Ads (728x90)

Moja ya nyumba zinazodaiwa kuwa ni mali ya halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambazo zinamilikiwa na baadhi ya wafanyabiashara

Nyumba ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambayo imepangishwa kwa taasisi ya kifedha ambayo inadaiwa kuwa fedha zinazotokana na pango la nyumba hiyo haziingii katika mfuko wa Halmashauri ya wilaya

Jengo la Halmashauri ya wilaya ambayo ni sehemu ya kitega uchumi cha halmashauri hiyo mapato yatokanayo na pango la nyumba hiyo yanadaiwa kuwa  hayaingii kwenye mfuko wa halmashauri ya wilaya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye akizungumza katika kikao cha Halmashauri ya wilaya ya Mbozi na kutoa tamko la kuvunja mikataba kwa wapangaji wa halmashauri hiyo

Baadhi ya Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi wakifuatilia kwa makini kikao cha Baraza ambacho kilitoa tamko la kuvunjwa kwa mikataba ya nyumba kwa wapangaji wake


HALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi imezinduka na kuvunja mikataba ya baadhi ya nyumba zake ambazo ilizitelekeza kwa zaidi ya miaka 30 na kuwataka wamiliki wa nyumba hizo kukabidhi nyaraka za mikataba walioingia na watumishi wa halmashauri hizo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa wilaya ya Mbozi Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elick Ambakisye alisema kuwa,baada ya kufuatilia kwa kina imebaini kuwa wapo watendaji wa halmashauri walioingia mikataba na wapangaji wa nyumba hizo ambazo halmashauri ilikuwa haipati chochote.

Alisema kuwa kuanzia jana Novemba Mosi nyumba zote za halmashauri ambazo upangaji wake una utata mikataba yake itavunjwa na kupitiwa upya ili halmashauri ianze kunufaika na mali zake.

Bw. Ambakisye alisema kuwa imebainika kuwa nyumba tatu zilizoripotiwa ni mali ya halmashauri ambapo aidha wapangaji wake waliingia mkataba na watendaji wa awali ambao hawakuweka bayana mikataba ya mali za halmashauri hiyo.

Alizitaja nyumba hizo kuwa ni pamoja na MDC ambayo ni Bar iliyokuwa ikimilikiwa na halmashauri lakini kutokana na kushindwa kuiendesha ilitelekezwa kwa wafanyakazi ambao walikusanya fedha za mapato ya Bar hiyo bila kuwasilisha ofisini.

Alisema nyumba nyingine ni jengo ambalo limepangishwa duka la Tanganyika Farmers Association (TFA) ambalo waliingia mkataba na halmashauri kwa miaka 12 na kwamba mkataba huyo utapitiwa upya na kuanzia Novemba Mosi makusanyo yote ya kodi yataingia katika mfuko wa halmashauri.

Aidha aliitaja nyumba nyingine ya halmashauri ambayo ilikabidhiwa kiholela kwa chama cha Akiba na Mikopo cha akina mama WAT SACCOS  ambao baadaye walijimilikisha kiholela ikiwa ni pamoja na kuingia mkataba na  wapangaji wengine na fedha zilizopatikana zilikuwa zikiingia katika mfuko wa akina mama bila kuihuisha Halmashauri.

Alisema kuanzia sasa makusanyo ya fedha zote ambazo kwa zaidi ya miaka 30 zimekuwa zikiingia katika mifuko ya pembeni zitaingia katika mfuko wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi.

Awali gazeti hili liliripoti taarifa za kutafunwa kwa mamilioni ya fedha zilizotokana na nyumba 3 za halmashauri kwa takribani miaka 30 huku ikidaiwa kuwa fedha hizo zilikuwa zikiingia mifukoni mwa watendaji wachache waliodaiwa kuficha vyanoz hivyo vya mapato.

Ilidaiwa kuwa tangu zilipopangishwa nyumba hizo mapato yake yalikuwa hayajulikani huku baadhi ya watendaji wakidaiwa kutafuna fedha hizo ilhali halmashauri husika ikiwa haiwatambui wapangaji wa nyumba hizo.

Post a Comment