CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jijini Mbeya kimetoa onyo kwa viongozi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kutotumia jina lao kwa propaganda za kuvuta wananchi kwenye
mikutano yao na kwamba wakiendelea kufanya hivyo chama hicho kitaanzisha vurugu
katika mikutano ya CCM.
Akizungumza
katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hotel ya Mbeya Peak jana
Mwenyekiti wa CHADEMA Jiji la Mbeya Bw.John Mwambigija alisema kuwa CCM imekuwa
ikiwalaghai wananchi kwamba kuna vigogo
wa CHADEMA waliojiunga na CCM ili kujaza watu kwenye mikutano yao.
Alisema kuwa
katika mkutano wa Agosti 8 uliohutubiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM)
Taifa Bw. Abdallah Bulembo ilitangazwa
kuwa kuna vigogo wa CHADEMA waliojiunga na CCM ambao ni Mwenyekiti wa Baraza la
Wazee CHADEMA Bw.Ambindwile Mwantondo na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana BAVICHA
Bw. Frank Fumbo.
Bw.
Mwambigija alisema kuwa katika chama chao hakuna viongozi wenye majina hayo na
kwamba walichokifanya CCM ni kutumia jina la CHADEMA kujipa umaarufu ambao
umepotea katika jimbo la Mbeya na kuongeza kuwa iwapo CCM itaendeleza
propaganda hizo chafu, watavuruga mikutano yao.
''Sisi
hatutumii jina la CCM kunadi chama chetu, wao wanawalaghai wananchi kwa
kutumia jina la Chama chetu,uvumilivu umefika mwisho, wakiendelea
tunatumia vijana wetu kuvuruga mikutano yao,''alisema, Bw. Mwambigija.
Alimtambulisha
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA kuwa ni Bw. Edward Mwakagenda na
Mwenyekiti wa BAVICHA kuwa ni Lule Mwashamba na kukukanusha idadi ya wanachama
360 wanaotajwa kujiunga na CCM katika mkutano huo.
‘’Hakuna
mwanachama yoyote aliyejiunga na CCM tangu tumalize uchaguzi wa Udiwani Kata ya
Iyela ambao tulishinda kwa kishindo, wanachokifanya CCM ni propaganda ambazo
zimepitwa na wakati,wakiendelea hatutavumilia, tutavamia mikutano yao na
kuvuruga’’alisisitiza Bw. Mwambigija.
Alisema
CHADEMA haijapoteza mwanachama yoyote na kwamba sasa kimejipanga kufanya
mikutano ya hadhara kaunzia Agosti 18 ambapo Mbunge wa Arusha, Godbless
Lema,ambaye ataambatana na wabunge wenzie Tundu Lissu na Halima Mdee watafanya
mikutano katika Jiji la Mbeya,Mlowo, Tunduma, Tukuyu, Kyela, Chunya na Ileje
katika operesheni maalumu ya ‘M4C’ ‘CHADEMA ni msingi.’
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Bw.Mwakagenda alisema kuwa yeye
ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee na kuwa katika baraza lake hakuna mtu
anayeitwa Mwantondo.
Post a Comment