Ads (728x90)







Dar es salaam
Jitihada za kutatua mgogoro na mgomo wa Madaktari nchini ambazo zilidhamiriwa kufanywa na Waziri mkuu Mizengo Pinda leo zimegonga mwamba baada ya madaktari hao kugoma kuhudhiuria kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu katika ukumbi wa Karimjee.
Hatua hiyo ya Madaktari imehitimisha kile kilichoelezwa kuwa serikali bado imeshindwa kutatua mgogoro wao wa muda mrefu na serikali kutosikiliza kilio cha wafanyakazi wa sekta ya afya nchini.
Katika ukumbi wa Karimjee ni baadhi ya watumishi wa taasisi za serikali pekee ndio waliohudhuria ambapo hakuna hata Daktari mmoja aliyehudhuria hata mara baada ya kuingia ukumbini Waziri Mkuu.
Kufuatia kutotokea kwa madaktari hao ambao walitarajiwa kukutana na Waziri Mkuu ili kusikiliza madai yao, Waziri Pinda alitangaza rasmi kuwa iwapo madaktari hao watagoma kuingia kazini kesho siku ya Jumatatu watakuwa wamejiondoa wenyewe katika utumishi wa umma.
‘’Madaktari hawa tunawataka kesho waingie kazini iwapo watashindwa kufika kazini kesho watakuwa wamejiondoa wenyewe kuwa watumishi wa umma’’alisema Bw. Pinda
Waziri Mkuu alitumia muda wake kuzungumza na watumishi wa taasisi mbalimbali za serikali na kudai kuwa serikali itaingia katika changamoto katika kipindi hiki cha mpito na kuwa hata hivyo bado serikali inatoa fursa ya kukutana na madaktari hao kutafuta ufumbuzi wa madai yao ambayo amedai kuwa ni ya msingi.

Post a Comment