Ads (728x90)

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi 
Na Rashid Mkwinda
MKAZI wa kijiji cha Kapele Tarafa ya Ndalambo wilayani Momba mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la Bonny Silumbe anatafutwa na Jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua ndugu yake aliyefahamika kwa jina la Adam Silumbe(27) kwa madai ya kulipiza kisasi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi alisema kuwa tukio hilo limetokea Januari 10  majira ya saa 3:00 usiku katika kijiji cha Kapele wilayani humo.

Kamanda Msangi alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo kimetokana na madai kuwa muuaji ambaye ni ndugu wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Bonny Silumbe alimchoma kisu mgongoni nduguye Adam kwa madai kuwa alikuwa akilipiza kisasi baada ya Adam kumtangaza kuwa alimtorosha mke wa mtu.

Alisema mara baada ya Adam kuchomwa kisu alikimbizwa katika Hospitali wilaya ya Mbozi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo Januari 12 majira ya saa 3:30 asubuhi alifariki dunia.

‘’Chanzo kinaelezwa kuwa ni kulipiza kisasi, baada ya marehemu kumtangaza mtuhumiwa hapo kijijini kuwa alimtorosha mke wa mtu, mtuhumiwa alikimbia baada ya tukio, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi,’’alisema Kamanda Msangi.

Kamanda Msangi ametoa taarifa kwa umma kuwa yoyote atakayemuona mtuhumiwa atoe taarifa kituo cha polisi au ajisalimishe mwenyewe kabla ya kutiwa mbaroni na vyombo vya dola na kwamba wanajamii wanapaswa kutatua matatizo yao ya kifamilia badala ya kuchukua sheria mkononi na kusababisha madhara.

Wakati huo huo mkazi wa kijiji cha Lema tarafa ya Ntembela wilaya ya Kyelaaliyefahamika kwa jina la Bicco Mwakibibi(28) aliuawa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kutoka kwa kutumia silaha za jadi za mawe na fimbo kutoka kwa wananchi waliomtuhumu kwa vitendo vya wizi.

Kamanda Msangi alisema kuwa tukio hilo limetokea Januari 12 majira ya saa 11 jioni ambapo kundi la wananchi wenye mawe na fimbo waliamua kujichukulia sheria mkononi baada ya kuwepo kwa madai kuwa marehemu alivunja kibanda cha biashara na kuiba.

Alisema hata hivyo marehemu alidaiwa kuwa alikuwa na mwenziye wakati wakitekeleza wizi huo ambapo alikimbia baada ya tukio hilo huku akiendelea kutafutwa na Jeshi la Polisi.


Post a Comment