-CHUNYA-
Baadhi ya wakazi wa Chunya mkoani Mbeya wakiwa katika makundi kujadili Rasimu ya Katiba Mpya
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Chunya wakiwa katika mjadala wa Rasimu ya Katiba Mpya |
WACHANGIAJI
katika rasimu ya Katiba mpya wilayani Chunya mkoani Mbeya wamependeleza kuwa
Mwenge wa Uhuru, uwekwe makumbusho na uwe ni sehemu ya Nembo za Taifa badala ya
kuiingizia gharama serikali kwa
kukimbizwa kila mwaka.
Wakichangia
katika mkutano wa kuchangia Rasimu ya Katiba mpya ulioitishwa na taasisi isiyo
ya kiserikali ya Kituo cha Msaada wa Kisheria na Unasihi(CHULECU) katika mji
mdogo wa Mkwajuni wilayani humo, wajumbe wa mkutano huo walipendekeza kuwa
mwenge huo uwekwe katika Jumba la Makumbusho ya Taifa ili iwe kumbukumbu kwa
vizazi vijavyo.
‘’Tunaomba
mwenge wa Uhuru uwekwe makumbusho ya Taifa, kila mwaka unakimbizwa ukiwa na
ujumbe ambao mwisho wake hauna utekelezaji, unagharimu fedha nyingi za walipa
kodi, matunda yake hayaonekani,’’alisema Bw.Bahati Komba mkazi wa kata ya
Mbuyuni.
Alisema kuwa
hata hivyo pamoja na mwenge huo kuitwa ni Mwenge wa Uhuru tafsiri yake
imepotoshwa kwa kuwa uliwashwa mwaka 1961 wakati Tanganyika ilipopata Uhuru
wake na kwamba badala yake mwenge huo unawakilisha pande mbili za Tanganyika na
Zanzibar.
‘’Tuwekwe
wazi kuwa huu ni Mwenge wa Uhuru wa Tanganyika mwaka jana uliwashwa Zanzibar
ambako Uhuru wao ni mwaka 1964, kama
tumeamua uwe ni mwenge wa pande zote basi uitwe Mwenge wa Taifa na uwe ni
sehemu ya nembo za Taifa,’’alisema Bw. Komba.
Alisema kati
ya alama za Taifa ambazo ni Bendera na Wimbo wa Taifa Mwenge nao uwe ni sehemu
ya alama hizo ambao utahifadhiwa katika makumbusho na kuenziwa kama
zinavoenziwa kumbukumbu zingine za nchi yetu.
Alisisitiza
kuwa dhana ya Mwenge huo ni kuleta amani pasipo na matumaini kuondoa chuki pale
penye dharau lakini hata hivyo pamoja na ujumbe mzuri wa Mwenge hakuna matokeo
wala mabadiliko yoyote yaliyotokea mara baada ya Mwenge huo kumaliza mbio zake
hivyo ni vyema ukapumzishwa na ukawekwa katika historia.
Naye Bi.
Margreth Sigereti mkazi wa kijiji cha Mkwajuni alisema kuwa iwapo kuna haja ya
kuendelea kuwa na Mwenge huo basi uwekwe Mwenge bandia ambao hauhitaji gharama
za mafuta na kwamba gharama kubwa za mafuta ya mwenge zielekezwe kwenye huduma
za kijamii kama vile elimu, afya, maji na miundombinu.
Bi. Sigereti
alisema kuwa miradi mingi iliyowekwa mawe ya msingi na mwenge imekufa na
haijaendelezwa hadi sasa na kwamba inawezekana dhana ya Mwenge inatumika kwa
ajili ya watu kujinufaisha kutokana na kuanzisha miradi hewa ambayo haina tija
kwa wananchi.
Kwa upande
wake mkazi wa kijiji cha Mangala aliyejitambulisha kwa jina la Justasi Wihege
alisema kuwa watendaji wabovu ndio wanaosababisha Mwenge wa Uhuru uonekane
haina manufaa kwa wananchi na kwamba ni muhimu kwa watendaji wabovu kumulikwa
na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kuweka nidhamu ya utumishi bora.
Naye Bw.
Festo Mambwe mkazi wa kijiji cha Mkwajuni alisema kuwa, kumekuwa na dhana ya
vitisho juu ya Mwenge wa Uhuru kiasi cha kuupa hadhi kubwa ambayo inawajengea
hofu watendaji ilhali ukweli ni kuwa mwenge huo unatumia fedha nyingi za walipa
kodi bila matokeo ya matumizi ya mbio za Mwenge kuwekwa bayana.
Wachangiaji
hao walishauri kuwa iwapo serikali itaona ni lazima kuwepo kwa mbio za Mwenge,
kuwekwe uwazi wa matumizi yake ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji ya miradi
mbalimbali iliyofunguliwa na mbio za Mwenge kote nchini na gharama
zilizotumika.
xxxxMJINI MBEYA WANAHABARI NAO WALIPATA FURSA YA KUKETI PAMOJA NA KUJADILI RASIMU YA KATIBA MPYA KAMA INAVYOONEKANA PICHANI
Wanahabari Mbeya wakinyoosha mikono kuafikiana jambo na kupitisha uamuzi wa kuondolewa kwa vifungu juu ya Uhuru wa kupata na kutoa habari baada ya kujadili kwa kina Rasimu ya Katiba mpya kwenye vifungu ambavyo vinanyanyasa utendaji kazi wa wanahabari nchini
Post a Comment