Ads (728x90)

 -STORI NA RASHID MKWINDA-
MKAZI wa kitongoji cha Iponjola kijiji cha Isange wilayani Rungwe mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la  Riziki Mwangoka(27)anadaiwa kufanya kitendo cha kinyama kwa kumuua mwanaye mdogo mwenye umri wa miaka mitatu kwa kuchimba shimo sebuleni kwake na kumfukia akiwa hai.
 Tukio hilo la kinyama linadaiwa kufanyika Novemba mwaka jana ambapo mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo kwa nguvu kutoka kwa mama yake ambaye awali alikuwa ni mkewe aliyefahamika kwa jina la Esther Mwambenja(23)na kulazimisha kwenda kuishi na mtoto huyo nyumbani kwake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amesema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa katika mgogoro wa kindoa na mkewe alilazimisha kumchukua mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Debora Riziki(3) kutoka kwa mama yake mzazi.
Amesema kuwa mtuhumiwa alimfuata mtoto huyo kwa mama yake umbali wa zaidi ya kilomita 30 katika kijiji cha Kiwira na kuibuka mzozo wa nani aishi na mtoto huyo ndipo mtuhumiwa alipomchukua mtoto huyo kwa nguvu na kuondoka naye.

Amesema kuwa alipofika nyumbani kwake mtoto alikuwa amechoka na kulala usingizi ndipo baba alipochimba shimo sebuleni na kumzika mwanaye akiwa hai.
Amesema kuwa kwa kipindi cha zaidi ya miezi minne mtuhumiwa alikuwa akiishi na maiti ndani ya nyumba yake ambapo mama wa mtoto alikuwa akihitaji kumchukua mtoto huyo lakini alikuwa akimpiga chenga ndipo alipotoa taarifa kituo cha polisi kuhitaji kumpata mwanaye.
Kamanda Athumani amesema kuwa polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuuliza alipo mtoto huyo ambapo kwa muda mrefu hakutoa ushirikiano wowote hadi jana aliposema kuwa alimuua mwanaye na kumzika katika shimo alilochimba sebuleni kwake.
Amesema kuwa polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kufukua shimo hilo na  kuukuta mwili wa mtoto huyo na kusema kuwa katika uchunguzi hawakuona dalili zozote za kuuawa kwa mtoto huyo na kuthibitisha kuwa mtoto huyo alifukiwa shimoni akiwa usingizini na baadaye kufariki dunia.

Post a Comment