Fursa adimu na adhimu ya ardhi wilayani humo inatoa tija kwa wakazi wake na kufika mahala kuwatoa ‘udenda’ baadhi ya wawekezaji wenye uchu na  matajiri wageni kuitamani ardhi hiyo na ikiwezekana kuihodhi na hata kupokonya kutokana na kuwa na  rutuba inayomea mazao lukuki yenye manufaa kwa wakulima.

Wilaya ya Rungwe ni moja kati ya wilaya zenye mashamba makubwa ya chai ambapo asilimia kubwa ya wakazi wake aidha wamelima chai ama familia zao zinategemea ama zimenufaika na zao hilo kongwe wilayani humo.

Chai ni moja ya mazao makubwa ya kibiashara wilayani humo ambayo yanachangia uchumi wa wilaya ijapokuwa kuna changamoto lukuki zinazowakumba wakulima wa zao hilo kutokana na uhitaji wa matajiri wakubwa kumiliki zao hilo na kuwafanya wakulima wa zao hilo kuwa kama manamba katika mashamba yao.

Hali hiyo imewafanya wakulima watafakari namna ya kujikwamua na ukiritimba wa wanunuzi na walanguzi wa chai ambao huwaacha wakulima wakiendelea kulima bila kuwezeshwa kwa mahitaji muhimu ya uzalishaji bora wa zao hilo kama vile wataalamu,pembejeo za kilimo na mbolea ya ruzuku.

Kimsingi kulingana na sheria na kanuni za tasnia ya zao la chai husimamiwa  na Bodi chini ya sheria ya chai Na. 3 ya mwaka 1997 sura ya 275 ya sheria ya Tanzania iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 pamoja na kanuni zake za mwaka 2010 kwa muji wa tangazo la serikali Na.42 la mwaka 2010.

Sheria hizo na kanuni zinaweka masharti ya msingi kwa ajili ya kuzingatiwa na mkulima, mnunuzi na msindikaji wa chai ili kuhakikisha kuwa chai inayozalishwa na kusindikwa inakidhi ubora unaokubalika  Kimataifa ili kuiwezesha kupata soko la uhakika.

Aidha sheria hii inalenga kumlinda mlaji au mtumiaji wa bidhaa za chai ili aweze kupata chai yenye ubora wa uhakika na hivyo kumuongezea kipato.

Wakulima wadogo wapatao 15,000 waliopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya huzalisha wastani wa jumla ya kilo milioni 20 kwa mwaka ambayo ni sawa na tani 20 ambayo  ni nusu ya wakulima wadogo wote nchini.

Idadi hii ya wakulima wa Chai waliojiunga pamoja wanaojulikana kwa kifupi  RSTGA (Rungwe Small Holder Tea Growers  Association) huuza majani ya chai mabichi katika kiwanda cha Wakulima Tea Company(WTC) ambao kimantiki wanahitaji kupata mfumo mpya wa maisha yanayowezeshwa  na kilimo cha chai.

Manufaa ya wakulima katika kiwanda hicho yanajionesha kulingana na maelezo yao kwamba umekuwepo umiliki wa pamoja wa kiwanda ambapo kila mkulima mwanachama ana hisa ya asilimia 30 ya kiwanda hicho kutokana na mauzo ya majani mabichi ya chai na ongezeko la thamani ya umiliki wa pamoja.

Kwa kuthamini thamani ya ardhi yao yenye rutuba wananchi wa wilaya ya Rungwe waliamua kujiunga pamoja na kuunda Umoja wa Wakulima Wadogo wa Chai(RSTGA) mwaka 1998 ukiwa na lengo la jumla la kuboresha maisha ya wakulima hao  kwa kuongeza mapato yatokanayo na majani mabichi ya chai na ongezeko la thamani ya umiliki wa pamoja.

Bw. Steven Mwaikuka mkulima na mkazi wa kijiji cha Katumba  mmoja wa wanachama wa (RSTGA)anasema kuwa kuwepo kwake katika umoja kumemuwezesha kujenga nyumba ya kisasa yenye umeme na maji ambapo pia anapata gawio la hisa kutoka kiwanda cha chai cha WTC.

Anasema  mbali na hisa anazopata kila mwaka kutoka kiwandani hapo ananufaika na  malipo ya pili kila baada ya miezi mitatu ikiwa ni pamoja na  kukopeshwa pembejeo za kilimo wanazorejesha  kwa kukatwa baada ya kuuza majani mabichi kila mwezi sh.75/.

