Ads (728x90)

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla akizungumza na wajumbe ya kamati ya ulinzi na usalama wilayani Kyela leo



MKUU wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi mkoani Mbeya kutenga siku moja ya Alhamisi kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Makalla alitoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye mkutano uliowahusisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, madiwani,maofisa  watendaji wa kata ,viongozi wa vyama vya kisiasa, viongozi wa dini, machifu, wazee maarufu na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kyela.
Aidha Makalla amewapongeza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Mbeya kwa jitihada za kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu na kuwa tangu Machi 27 mkoa wa Mbeya hauna mgonjwa hata mmoja wa kipindupindu.
‘’Niliporipoti mkoani Mbeya Machi 17 niliwaagiza MADC na wakurugenzi kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu, tangu Machi 27 hadi sasa hakuna mgonjwa hata mmoja wa Kipindupindu,’’alisema Makalla.
Katika kuzingatia hali ya usafi Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya Makalla aliwataka wananchi kuzingatia kanuni za Afya kuanzia ngazi ya kaya na kuhimiza kila kaya iwe na choo kizuri.
Pia katika kuhakikisha tatizo la madawati linakoma mkoani Mbeya amewaomba Wabunge, madiwani na wananchi kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha tatizo la madawati linaisha ifikapo Mei 31 mwaka huu.

Post a Comment