Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa Saturnine Katanga akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake leo mchana. |
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa wamemzonga Ofisa wa Shirika la Nyumba ambaye alifika kufungua mlango wa duka hilo baada ya kuwafungia ndani wamiliki wa duka hilo kwa masaa matatu |
Duka la Vifaa vya Maofisini ambalo lilifungwa kufuri na wamiliki wa duka hilo wakiwa ndani. |
Mlango wa duka ukiwa umepigwa kufuri |
Ofisa wa NHC akiondoka eneo la tukio huku akikwepa kueleza chochote juu ya kadhia hiyo |
Umati wa watu ulikusanyika mbele ya duka la Vifaa vya maofisini mtaa wa Uhindi Jijini Mbeya leo asubuhi umeshuhudia mambo ambayo si ya kawaida baada ya watumishi wa Shirika la Nyumba NHC kumweka mahabusu kwa masaa matatu ndani ya duka lake mfanyabiashara Boniface Ishabakaki ndani ya duka lake kwa masaa matatu kwa kile
kilichodaiwa kuwa amechelewa kulipa kodi ya pango la chumba hicho ambacho
kinamilikiwa na shirika hilo.
Hali hiyo
ambayo ilisababisha umati wa watu kujaa nje ya duka hilo na kuhoji sababu za
NHC kuwaweka mahabusu wapangaji wake kinyume cha taratibu ilizusha taharuki
miongoni mwa wapiti njia na kusema kuwa huo ni ‘’Ukiukwaji wa Haki za Binadamu’’.
‘’Hii sio
haki kama mtu ameshindwa kulipa kodi zipo taratibu zinazopaswa kufuatwa,
mpangaji anapewa notisi na baadaye kuamriwa kuhama, sio kumuweka mahabusu kwa
masaa hayo,’’alisema mmoja wananchi aliyekuwepo eneo la tukio.
Nyumba hiyo
iliyopo katika Kiwanja namba 6 Kitalu namba 3 mtaa wa Lupa Uhindini Jijini
Mbeya imepangishwa na Shirika la Nyumba kwa mpangaji wake Ishabakaki ambaye
anafanya biashara ya duka la kuuza Vifaa vya Ofisini ‘’Stationary’’.
Wafanyakazi
wa Shirika la Nyumba walifika eneo hilo majira ya saa 3:00 asubuhi na kuweka
kufuri kwa nje huku mmiliki wa duka na wafanyakazi wake wawili wakiwa ndani ya
duka hilo.
Akizungumza
kupitia kwenye kioo cha dirisha la duka hilo ambalo halina madirisha ya
kuingiza hewa mmoja wa wafanyakazi wa duka hilo Cesilia Julius alisema kuwa
wafanyakazi hao wamefika hapo na kuongea na Bosi wake lakini baadaye wakatoka
nje na kufunga milango na kisha kuondoka zao.
Cesilia
ambaye alikuwa akisikika kwa mbali kutokana na dirisha hilo kutopitisha sauti
alisema kuwa wamefungiwa kutokana na madai kupitisha pango la mwezi huu.
Saa 6: 00
mmoja wa watumishi wa Shirika la Nyumba aliyefahamika baadaye kwa jina la
Khalfani Chaula ambaye ni Ofisa Mmiliki msaidizi wa shirika la Nyumba mkoa wa
Mbeya alifika dukani hapo na kufungua kufuri lililokuwa linaning’inia mlangoni.
Muda mfupi
baada ya kufunguliwa kwa kufuri hilo, mmiliki wa duka hilo Ishabakaki
alionekana akitoka nje huku akiwa anahema kwa nguvu na kujifuta jasho hali
ambayo ilionekana ni kama vile alipokuwa ndani ya mahabusu hiyo alikuwa akikosa
hewa.
Waliofungiwa
ndani ya duka hilo ni mmiliki wa duka Ishabakaki na wafanyakazi wawili Cesilia
Julius na Baron Boniface.
Hata hivyo
Ofisa huyo alipofuatwa kuulizwa sababu za kuwafungia watu ndani alisema kuwa
yeye si msemaji bali taarifa zote zitapatikana ofisini saa 8:00 mchana.
Waandishi wa
habari walisubiri hadi saa 8: 00 mchana na kuonana na Kaimu Meneja wa Mkoa
Saturnine Katanga ofisini kwake aliyeambatana na wasaidizi wake wawili Amos
Manyama ambaye ni Ofisa mmiliki wa mkoa na msaidizi wake Chaula.
Alipotakiwa
kueleza kama zipo sheria za kumfungia mpangaji ndani ya chumba chake Katanga
alisema kuwa hakuna sheria hiyo bali tatizo hilo limetokana na mpangaji huyo
kutolipa pango la nyumba la mwezi Januari sh. 222,450.00.
Alipobanwa
zaidi kuhusu sakata hilo na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Ofisa
aliyewafungia ndani wafanyakazi wa Stationary hiyo, Katanga alisema suala hilo
litashughulikiwa kiofisi.
Naye mmiliki
wa duka hilola vifaa vya Ofisini ambaye ana matatizo ya kisukari na kupumua kwa
shida Ishabakaki alisema kuwa alikuwa akijisikia vibaya alipokuwa amefungiwa
ndani ya duka hilo kutokana na kupumua kwa shida.
Alisema
anasumbuliwa na tatizo la kisukari na kwamba iwapo wangechelewa kufungua kwa
saa moja angeweza kuzimia kwa kupoteza pumzi.
Post a Comment