Ads (728x90)


BAADHI ya askari Polisi waliokuwepo ndani ya chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Iringa wakati askari mwenzao Pacificius Cleophace Simoni akitiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia ya mwanahabari Daudi Mwangosi, walivuruga utulivu wa mahakama hiyo baada ya simu zao kupigwa wakati Jaji Paulo Kiwehlo akiendelea kusoma maelezo ya kesi hiyo.
Hatua hiyo iliyowashangaza wanahabari na raia wengine waliojitokeza kusikiliza hukumu hiyo, ilitokea muda mfupi baada ya mmoja askari Polisi aliyekuwepo ndani ya mahakama hiyo kutoa tangazo liliwatisha watu wengine kabla shughuli ya mahakama hiyo haijaanza.
Huku akionekana ana hasira, kwa sauti ya ukali askari huyo alimtaka kila mtu aliyepo ndani ya mahakama hiyo azime simu yake na shughuli ya mahakama itakapokwisha anyanyuke kimyakimya na kutoka nje kwa utulivu kama hataki kukutana na nguvu ya jeshi hilo ambalo waliokuwepo mahakamani hapo jana walishuhudia jinsi lilivyokuwa limejipanga kukabiriana na raia wasio na hatia waliokwenda kushuhudia kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo.
Barabara mbili za kuingilia mahakamani hapo, ile inayotokea hospitali ya mkoa wa Iringa na ile inayotokea kwa mkuu wa wilaya Iringa zilikuwa zimesheheni askari waliokuwa na silaha kali, mobomu na magari kadhaa yenye bendera nyekundu likiwemo gari lao kubwa maarufu kama gari la washawasha.
Wakati wanahabari na raia wengine waliokuwepo mahakamani hapo wakitii amri ya askari huyo, askari wenzao hawakutii amri hiyo na simu zao zilipoita hawakuchukuliwa hatua yoyote ile.
Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo alisema; “Nadhani amri ile ilikuwa ikiwalenga wanahabari na wananchi wengine waliofika mahakamani hapa. Na kama ingetokea simu ya mwanahabari ingeita hata kwa bahati mbaya nadhani pasingetosha.”
Makamu Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile alisema ni kama amri ile ilikuwa ikiwalenga wanahabari ambao wamekuwa wakipata misukosuko mingi katika kipindi chote kesi hiyo itakayotolewa hukumu yake kesho Julai 27, ilipokuwa ikifikishwa mahakamani.
Balile alisema watahakikisha wanakutana na Inspekta Jenerali wa Polisi na Jaji Kiongozi ili kuwasilisha malalamiko ya namna shughuli za kimahakama zinavyoingiliwa na askari Polisi.
Taarifa iliyotolewa na wanaharakati wa haki za binadamu inaonesha katika maeneo mengine mawakili wamekuwa wakizuiwa na jeshi la Polisi kufanya kazi zao.(STORI NA PICHA KWA HISANI YA BONGOLEAKS BLOGU)

Post a Comment