Ads (728x90)


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya CCM mkoa iliyopo  Sokomatola Jijini Mbeya.

Nape Nnauye
Ni kama vile anasema ''CHADEMA wasitafute mchawi wanakumbatia ukanda udini na ukabila hili litawagharimu''
Baadhi ya waandishi wa HABARI wakiwa katika kikao na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye katika ukumbi wa ofisi za mkoa za chama hicho Sokomatola Jijini Mbeya.


Nape Nnauye akiwa na Katibu wa Mkoa wa CCM Maganga Sengelema(kulia) na Meya wa Jiji la Mbeya Athanas Kapunga(wa pili kutoka kulia)
Na Rashid Mkwinda

 CHAMA cha Mapinduzi CCM kimesema kuwa CHADEMA hakipaswi kuwatafuta wachawi kutokana na mgogoro ulioibuka hivi karibuni wa kufukuzana uongozi bali wanapaswa kuangalia tatizo walilonalo la kukumbatia udini, ukabila na ukanda.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Mbeya leo asubuhi Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye amesema kuwa chama hicho kilijisahau mara baada ya kimeanza kupata umaarufu kwa kuanza kuwabeza baadhi ya wanachama wao kwa kuwagawanya kwa makundi kutokana na itikadi zao za dini, ukabila na ukanda.

Amedai kuwa chama hicho kimekuwa kikikumbatia baadhi ya watu wa kabila fulani na kuwatenga watu wasio kuwa wa kabila hilo na hivyo kuendelea kuibua migogoro na kufukuzana uongozi na uanachama jambo ambalo amedai kuwa linadhoofisha demokrasia ndani ya vyama vya upinzani.

Amesema hakuna chama cha kisiasa ambach hakina migogoro na kwamba migogoro inayokuwepo ndani ya chama tawala inamalizwa kwa njia za busara tofauti na ilivyo kwa CHADEMA ambao badala ya kuketi chini kumaliza tofauti zao kwa njia za mazungumzo wanafukuzana uanachama na kutumia gharama kubwa kuzunguka nchi nzima kumuelezea mtu mmoja.

‘’Hili jambo litakigharimu chama hiki, itafika mahala upinzani utakufa  jambo ambalo sisi  ‘’CCM’’ hatupendi litokee, unaona sasa, wanatumia gharama kubwa kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kummaliza ZITTO badala ya kuimarisha chama,’’amesema.

Nape ameendeleza madai yake kuwa moja ya chuki wanazopandikiza zinazoashiria udini ni kitendo cha maandamano ya CHADEMA kutengeneza jeneza lenye msalaba wakiwa na maana kuwa wanamzika Zitto Kabwe jambo ambalo linatafsiri kejeli dhidi ya mtu na dini yake.

Amefafanua kuwa migogoro ndani ya vyama haikosekani na  kuwa hata ndani ya CCM kuna migogoro ambayo inamalizwa kwa busara na kwamba iwapo CCM ingekuwa ina desturi ya kufukuza vijana machachari hata yeye ‘’NAPE’’ angefukuzwa siku nyingi kwa kuwa alikuwa ni mkorofi ndani ya chama.

Amesema kuwa vyama vya siasa vinapaswa kujenga tabia za kuvumiliana ili kuimarisha demokrasia na kwamba vijana wanaojitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya vyama hawapaswi kuzibwa midomo kama ilivyofanyika CHADEMA kutokana na Zitto kuweka bayana nia ya kuwania Uenyekiti.

Ammesema matatizo yanayovikumba vyama hivyo ni uroho wa madaraka na kwamba kila wanapofikia katika mafanikio wanaanza kubaguana na kutimuana jambo ambalo linavifanya vyama hivyo kuwa na safari ndefu kuelekea katika demokrasia ya kweli ndani ya vyama vyao.

Ametolea mfano katika vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF ambavyo baada ya kuonekana vina nguvu viongozi wa juu wakaanza kuwatenga na hata kuwajengea mizengwe ya kuwatimua wenzao akina Mabere Marando (NCCR Mageuzi) na Hamad Rashid (CUF) na kwamba wimbi hilo limeingia CHADEMA kwa sasa.

Nape yupo mkoani Mbeya katika maandalizi ya sherehe za kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa chama hicho ambayo yanatarajiwa kufanyika Kitaifa Mkoani Mbeya Februari 2 na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete.




Post a Comment