MATUMAINI YA WAFANYABIASHARA WA SOKO
LA MWANJELWA LILOTEKETEA KWA MOTO YAYEYUKA .
-Ni baada ya mkandarasi
kuvunja mkataba na kuitia halmashauri hasara ya mabilioni.
DALILI za kumalizika kwa soko la
Mwanjelwa lililogharimu zaidi ya sh. bilioni 13 ambalo linatarajiwa kutumiwa na
wafanyabiashara wanaokadiriwa
1000,zinaonekana kugonga mwamba baada ya mkandarasi aliyekabidhiwa kujenga soko
hilo kuvunja mkataba.
Soko la Mwanjelwa liliungua Disemba
2006 na kusababisha hasara kubwa ambapo
wafanyabiashara waliokuwa wakilitumia soko hilo walihamishiwa katika soko la
muda katika uwanja unaomilikiwa na Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo Nchini (SIDO).
Hatua ya Mkandarasi huyo kampuni ya
Tanzania Building Works kuvunja mkataba unadaiwa umetokana na msuguano uliopo
baina yake na mmiliki wa Soko hilo ambaye ni Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani
wa Halmashauri hiyo hivi karibuni, wajumbe wa kikao hicho walihitaji kupewa
taarifa za maendeleo ya ujenzi wa soko hilo ambao tangu kuanzishwa kwake
limekuwa likikumbana na malumbano ambapo mkataba wa awali wa soko hilo
ulitakiwa kuishia mwaka 2010.
Kwenye kikao hicho Meya wa Jiji la
Mbeya Bw.Athanas Kapunga alimzuia Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Jiji Dkt.Samwel
Lazaro kutoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa soko hilo kwa kile
kilichoeleza kuwa kinaweza kuibua maswali mengi kutoka kwa madiwani ambao
walihitaji kupewa taarifa hizo.
Imeelezwa kuwa msuguano huo
umetokana na mkandarasi kushindwa kukabidhi soko kulingana na mkataba wake
pamoja na kulipwa fedha sh.bilioni 10.6 ambazo ni sehemu ya malipo ya kati ya
sh.bilioni 13 ambazo ndizo gharama halisi ya ujenzi wa soko hilo la kisasa
lenye ghorofa tatu.
Aidha ujenzi wa soko hilo umedaiwa
kuiingizia hasara halmashauri ya Jiji hilo ambapo katika kamati ya Bunge Hesabu
za Serikali za mitaa(LAAC) jambo hilo liliibuliwa na kuelezea sababu za
kukwamisha mradi huo wa soko ambalo likimalizika linaweza kuhudumia
wafanyabiashara zaidi ya 3000.
Katika taarifa ya (LAAC) halmashauri
ilimlalamikia Mkandarasi kukiuka sheria za mkataba ambapo kila alipokabidhiwa
fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa soko hilo inadaiwa kuwa alikuwa
akitumia fedha hizo kwa kuendeleza miradi mingine inayoendeshwa na kampuni hiyo
mahala pengine.
Awali ujenzi wa soko hilo
ulitarajiwa kutumia jumla ya miezi 18 baada ya kuanza kutekelezwa kwa mradi huo
Februari 25 mwaka 2010 na kukamilika Agosti 25 mwaka 2011.
Pamoja na mkandarasi huyo kushindwa
kutekeleza mradi huo kwa wakati, Halmashauri ya Jiji ilimpa muda wa ziada kwa
awamu tatu za wiki 20 ambapo alishindwa kukamilisha hadi Juni 19 mwaka huu
alipoandika barua ya kuvunja mkataba.
Kwenye barua yenye kumbukumbu
SAM/828/RET ya Julai 19, 2013
inamtaarifu mmiliki( Halmashauri ya Jiji) kusudio lake la kuvunja mkataba kwa
kile alichodai kunyimwa nyongeza ya muda wa ziada wa miezi 9 ili amalizie
asilimia 80 ya ujenzi wa soko hilo na kulikabidhi.
Kwa upande wake Halmashauri ya
Jiji iliridhia ombi la kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi wa soko hilo kwa barua
yenye kumbukumbu namba MD/MM/MBEYA/152/2013 ya Julai 25 na kueleza kuwa
inchokisubiri ni taratibu za kisheria ili kukubali kuvunja mkataba huo.
Katika sehemu ya barua ya
halmashauri ya jiji imeeleza hatua zilizochukuliwa baada ya muda wa makubaliano
kumalizika Julai 25 ambapo Halmashauri ilipokea utaratibu wa hatua
zinazoendelea wakati wa uvunjaji wa mkataba kutoka kwa mkandarasi kutakiwa
kuweka walinzi eneo la ujenzi ili kulinda mali zisitoroshwe.
Imeelezwa kuwa hatua ya Halmashauri kusitisha
mkataba wa ujenzi unaweza kuiongezea gharama halmashauri ambapo italazimika
kutumia ziada ya sh bilioni 3 ikiwa ni ongezeko la za gharama halisi ya sh.
bilioni 6 za kumalizia mradi huo.
Ongezeko la gharama kwa Halmashauri
ya Jiji litatokana na kutangaza upya zabuni ya kumpata mkandarasi mpya
atakayechukua kazi ya kumalizia asilimia 20 ya ujenzi iliyobaki.
Hasara nyingine ambayo itaigharimu
halmashauri ya Jiji baada ya kukubali kuvunjwa kwa mkataba na kumtafuta
mkandarasi mpya ni pamoja na kumlipa mkandarasi mshauri wa kampuni ya MD ya
Jijini Dar es salaam kiasi cha Sh. bilioni 1.2.
Inaelezwa kuwa hali hiyo itasababisha
Halmashauri kupangisha wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa katika soko hilo
ili kupata fedha za kufidia ongezeko la gharama za kumalizia ujenzi wa soko
hilo na kuwanyima fursa wafanyabiashara ambao ni wahanga wa soko lililoungua.
Post a Comment