Bi. Josephine Kindole Njunwensi(56) ni mkulima wa kijiji cha Bujesi ni mmoja kati ya wakulima wa chai  mahiri wa zao hili ambaye mwaka huu  ametunukiwa cheti na zawadi kwa kuwa na shamba bora la chai kuliko mashamba yote nchini.

Mkulima huyu ambaye ni mjane anasema kuwa anathamini zao la chai kwa kuwa linamuendeshea maisha yake na kuwa yeye ni miongoni mwa wanahisa wa Kiwanda cha Chai cha WTC ambapo ananufaika kwa kupata pembejeo za kilimo na gawio la hisa kulingana na hisa zake zilizopo kiwandani.

Anasema kutokana na kilimo cha chai ameweza kumudu  maisha bila kuwepo mumewe ambaye kwa sasa ni marehemu aliyemtaja kwa jina la  Zephrine Njunwensi na kwamba anashukuru jitihada za mumewe kumuwekea msingi bora wa maisha ya kilimo cha chai ambacho kwa sasa ndicho kinachomuendeshea maisha pamoja na watoto wake watano aliomuachia.

‘’Kutokana na chai nimefungua mradi wa maduka mawili, duka la vinywaji vya jumla na rejareja na shamba kubwa la chai, kutokana na ubora wa shamba letu nimefanikiwa kuwa mkulima mwenye shamba bora la chai nchini’’ anasema Bi. Njuwensi.

Mtendaji mkuu wa Umoja huo Bw.Lebby Gabriel anasema kuwa  tangu kuanzishwa kwake, umoja huo umekuwa ukitekeleza mikakati mbalimbali kuendeleza maslahi na ustawi wa wakulima wadogo wa chai wilayani Rungwe ikiwa ni pamoja na kuboresha uwingi wa majani yanayozalishwa na wanachama, kuwakilisha umiliki wa mwanachama na maslahi yake.

Anasema kuwa hisa za mwanachama huwakilishwa katika kampuni yoyote ya kibiashara inayoongeza thamani ya mapato kwa nia ya kuinua hali ya biashara na kusimamia fedha na miradi ya pamoja na kufanya mawasiliano baina ya wanachama na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Bw. Gabriel anasema kuwa katika mikakati hiyo ya umoja umeweza kupata mafanikio kutokana na wanaumoja kuboreshewa maisha yao ambapo hadi sasa uzalishaji wa masjani mabichi ya chai umeongezeka kutoka tani 3,000 mwaka 2001 hadi tani 20,500 mwaka 2012.

Anasema kuwa sanjari na ongezeko hilo wakulima wameanza kunufaika na bei ya majani mabichi ya chai kutoka sh. 71.25 mwaka 2001 hadi sh.231.00 mwaka 2013 ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa malipo ya pili kwa majani mabichi ya chai yaliyofikia wastani wa sh.25/= kwa kilo mwaka 2012.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakulima wadogo Bw. Johnson Mwakasege kupitia umoja wao wa (RSTGA) wameweza kunufaika na ujenzi wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya sh. bilioni 1.7 tangu mwaka 2002 ambayo ni ujenzi wa madarasa, zahanati, Nyumba za walimu,ujenzi wa madaraja, maji safi na kuwezeshwa kuanzishwa kwa chama cha Akiba na Mikopo SACCOS.

Bw. Mwakasege anasema kuwa  mwaka 2012 kampuni ya WTC ilikusanya sh. milioni 200 kutokana na ununuzi wa hisa kwa wanachama wake ambazo zinawanufaisha wanachama kwa kupata gawio kila mwaka kulingana na hisa za mwanachama.

Anasema kuwa thamani ya zao hilo inatokana na kilimo bora cha chai kutoka kwa wataalamu wa kilimo,uhifadhi wa mazingira ya kilimo cha zao hilo sanjari na uanzishwaji wa vitalu vya miti ambapo pia kamati za Chai  hupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ya uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Mkuu wa wilaya ya Rungwe Crispin Meela anasema kuwa zao la Chai ni kati ya mazao ya mazao makubwa ya biashara yanayopatikana wilayani humo na kwamba wakulima hawapaswi kukatishwa tamaa juu ya kilimo hicho ambacho kinawapa tija na kuinua uchumi wao na uchumi wa wilaya ya Rungwe.








Post a Comment