Shamba la pareto lililotelekezwa bila kuchumwa |
Wakulima wa kijiji cha Nsheha wakilima kuondoa maua ya pareto yaliyotelekezwa ili kupanda maharage |
Mwenyekiti wa kijiji cha Pashungu Akson James akonesha shamba la Viazi ambalo hapo mwanzo lilikuwa ni shamba la Pareto |
KATIKA hali
isiyo ya kawaida baadhi ya wakulima wa zao la Pareto katika vijiji vilivyopo
kata ya Santiliya, Isuto na Itawa wilayani Mbeya wameamua kutelekeza mashamba
ya pareto kwa kung’oa maua yaliyopo kwa ajili ya kulima mazao mengine ya
kibiashara ya maharage na Viazi mviringo.
Mwandishi wa
habari hizi alishuhudia wakulima katika vijiji vya Nsheha,Jojo na Pashungu kata
za Santiliya na Itawa waking’oa pareto mashambani kwa madai kuwa zao hilo kwa
sasa limekosa soko.
Wakizungumza
katika maeneo mbalimbali ya mashamba kwenye vitongoji vya Pashungu,Idunda na
Sakukwa katika kata ya Itawa na vitongoji vya Jojo a Shigamba katika vijiji cha
Jojo na Shigamba kata ya Santiliya baadhi ya wakulima hao walisema kuwa kwa
sasa zao hilo limeingiliwa na matapeli wanaochukua pareto yao bila kuwalipa.
‘’Tunalima
kwa gharama zetu, maua yakiwa tayari wanakuja matapeli wanaokopa maua bila
kulipa, hatujalipwa maua yetu kwa zaidi ya miezi nane,’’alisema Ezekiel Satiel mkulima mkazi wa kijiji cha
Pashungu.
Alisema kuwa
serikali ndiyo iliyosababisha wakulima waamue kung’oa pareto na kulima mazao
mengine biashara, tulijitokeza kulima kwa wingi zao la pareto, msimu uliopita
sasa hivi kila nyumba ya mwanakijiji wamekumbwa na njaa,pareto imechukuliwa kwa
mkopo bila kulipwa,’’alisema Satiel.
Naye Bahati
Sifuku mkulima wa Pashungu alisema kuwa alikopesha pareto yake kwa kampuni moja
kubwa (jina linahifadhiwa kwa sasa) lakini hadi sasa imepita miezi minne
hajalipwa fedha yake na kuwa kutokana na hali hiyo shamba lake la pareto
ameamua kulima maharage badala ya pareto.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa kijiji cha Pashungu Akson James alisema kuwa eneo kubwa
lililokuwa linalimwa pareto kwa sasa yamelimwa mazao mengine ya Viazi na maharage
na baadhi ya mashamba ya pareto yametelekezwa na kuota majani bila kupaliliwa.
Alitaja moja
ya shamba la hekari mbili ambalo limetelekezwa kuwa ni shamba la Umoja wa
kanisa la Jeshi la Wokovu la kijiji hicho, ambapo kiongozi wa kanisa hilo Mchungaji
Johson Nyamuhanga alisema kuwa wameamua kulitelekeza shamba hilo bila kuvuna
kutokana na kukosekana kwa soko.
‘’Shamba
letu ni hekari mbili tumeamua kuacha pareto iharibike kwa kuwa hakuna pa
kuiuza, waumini wapo kwenye mashamba yao wanang’oa pareto na kulima viazi,hata
tungechuma hakuna pa kupeleka tumeamua kuliacha kama lilivyo,’’alisema Mchungaji
Nyamuhanga.
Mchungaji
Nyamuhanga alisema kuwa makadirio ya ukubwa wa shamba hilo wangeweza kuvuna
gunia sita ambazo ni sawa na kgm 300 ambazo wangeuza kiasi cha sh.600,000 kwa
bei y ash.2000 kwa kilo moja ya pareto.
Naye Ofisa Mtendaji
wa kijiji cha Jojo kilichopo kata ya Santilya Anderson Yamaliha alisema kuwa
zaidi ya vijana ambao ni nguvu kazi ya kijiji wapatao 600 wamejikuta wakiachana
na kilimo cha pareto na kulima mazao mengine ya biashara kama vile viazi na
maharage ili waweze kujiongezea uchumi.
Alisema kuwa
moja ya sababu zilizowafanya waachane na kilimo cha pareto limetokana na
kushuka kwa ghafla kwa bei kutoka sh.2400 hadi sh.1800 kutokana na kuwepo kwa
ukiritimba wa ununuzi wa zao hilo.
Alisema kuwa
msimu uliopita wakulima waliongeza kilimo cha zao hilo baada ya bei kupanda
hadi kufikia 2500 lakini baada ya kukosekana ushindani wa ununuzi kwa makampuni
mengi limebaki kampuni moja ambalo linawakopa wakulima kwa sh. 2000 na malipo huja baada ya miezi
kadhaa.
Post a Comment