Mtoto Agustino Sanga akiwa na jereha kubwa kifuani lililotokana na moto baada ya kumwagiwa maji ya moto na Kigogo wa CCM |
Mtoto Agustino akiwa katika maumivu makali baada ya kuishi na jeraha hili la moto kwa zaidi ya miezi 6 |
Mtoto Agustino ambaye alimwagiwa maji ya moto na kwa madai kuwa alikuwa akila chakula kingi na kuwapunja watoto wa kigogo wa CCM |
Mwandishi wa habari hizi Esther Macha akimfariji mtoto yatima Agustino ambaye alichomwa moto na bosi wake ambaye ni Mwenyekiti wa CCM. |
Mwandishi wa habari hizi Esther Macha akimfuta usaha mtoto Agustino ambaye alimwagiwa maji ya moto na Bosi wake aliyekuwa akimtumikisha kwa kumchungia ng'ombe na mbuzi. |
Msamaria mwema aliyemuokoa Agustino kwa kumnunulia dawa |
Bibi wa Agustino |
NA ESTHER MACHA,
MBARALI
SIKU zote tumezoea kuona baadhi ya wanasiasa na
viongozi wakiwa mstari wa mbele kupinga ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na
hata kupinga ajira kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Hali hiyo
imekuwa ni tofauti kwa Kigogo mmoja wa Chama Tawala CCM wilayani Mbarali mkoani
Mbeya ambaye mbali na kumtumikisha mtoto aliyechini ya miaka 18 bali pia
amemfanyia unyama na ukatili uliopitiliza kwa kummwagia maji ya moto kwa kile
kinachodaiwa kuwa mtoto huyo anakula sana.
Kigogo huyo ambaye
ni Mwenyekiti wa CCM Kitongoji cha Mahango kijiji cha Mageya kata ya Rujewa
wilayani Mbarali aliyefahamika kwa jina la Ziada Bakari Mwihesi anadaiwa
kummwagia maji ya moto mtoto Agustino Sanga(12) ambaye alikuwa akimtumikisha
kwa kufanya kazi za kuchunga mifugo yake kuanzia alfajiri hadi usiku bila kumpatia chakula cha uhakika.
Mtoto Agustino
ambaye ni yatima anayelelewa na bibi yake baada ya kufiwa na wazazi wake
huko wilayani Makete mkoani Njombe alianza kuishi na Mwenyekiti huyo wa chama mwaka 2011 akitokea wilayani Makete
mkoani Njombe ambapo Bibi yake kutokana na kutokuwa na uwezo alimkabidhi mama
huyo ili aishi naye huku akimsaidia kazi za kuchunga mifugo yake.
Akizungumza mkasa huo mbele ya mwandishi wa habari
hizi aliyefika kijijini hapo kufuatilia
taarifa za unyanyasaji dhidi yake, mtoto huyo alisema kuwa aliletwa nyumbani
kwa mama huyo mwaka 2011 na Bibi yake akitokea Wilayani Makete Mkoani Njombe
ili aweze kufanya kazi ya kuchunga ng’ombe kwa mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa tukio la kuunguzwa moto lilimtokea mwezi
Juni 2013 shambani kwa Mwenyekiti huyo eneo la Jangulutu majira ya usiku ambapo
Mwenyekiti huyo alianza kumsimanga kwa madai kuwa amekuwa akila chakula kupita
kiasi na kusababisha watoto wake
kutoshiba.
Mtoto Agustino
aliendelea kusema kuwa, mama huyo aliendelea kumsimanga na ghafla alichukua
maji yaliyoinjikwa jikoni yakiwa yamechemka kwa ajili ya kupika ubwabwa usiku huo na kummwagia kifuani na baadaye
kumfungia ndani huku akilia kwa uchungu.
“Nilipata uchungu mkubwa, nililia sana sikuwa na
msaada wowote usiku ule mama Yule alinifungia ndani, sikupata matibabu yoyote,’’aliongea
kwa uchungu mtoto Agustino.
Agustino
aliendelea kufafanua mkasa huo kwa kusema kuwa akiwa amefungiwa ndani mama huyo alikuwa
akisaga mifupa ya ng’ombe na kumpaka
katika jeraha la kidonda alichounguzwa na kwamba kila alipokuwa akimpaka ndipo
kidonda kilipozidi kutoa usaha.
Alisema akiwa
ndani Bibi yake alianza kumtafuta ndipo siku hiyo alipofika nyumbani kwa
Mwenyekiti huyo na kumuuliza alipo ambapo alimweleza kuwa mjukuu wake aliungua
moto alipokuwa akicheza karibu na moto.
Agustino
aliendelea kubainisha kuwa tangu alipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo mwaka
2011 hajawahi kupumzika na kwamba amekuwa akitumikishwa kama Punda kuanzia
alfajiri hadi usiku huku akipewa chakula kidogo.
Kwa upande wake Babu wa Mtoto huyo Method Ndelwa(55)
Mkazi wa Kitongoji cha Mahango alisema mtoto huyo baada ya kufika nyumbani hapo
alikuja mume wa Mwenyekiti aitwaye Seleleka Twasanga na kumuomba mtoto huyo awe
anamchungia ng’ombe na mbuzi shambani kwake.
