Mhandisi Gabriel Kalinga, mratibu wa Kitaifa mradi wa Bonde la Mto Songwe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Watumia Maji wa Bonde la Mto Songwe, (JUWABOSO) |
Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dkt. Michael Kadeghe akizindua Jumuiya ya Watumia maji wa bonde la Mto Songwe |
KATIKA hali isiyo ya kawaida serikali ya
Kijiji cha Idiwili kilichopo kata ya Iyula wilayani Mbozi mkoani Mbeya imegomea
mpango wa utunzaji wa mazingira unaoendeshwa na Bonde la Ziwa Nyasa kwa madai
kuwa wamekuwa wakiendesha kilimo katika vyanzo vya maji tangu enzi za mababu.
Hali hiyo imeibuka mwishoni mwa wiki
wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Watumia Maji wa Bonde la Mto Songwe,(JUWABOSO)
uliofanyika katika kijiji cha Nyimbili kata ya Iyula wilayani Mbozi.
Awali ilielezwa kuwa mara baada ya
wataalamu wa utunzaji wa mazingira na wahifadhi wa bonde la mtu Songwe kutembelea
katika kijiji cha Idiwili kwa nia ya kuwahamasisha wakazi wa maeneo hayo juu kuacha
kulima katika vyanzo vya maji walisema kuwa hawako tayari kuacha kilimo kwa
kuwa kinawanufaisha.
‘’Sisi tulifika pale kuwahamasisha uhifadhi
wa mito na utunzaji wa mazingira, wenzetu wakiongozwa na Mwenyekiti wa kijiji cha
Idiwili waligoma kabisa katika utunzaji wa vyanzo vya maji,’’alisema Ofisa
Maendeleo ya Jamii wa Bonde la Ziwa Nyasa Bi.Mishi Salim Kombo.
Bi. Kombo alisema kuwa kijiji cha Idiwili
kina vyanzo vingi vya maji ambayo yanapita katika mto Songwe kuelekea Ziwa
Nyasa na kwamba wananchi wake wanaharibu vyanzo kwa kuchimba madini ndani ya
mto hali ambayo inasababisha mto kuhamahama mara kwa mara.
Kwa upande wake Ofisa wa Maji wa Bonde la
Ziwa Nyasa Witgal Nkondola alisema kuwa changamoto walizokutana nazo waratibu wa Bonde
la Ziwa Nyasa ambao mto Songwe unaingiza maji katika Ziwa hilo, serikali ya
kijiji cha Idiwili imekuwa kikwazo cha harakati za utunzaji wa mazingira na
uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Alisema kuwa wamekuwa katika harakati za
kuhamasisha wananchi wa vijiji mbalimbali kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na
kutolima katika vyanzo vya maji ambapo Mwenyekiti wa kijiji cha Idiwili amekuwa
kikwazo hivyo wamechukua hatua za kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri
na mkuu wa wilaya kwa ufuaatiliaji.
Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa
Wilaya ya Mbozi Dkt.Michael Kadeghe alisema kuwa serikali ya wilaya ya Mbozi
itafuatilia suala hilo kwa kumuita Mwenyekiti wa kijiji na Ofisa mtendaji wake
ili kupewa elimu juu ya matumizi na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Post a Comment