Ads (728x90)Na, Bloga Wetu

MAHAKAMA ya hakimu mkazi wa wilaya ya Mbeya imemhukumu kifungo cha miaka 30, mshitakiwa kosa la unyang;anyi wa kutumia silaha,Ali Salum (32) baada ya kukiri kutenda kosa hilo mahakamani hapo.

Mshitakiwa ambaye alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza pamoja na wenzie watatu Juni 17 alikiri baada ya kusomewa mashtaka ya uvamizi wa kutumia silaha na kupora bunduki aina ya SAR yenye namba za usajili TZ PS 39847164020 mali ya serikali inayomilikiwa na Jeshi la Magereza.

Akitoa maelezo ya hukumu ya kesi hiyo Hakimu mkazi wa wilaya Bi.Aneth Nyenyema alisema kuwa anatoa uamuzi huo baada ya mshtaakiwa kukiri mwenyewe kutenda kos hilo na kwamba adhabu inayotolewa kwa mshtakiwa hailengi kumkomesha bali inalenga kumfundisha.

‘’Adhabu zinazotolewa na Mahakama hazina nia ya kukomesha bali zina nia ya kufundisha, kutokana na hilo mahakama inakutia hatiani kufuatia kukiri kwako makosa, utatumikia kifungo cha miaka 30 jela,’’alisema Hakimu Nyenyema.

Akisoma mashataka hayo kabla ya hukumu mbele ya hakimu mkazi wa wilaya ya Mbeya Bi.Nyenyema, Wakili wa serikali Bi. Mwajabu Tengeneza alisema kuwa mnamo Mei 5 mwaka huu katika eneo la Songwe gerezani mshtakiwa pamoja na wenzake watatu walikula njama na kumvizia askari magereza WDR Ambrose Ngonyani ambaye alijeruhiwa na kuporwa bunduki.

Alisema kuwa mshtakiwa pamoja na wenzie walimvizia askari huyo wakati anarejea nyumbani nyakati za jioni kwa ajili ya kujipatia chakula cha jioni ndipo, washtakiwa wakiwa na panga walimvamia na kumjeruhi mkononi kisha wakampora bunduki.

Wakili Tengeneza alisema kuwa washtakiwa walikiuka sheria kifungu namba 287 A ya sheria kanuni ya adhabu sura namba 16 iliyorejewa mwaka 2002 na kuongeza kuwa mahakama inapaswa kutoa adhabu kali iwe fundisho kwa vijana wanaotumia silaha kuhatarisha usalama wa nchi.

Awali akitoa maelezo ya mshtakiwa aliyoyathibitisha polisi, askari mpelelezi wa kesi hiyo Koplo Vicent Henjewele alisema kuwa mshitakiwa alitoa maelezo polisi kwa kina ikiwa juu ya ushiriki wake wa uvamizi na uporaji huo wa silaha na kuongeza kuwa historia ya mshitakiwa inaonesha kuwa ameshiriki matukio mengi ya uporaji.

Koplo Henjewele alisema kuwa mtuhumiwa alikiri mbele ya polisi kuwa yeye alifukuzwa kijijini kwao Lupa Tingatinga wilayani Chunya ambapo wananchi walimchomea nyumba yake kutokana na vitendo vyake vya wizi na uporaji ambapo baadaye alihamia katika mji mdogo wa Mbalizi alikokutana na mmoja wa washtakiwa wa kesi hiyo.

Alisema kuwa alipokutana na mshtakiwa mwenzie aliyemtaja kwa jina la Emanuel Martin aliyeweahi kukutana naye gerezani ndipo walipopanga njia za kupata bunduki kwa ajili ya kutekeleza kazi zao za ujambazi wakiwa uraiani.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wakikana mashataka yao ni pamoja na Martin, Bryson Sanga na John Waziri ambapo hata hivyo mshitakiwa Martin aliichekesha mahakama hiyo kwa kusema kuwa haoni sababu ya kuisumbua mahakama naye anakiri kosa hilo ili afungwe.

Hata hivyo Hakimu Nyenyema alisema kuwa utaratibu wa maelezo hayo utaletwa tena mahakamani hapo Julai Mosi ambapo kesi hiyo imepangwa tena kusikilizwa.

Post a Comment