Ads (728x90)

Ayasi Ramadhan Diwani wa Kata ya Songwe  akizungumza wakazi wa kijij Songwe kati kuhusu mgogoro wa fidia ya mashamba



Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Diwani kuzungumzia mgogoro wa fidia ya mashamba ya Kaloleni





Mwenyekiti wa kamati ya fedha Paulo Mwasuka akisoma mapato na matumizi ya kijiji hicho kwa miezi mitatu

Mwananchi wa kijiji cha Songwe Asajile Kandonga akichangia hoja kwenye mkutano wa hadhara wa kijiji hicho kuhusu mgogoro wa ardhi wa mashamba ya Kaloleni

WANANCHI wa kijiji cha Songwe Kati kilichopo katika kata ya Songwe wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya wamewataka watendaji wa Halmashauri ya kijiji hicho waachie ngazi kutokana na kuruhusu upotevu wa fedha zaidi ya sh. milioni 50 zinazotokana na fidia ya mashamba ya kijiji hekari 15.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Diwani wa Kata hiyo Ayasi Ramadhani walidai watendaji hao ikiwemo kamati ya ufuatiliaji wa fidia walishindwa kufanya tathmini ya hekari za mashamba ya kijiji ambazo ni hekari 15.4 na badala yake wamefanya tathmini hekari 5.6.
‘’Hekari hizo 5.6 tumepata kiasi cha sh mil 27, lakini tulikuwa na jumla ya hekari 21, hekari zingine 15.4 hazijulikani zimepotelea wapi na watendaji wa kijiji walitathmini namna gani,’’ alisema Asajile Kandonga mkazi wa kijiji hicho.
Naye Cletus Nyilela alisema kuwa wakazi wa kijiji hicho walikuwa na hekari za mashamba ambazo zilikuwa zinakodishwa kwa wananchi na fedha zake zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya kijiji lakini watendaji hao wa kijiji wameachia kiasi cha hekari 15.4 na hivyo kukikosesha kijiji zaidi ya milioni 50.
Alisema kuwa kamati hiyo imetumia fursa hiyo kuhujumu mashamba ya kijiji kwa manufaa yao hivyo kutokana na hali hiyo wanapaswa kuachia ngazi na kuchukuliwa hatua za kisheria, ‘’ Hawa ni wabadhirifu na wahujumu wa uchumi wachukuliwe hatua za kuhujumu mali ya kijiji,’’ alisema Kipenda John mkazi wa kijiji hicho.
Awali akisoma taarifa za mapato na matumizi ya kijiji hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha Paulo Mwasuka alisema kuwa jumla y ash mil 28.9 zilitokana na mapato mbalimbali ya kijiji ambapo kati ya hizo kiasi cha sh mil 27.7 kilitokana na fidia ya mashamba hekari 5.6.
Baada ya taarifa hiyo wananchi walikuja juu ya kudai kuwa kiasi hicho cha hekari za mashamba si halisi kwa kuwa eneo lao la mashamba ni kubwa ukilinganisha na ukubwa huo wa hekari 5.6.
Diwani wa kata hiyo Ayasi Ramadhan alidai kuwa alienda kupima eneo hilo akiongozana na baadhi ya wazee wa kijiji hicho kwa hatua za miguu na kukuta jumla ya hekari 28 na baadaye walipima kwa futi kisha wakapima kwa kipimo cha GPS na kukuta jumla ya hekari 33.83.

Ramadhani alisema kuwa kutokana na hali hiyo alibaini kuwa kuna udanganyifu uliofanyika hivyo alilazimika kuunda kamati ya watu 7 watakaofuatilia tatizo hilo huku Halmashauri ya kijiji na wafuatiliaji wa fidia wa awali wakilazimika kukaa pembeni kupisha uchunguzi wa kamati hiyo ambayo itafanya kazi kwa siku 14.

Post a Comment