Ads (728x90)

Leo niliamua kujiridhisha kwa kutembea umbali wa kilomita 2 hatua kwa hatua kutokea Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani iliyopo jijini Mbeya hadi Meta, katika hatua zangu nikajionea barabara mpya iliyokabidhiwa takribani miezi miwili iliyopita ikiwa katika hali hii unayoiona pichani.

Mafundi wakijaribu kuziba viraka katika barabara ya kilomita 2 kutokea Stendi Kuu hadi Meta ambayo imetengenezwa chini ya kiwango na kusababisha kubomoka miezi miwili tu tangu ianze kutumika.
Harakati za kufukia mahandaki kwa viraka katika barabara mpya ya Stand Kuu hadi Meta ilikuwa hivi

 
Nimeshuhudia barabara hiyo ikiwa na mahandaki kiasi cha kusababisha baadhi ya magari yanayopita njia hiyo kukwepa pembeni na kuharibu ladha yote ya safari kwa wasafirishaji na abiria waliomo katika vyombo vya usafiri wanavyotumia.

Kwa kuangalia haraka haraka unaweza kudhani ni maua yamechorwa katika barabara hii, La hasha haya si maua bali ubovu wa barabara iliyotengenezwa na Kampuni moja ya Kichina.

Awali mara baada ya kukamilika kwa barabara hii madereva na wasafiri walikuwa wakijivunia kupita katika barabara hii lakini kwa sasa imekuwa ni machungu kwa magari kukutana na adha ya mahandaki.
Barabara inavyoonekana baada ya kuanza kutumiwa
Barabara kati ya Stendi Kuu na Meta inavyoonekana pichani.
Gari likijitahidi kupita kwa uangalifu katika mahandaki yaliyopo katika barabara mpya iliyokabidhiwa na kuanza kutumika kama inavyoonekana pichani.
Viraka katika barabara ya Stendi Kuu hadi Meta inavyoonekana
Hivi ndivyo inavyoonekana barabara hiyo kama ilivyokutwa leo asubuhi na paparazi wetu aliyeamua kujiridhisha na kutembea hatua kwa hatua kujionea hali halisi ya barabara hiyo.

''Nilitamani kuishia njiani kwa safari yangu lakini nilijikuta kadri ninavyoendelea kutembea ndivyo ambavyo niliendelea kukutana na madudu mengine, maana kila nilipoangalia mbele yangu niliona mahandaki mengine yakiwa yamepangana hatua kwa hatua.



Viraka vya barabara mpya iliyokabidhiwa na kuanza kutumika hivi karibuni
Niliendelea kuiivinjari barabara hatua kwa hatua huku jasho likinitiririka kama vile na mie ni mhandisi wa Jiji, hakuna lolote ni umbea tu uliendelea kunisukuma na kunifikisha hapa, lakini Noo!! naamini huu umbea una mantiki ni umbea wenye manufaa, ni umbea chokonozi unaoweza kuibua mengi yaliyojificha juu ya mikataba inayopitishwa na Halmashauri zetu na hata kugawa zabuni kwa wakandarasi wasiokidhi vigezo.


Hapa ni eneo la Mabatini ambako barabara hiyo iliyogharimu fedha za walipa kodi imepita kuelekea karibu na Hospitali ya wazazi META.

Niliendelea kujisukuma taratibu na akupandisha kilima kidogo kutokea Mabatini hadi kituo cha Meta hospitali..

Na hapa ndio mwisho wa safari yangu ya kutembea kwa miguu kuchokonoa juu ya hali ya barabara iliyojengwa na kampuni moja ya kichina na kukabidhiwa, yapo maswali mengi ambayo bado hayajajibwa juu ya barabara hii, nadhani hata msomaji atahoji kwa nini sijajikita ndani zaidi kujua mengi yaliyojificha kuhusu barabara hii, naomba niishie hapa ila hii ni tip kwa wengine watakaopenda kufuatilia kwa undani juu ya haya yafuatayo, kwanza, mkataba wa mkandarasi na Halmashauri ya Jiji ukoje, pili zabuni hii ilishindanishwa hadi kukabidhiwa mzabuni huyu aliyeboronga?,makubaliano yakoje baina ya Mkandarasi na Halmashauri ya Jiji, Mkandarasi aliyepewa kazi hii anayo sifa inayokidhi vigezo kukabidhiwa kazi hii? maswali haya na mengine mengi yanafaa kuulizwa ili kukamilisha stori hii, nia yetu si kubomoa bali ni Kujenga, naamini kwa pamoja tunaweza kuijenga Mbeya ikasonga mbele katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.


Post a Comment