Ads (728x90)

Mkuu wa wilaya ya Mvomero Betty Mkwassa akivika mgolole wa heshima Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Nice Catering Yona Sonero  kwenye sherehe za kila mwaka anazowafanyia wafanyakazi wa kampuni hiyo zilizofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Nashera mjini Morogoro


Mkurugenzi wa kampuni ya Nice Catering Yona Sonero akimjulia hali mmoja wa watu wenye ulemavu Jabir Mwaipaya kwenye kituo cha kulelea yatima, wazee na watu wenye ulemavu cha Mehayo mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.


Mkurugenzi wa kampuni ya Nice Catering Yona Sonero na Meneja wa Kampuni ya Mabasi ya Rungwe Express Bonny Mbamba wakiwa kwenye maombi maalumu kabla ya kukabidhi msaada wa vyakula, mafuta na sabuni kwenye kituo cha Mehayo cha mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.
Watoto  yatima na wenye ulemavu wa akili na viungo wa kituo cha Mehayo Mkoani Morogoro,mwishoni mwa wiki wamekabidhiwa  msaada wa vyakula mbali mbali na fedha tasilimu Sh750,000 kutoka kwa  Kampuni ya Nice Catering.
 Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo,Mkurugenzi wa Kampuni ya  Nice Catering,Yona Sonero alisema  sadaka kubwa inayomgusa mungu ni ya kusaidia watoto yatima kwa kuwawezesha kuishi maisha kama walivyo watoto wengine.
“Kuna wafanyabiashara wengi ambao wamejaliwa kuwa na kipato kikubwa ni vema wakatumia sehemu ya fedha zao kuwasaidia watoto hawa ili na wao waweze kuishi kama binadamu wengine.
Aidha Sonero alisema pamoja na msaada huo wa chakula anajitolea kununua baiskeli mbili za miguu mitatu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa miguu.
Alisema kampuni hiyo imekuwa ikifanya hivyo kila mwaka ambao ilitanguliwa na semina elekezi kwa watumishi wake zaidi 1000 na kwamba sadaka kuu ambayo anaitoa kwa mungu ni kuwasaidia watoto hao ,ambao wanamahitaji mengi na maisha yao ni magumu kutokana na uwezo mdogo walionao watu waliojitolea kuwalea.
Kwa upande wake mlezi wa kituo cha Mehayo kilichopo mjini Morogoro Linda Ngido alisema  kituo  hicho kina jumla ya watoto 65 wenye umri wa kuanzia miaka saba hadi 42 ambao ni yatima na ulemavu wa akili na viungo ,lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya huduma ya afya kutokana na kituo hicho kushindwa kumudu gharama za matibabu mara wanapokwenda hospitalini.
“Tunaomba serikali ikitambue hiki kituo kuwa ni kazi ya kujitolea hivyo hawa watoto wapewe msamaha wa matibabu ili waweze kupata matibabu kama ilivyo kwa watu wenye uwezo na kuondokana na usumbufu ambao tunaupata katika vituo vya afya”alisema Ngido.
Alisema anashukuru kupata msaada huo kwani utawasaidia watoto hao kupata chakula cha uhakika kwani kwa mlo mmoja anatumia sh100,000 kutokana na idadi kubwa ya watoto alionao katika kituo hicho.
Aidha alisema changamoto nyingine ni  ukosefu wa maji kutokana kushindwa kulipia gharama za maji safi na taka za Moruwasa na kusababisha kutumia maji ya visima ambayo ladha yake ni ya chumvi.Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye sherehe hiyo Mkuu wa wilaya ya Mvomero Betty Mkwassa aliwataka wamiliki wa makampuni mbalimbali nchini kuwa na nidhamu ya kulipa kodi serikalini.
Mkwassa alisema iwapo makampuni yatajitokeza kulipa kodi bila kusukumwa na mamlaka ya mapato nchini uwezekano wa makadirio ya ukusanyaji mapato serikalini utaongezeka mara dufu.
Alisema Kampuni ya Nice Catering ni mfano wa kuigwa kutokana na kufanya shughuli zake kwa uwazi.
''Kufanya vizuri kwa kampuni hii kunatokana na uwazi wake wa shughuli mbalimbali, hii ni dalili kwamba ni walipaji kodi wazuri,''alisema Mkwassa.


Nice Catering ni kampuni tanzu inayomiliki kampuni ya mabasi ya Rungwe Express na Rungwe Hotel ya Jijini Dar es salaam
(HABARI NA PICHA KWA MSAADA WA BLOGU YA BRANDY NELSON) 

Post a Comment