Alisema tangu mjukuu wake alipoungua mwaka 2013 mwezi wa 6 hakuna
msaada wowote ambao unatolewa na familia ya Mwenyekiti na kwamba ameendelea
kuugulia na majereha yake bila kupatiwa matibabu ya uhakika.
“Mimi na Bibi wa wa mtoto huyu hatuna hali zetu
ni duni kipato chetu ni kidogo kama
mnavyoona kidonda cha mtoto kinatoa usaha na hapo mwanzo kilikuwa kinatoa funza,
mama mmoja Rukia Shomari alitusaidia kumnunulia dawa,’’alisema Babu wa mtoto
huyo.
Alisema kuwa hakuwa anajua utaratibu wowote wa kutoa
taarifa hizo kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Polisi na kwamba tangu
alipounguzwa moto walikuwa wakimuangalia tu mtoto huyo huku wakishindwa
kujua hatima yake.
“Tunaomba
mtusaidie kulifikisha hili ili jamii ijue kama mna uwezo wa kumsaidia mtoto
huyu tunaomba msaada wenu kumuokoa mtoto huyu’’,alisema Mzee Ndelwa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahango ambaye ndiye anayedaiwa kufanya unyama huo,Ziada Mwihesi alikana kumchoma moto mtoto huyo na kudai kuwa siku ya
tukio alipigiwa simu na mume wake aliyemtambulisha kwa jina la Seleleka kuwa
mtoto Agustino ameungua moto ndipo alipoondoka na kwenda shambani na
kumkuta mtoto huyo akiwa ameungua kifuani.
Hata hivyo
Mwenyekiti huyo anadai kuwa chanzo cha mtoto huyo kuungua ni kutokana na
kuota moto asubuhi wakati akipasha kiporo cha wali katika jiko la kuni na
kusema kuwa mtoto huyo alishaungua moto akiwa kwa bibi yake na kudai kuwa
hapo amekuja kuungua kwa mara ya pili.
Pamoja na
kufanya unyama huo Mwenyekiti huyo alionekana kutohitaji kutoa ushirikiano kwa
mwandishi wa habari hizi kwa kutoa majibu ya mkato wakati alipokuwa akiendelea
kuulizwa maswali juu ya kuchomwa moto kwa mtoto huyo ambapo pia
alikanusha kummwagia maji ya moto mtoto huyo kwa madai ya kumaliza chakula.
Naye Mume wa
Mama huyo Seleleka Twasanga alikiri kuungua kwa mtoto huyo na kudai kuwa yeye
alipata taarifa baada ya kupigiwa simu na jirani yake ambaye wapo jirani
shambani kwamba Mtoto Agustino ameungua moto ndipo alipoondoka na kwenda
shambani ili kujua chanzo cha tukio hilo.
Bw.Twasanga
alisema wakati anamchukua mtoto huyo kwa Bibi yake walifanya kama kubadilishana
na Bibi huyo ambaye alihitaji kila mwaka alimiwe shamba la heka mbili kwa
ng’ombe wakati mtoto Agustino akifanya kazi ya kulima na kuchunga Ng’ombe na
mbuzi shambani kwa Twasanga.
Akielezea zaidi mume wa mama huyo alisema aliendelea
kumlimia shamba bibi wa mtoto Agustino na kukiri kutomlipa chochote zaidi ya
bibi huyo kulimiwa shamba.
Chama Cha
Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kimekuwa katika harakati za kupinga ukatili
wa kijinsia ikiwemo unyanyasaji wa wanawake na Watoto.
Mkurugenzi wa
TAMWA Valerie Msokwa kupitia jarida lake linalotolewa na taasisi hiyo alisema kitendo
hicho ni ukiukwaji wa sheria ya Kimataifa ya haki ya mtoto ya mwaka 2009
iliyowekwa katika tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Mtoto linalotoa mwongozo
wa kulinda na kutambua haki za mtoto nchini.
Alisema watoto
wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya vitendo vya
unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa watoto katika maeneo mengi ya mijini
na vijijini.
Naye Diwani wa
Kata y Rujewa Bi.Gurzar Sabil alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo la kinyama la
mwenyekiti huyo alisema kuwa hana taarifa hiyo lakini aliahidi
kuwasiliana na Ofisa Ustawi wa jamii wilaya ya Mbarali ili waweze kwenda
nyumbani kwa mtoto waweze kumsaidia ikiwa ni pamoja na kumkamata mtuhumiwa.
Mara baada ya
Mwandishi wa habari hizii kuondoka wilayani humo Ofisa Ustawi wa Jamii wilaya
ya Mbarali Winifrida Mahali akiambatana na Mratibu wa Dawati la Jinsia wilayani
humo Christa Komba walifika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumchukua hadi kituo
cha Polisi.
Bi Mahali alisema kuwa walimfuata mtuhumiwa pamoja na
mumewe na kuwapeleka kituo cha polisi ambako walilala hadi asubuhi leo na
kufikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbarali ambako wamesomewa mashtaka ya
kujeruhi na wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana hadi Januari 29.
Post a Comment