Ads (728x90)

Wananchi na wadau wa zao la kahawa wilayani Mbozi wakiwa wamesimama mlangoni kumzuia Waziri wa Kilimo Profesa Maghembe asiingie ukumbini kwa madai kuwa ni mamluki aliyenunuliwa ili kuwatetea walanguzi wa kahawa.
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe akitoka katika mkutano wa wadau wa zao la Kahawa wilayani Mbozi leo mchana
Profesa Maghembe akizungumza na  Waandishi wa Habari nje ya Ukumbi wa mikutano baada ya kikao na Wakulima wa kahawa.
Profesa Maghembe nje ya Ukumbi akiwa na Mkuu mkoa wa Mikutano
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akisisitiza jambo katika kikao cha Wadau wa Kahawa wilayani Mbozi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Bw. Anderson Kabenga akizungumza kwa hisia mbele ya Profesa Maghembe kutokana na kukosa umakini wa utendaji dhidi ya wakulima
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbozi Aloyce Mdalavuma akielezea hisia zake juu ya matatizo yanayowakumba wadau wa Kahawa na namna ambavyo wizara imekosa umakini katika kufuatilia matatizo ya wakulima
Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi akimshushia makombora Waziri wa Kilimo juu ya matatizo ya wakulima wa kahawa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbozi Helick Minga akilaumu utendaji wa Wizara ya Kilimo kutokana na ubabaishaji dhidi ya mipango ya utekelezaji dhana ya Kilimo Kwanza
Mkuu wa wilaya ya Mbeya Evance Balama akielezea matatizo ya ununuzi wa kahawa mbichi yanavyoathiri wakulima 




 Na, Mwanafasihi Wetu, Mbozi
SAKATA la ununuzi wa kahawa mbichi mkoani Mbeya limechukua sura mpya baada ya wakulima na wadau wa zao la kahawa kumtaka Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe kuwajibika kwa kuwa ameshindwa kutekelezaa ilani ya chama chake anachokiongoza kwa madai ya kukumbatia wanunuzi wanaowanyonya wakulima.

Wananchi na wadau wa kilimo walifikia hatua hiyo baada ya kuibuka madai ya  Waziri huyo kununuliwa na baadhi ya makampuni yanayodaiwa kuwanyonya wakulima, ambapo aliwasili wilayani Mbozi na wakulima kumzuia kuingia katika ukumbi wa mikutano kwa madai kuwa ni mamluki, ambapo hata hivyo aliokolewa na Mkuu wa mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro aliyewasihi wananchi hao kutulia.

Wakizungumza kwa namna ya kumshambulia ndani ya Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi baadhi ya viongozi waliokuwepo walisema kuwa nafasi aliyonayo ya Waziri wa Kilimo inawezekana kuwa haimfai kutokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo katika matatizo ambayo yanaigusa jamii moja kwa moja pamoja na kuwepo kwa kauli mbiu ya serikali ya Kilimo Kwanza.

''Hii Wizara itakuwa ngumu kwako na ugumu wenyewe utajipa  mwenyewe,unatuchanganya wakulima katika suala ambalo liko wazi kabisa, wewe umekuwa tatizo katika maslahi ya wakulima...tatizo la pembejeo wewe!!! tatizo la ununuzi wa kahawa mbichio wewe!!!sisi ndio wakulima, inaonekana wizara imekushinda'' alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Bw.Anderson Kabenga Maarufu kwa jina la Ndombolo ya Solo.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbozi Bw. Aloyce Mdalavuma alisema kwa hasira kuwa kuwepo kwa viongozi wa aina ya Waziri wa Kilimo kunasababisha kuwepo kwa serikali legelege ambayo inatupiwa mfano mbaya kwa wananchi.

''Ninyi mpepewa dhamana ya kusimamia uadilifu inaonesha wazi kuwa uadilifu katika uitendaji hakuna...mnaifanya Mbozi ni mahala pa kujifunzia sisi Mbozi hatutaki, badala ya kushughulikia suala la msingi la tatizo la Pembejeo kwa wakulima mnakuja kujadili suala la ununuzi wa kahawa mbichi...hili suala liko wazi kahawa mbichi haimsaidii mkulima,''alisema na kuongeza.

''Mnatupa shida sana tunapokaa na wananchi mimi ndiye Mwenyekiti wa CCM hapa...serikali legelege huzaaa viongozi legelege''alisisitiza kwa hasira Bw. Mdalavuma.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Mashariki Bw.Godfrey Zambi alimwambia Waziri Maghembe kwamba katika suala hili usiwepo ushabiki wa baadhi ya watu kuona kuwa kuna mtazamo ambayo si sahihi bali alisema kuwa jambo la msingi ni kuangalia sheria na kanuni zinasemaje juu ya ununuzi wa kahawa mbichi.

Alisema kuwa ununuzi wa kahawa mbichi unamnyonya mkulima hivyo yeye kama mbunge anakemea kitendo ca kuendelea kuruhusu baadhi ya makampuni kununua kahawa mbichi na kuwa kuanzia sasa serikali iondoe leseni ya ununuzi wa kahawa mbichi.

''Itakuwa sisi ni wendawazimu kukubali kuwepo kwa ununuzi wa kahawa mbichi...narudia swali langu ambalo niliwahi kukuuliza bungeni na kuhusu msimamo wa serikali kununua kahawa mbichi....ulisema kuwa serikali hairuhusu ununuzi wa kahawa mbichi...leo hii mwanasheria wako anasema kulikuwa na kanuni ya dharura kuruhusu hili...mnatuchanganya wakulima,''alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Helick Minga alisema kuwa,upo uwezekano mkubwa wa Waziri kushindwa kumudu kufanya Wizara hiyo na kuwa iwapo Waziri atasimamia kuendelea ununuzi wa kahawa mbichi yuko tayari kumuona Rais Jakaya Kikwete na kwamba inawezekana uwezo wa Waziri huyo ndani ya Wizara hiyo ni mdogo. 

Naye Mkuu wa Mkoa alisisitiza msimamo wa mkoa wa Mbeya kutoruhusu ununuzi wa kahawa mbichi na kusema kuwa wadau wa halmashauri za wilaya zinazolima zao hilo zimeweka msimamo huo kwa maslahi ya wakulima.

''Biashara ya kukata kichwa inaua wakulima..sisi hatukubali ununuzi wa kahawa mbichi na msimamo wetu huu una nia njema kwa wakulima..tunasimamia wakulima wapate bei nzuri, alisema Bw. Kandoro.

Hata hivyo baada ya masmbalizi kutoka maeneo mbalimbali Profesa Maghembe alisema kuwa lengo lake lilikuwa ni jema kupata uwakilishi kutoka makundi ya wananchi na wadau na kuwa tatizo alilokuwa nalo dhidi ya wakulima ni kuwa na bei ndogo ya uuzaji wa kahawa.

''Bei ya kahawa ni ndogo..bei za wakulima zisimamiwe kwa nguvu zote na tuimarishe vyama vya ushirika, wizara haina tatizo na maamuzi ya vikao halali,''alisema.




Post a Comment