Ads (728x90)

Eva Kleruu akiwa na Mwandishi wa makala haya alipokuwa Mbeya
Eva Kleruu na Amani Mwamwindi baada ya kukutana

Eva na Amani

MWEZI March utakumbukwa kuwa ni mwezi wa historia kwa familia mbili za aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Wilbert Kleruu na Mkulima wa Mkungugu Isimani mkoani Iringa Mzee Said Mwamwindi ambao wote kwa sasa ni marehemu.

Dkt. Kleruu aliuawa kwa kupigwa risasi na Mzee Said Mwamwindi ilhali Mzee Mwamwindi aliuawa kwa kunyongwa baada ya mahakama  kujiridhisha kuwa alifanya kosa la mauaji.
Imepita miaka mingi baada ya muda mrefu familia hizi kutengena ilhali wakati tukio hili la mauaji linatokea watoto wa wazee hawa walikuwa wangali ni wadogo.
Eva Kleruu na Amani Mwamwindi ni wazaliwa wa kwanza kwa familia za Dkt. Kleruu na Mkulima Said Mwamwindi.
Alikuwa ni Eva Kleruu aliyeibukia mkoani Mbeya ambapo katika utambulisho wake alijitaja kuwa ni mtoto wa kwanza wa Dkt.Kleruu na kwa kufuatilia historia ya Dkt. Kleruu na jinsi kifo chake kilivyotikisa anga la mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla mwandishi wa Blog hii alijaribu kunmdodosa mtoto wa Dkt. Kleruu na kuelezea hisia zake juu ya kile kilichojiri miaka 43 iliyopita na nia yake ya kukutana na mtoto wa kwanza wa Mwamwindi ambaye ndiye Meya wa Manispaa ya Iringa.
Blog hii ilifanya jitihada za kutafuta mawasiliano ya Meya wa Iringa Mwamwindi ili kuziunganisha familia hizi ambapo kwa jitihada za Blog washirika ya Mkoa wa Iringa ya Frank Leonard wanafamilia hawa walikutana na kueleza hisia zao kama zilivyorekodiwa na mtandao wa frankleonard.blogspot.com. kama ifuatavyo
SIMANZI na machozi yalibubujika wakati familia mbili za Dk Wilbert Kleruu na Said Mwamwindi zilipokutana juzi mjini Iringa kwa ajili ya maridhiano yaliyoondoa tofauti zao.
Dk Kleruu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa Desemba 25, 1971 na Mamwindi aliyekuwa mkulimaa maarufu wa mahindi katika kijiji cha Isimani, wilayani Iringa.
Tangu kifo cha mkuu wa mkoa huo kitokee miaka 43 iliyopita, kabla ya kukutana juzi, familia hizo mbili hazikuwahi kukutana.
Watoto wa kwanza wa familia hizo, Eva Kleruu (56) na Amani Mwamwindi (63) ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa kwa niaba ya familia zao walikutana na kufanya maridhiano hayo.
Maridhiano hayo yalifanyika katika ofisi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, mjini Iringa juzi.
Mtoto wa kwanza wa Dk Kleruu, Eva alisema; “tumekuwa tukikumbuka historia ya maisha yetu na jinsi marehemu baba yetu alivyouawa.”
Huku akitetemeka na kuongea huku akitokwa na machozi, Eva alisema tukio hilo lilikuwa likiifaanya familia ya Dk Kleruu iogope kuja Iringa.
“Pamoja na hofu hiyo niliweka nadhiri kwamba ipo siku nitafika Iringa na kutembelea sehemu ambayo marehemu baba yangu aliuawa katika shamba la Mwamwindi,” alisema.
Alisema baada ya kutembelea eneo hilo alipanga kukutana na watoto wa Said Mwamwindi ili kuweka maridhiano yatakayofanya watumie tukio lile la mauaji ya Dk Kleruu kuwaunganisha.
Kwa kupitia Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, Eva alisema waliweza kukutana na kufanikisha azma yao hiyo.
“Ile siku imefika na leo nimekutana na mtoto wa kwanza wa Said Mwamwindi, Meya Amani Mwamwindi na kumaliza tofauti zao zilizosababishwa na mauaji hayo,” alisema.
Eva alisema baada ya kukutana na Mwamwindi na kuziweka kando tofauti za kihistoria baina ya familia zao anajihisi ni sehemu ya maendeleo ya mkoa a Iringa.
Alisema kwa kupitia kampuni yao ya Power Supply Cooperation wako tayari kuhakikisha kwamba miradi midogo ya uzalishaji umeme inajengwa katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa ili kufikisha nishati hiyo kwa watu wengi zaidi.
Katika kikao chao hicho kilichomtoa machozi pia Amani Mwamwindi, walikubaliana kukutana na familia zao na kutoa taarifa ya maridhiano hayo.
Kwa upande wake Mwamwindi aliyekuwa akiongea kwa hisia inayoashiria uchungu fulani alisema; “nimefurahishwa kukutana na dada yangu huyu na kuondoa tofauti zetu za kihistoria.”
Mwamwindi alisema; “kabla na baada ya tukio tukio hilo litokee miaka 43 iliyopita familia zetu zilikuwa hazijuani vizuri. Na sisi tulikuwa watoto, leo tunakutana tukiwa watu wazima, ni jambo la kushukuru mwenyezi Mungu.”
Alisema baada ya kikao chao hicho watapanga siku nyingine ambayo kwa pamoja familia hizo mbili zitakutana zikiwa na wawakilishi wengi zaidi.(STORI YA NYONGEZA NA PICHA KWA HISANI YA BLOG YA FRANK LEONARD)

Post a Comment

  1. Hongereni sana kwa hili kuna mengi ya kujifunza kutokana na hili, mtakuwa waelekezi wazuri kama si waalimu wa kufanya maridhiano kwa watu walio / wanaohasimiana

    ReplyDelete
  2. Amani na kusameheana ndo jambo zuli

    ReplyDelete
  3. Amani na kusameheana ndo jambo zuli

    ReplyDelete
  4. Amani na kusameheana ndo jambo zuli

    ReplyDelete