Ads (728x90)

Bosi Mmalawi Evance Mwale akiongozwa na askari polisi kuingia katika chumba cha mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Mbeya alikoshitakiwa kwa kosa la Rushwa ya Ngono na Ushawishi wa ngono, amerudishwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana.

Askari Polisi wakimrejesha rumande Bosi Mmalawi Evance Mwale anayeshitakiwa kwa makosa ya Rushwa ya Ngono




Na, Bloga Wetu, Mbeya
MENEJA wa Bandari Kavu ya Malawi ‘Malawi Cargo’iliyopo eneo la Iyunga jijini Mbeya Evance Mwale (49)amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Mbeya akituhumiwa kwa makosa ya kulazimisha ngono kwa mke wa mfanyakazi wake na kutumia vibaya madaraka ya kazi yake.
Mshitakiwa ambaye ni raia wa nchi jirani ya Malawi alidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Novemba na April mwaka huu katika eneo la Iyunga jijini Mbeya ambapo alimlazimisha mke wa mfanyakazi wake kufanya naye ngono bila ridhaa yake.
Akisoma mashtaka ya mshitakiwa huyo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Bw. Gilbert Ndeuruo,Wakili wa serikali Bw. Basilius Namkambe alisema kuwa mshitakiwa anakabiliwa  mbili za rushwa ya  ngono  na kutumia vibaya madaraka yake.
Bw. Namkambe alisema kuwa mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo April 11 mwaka huu katika Hotel ya Moja One iliyopo Iyunga jijini Mbeya ambapo alijaribu kumlazimisha mke wa mfanyakazi wake Bw.Charles Nyondo, Bi.Roda Kanjeli kufanya naye ngono bila ridhaa yake.
Alisema kuwa mshitakiwa alifanya makosa hayo kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano kifungu namba 25 cha sheria za kuzuia na kupambana na rushwa ACT namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema kuwa shitaka la pili linalomkabili mshitakiwa huyo ni kutumia wadhifa wake wa kazi kumshawishi Bi. Roda Kanjeli kufanya naye ngono bila ridhaa yake kinyume cha sheria za kuzuia na kupambana na rushwa namba 31 ACT namba 11 ya mwaka 2007.
Mshitakiwa ambaye amekana mashitaka yake alirejeshwa rumande hadi  Julai mosi mwaka huu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya sh. milioni 10 kila mmoja na kukabidhi hati ya kusafiria mahakamani.

Post a Comment