Ads (728x90)
SERIKALI imesema kuwa imeshindwa kuongeza kima cha chini cha Mshahara kutokana na mapato ya ndani kutokidhi mahitaji ya mishahara yote ya wafanyakazi nchini ambayo ni asilimia 44 ya bajeti nzima ya nchi ambayo ni zaidi ya sh. Trilioni 10.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa bajeti nzima ya mishahara ya wafanyakazi nchini ni sh. Trilioni 4.7.
Alisema kuwa bajeti ya serikali ni finyu ambayo haikidhi ongezeko la mishahara ya wafanyakazi wote nchini  na kwamba kiasi hicho ni sehemu ya bajeti nzima ya serikali kwa mwaka wa fedha.
‘’Hatuwezi kutumia mapato yote ya serikali kwa mishahara, sio kwamba tunashindwa kuongeza mishahara kwa ‘’mtima nyongo’’ (roho mbaya) bali uwezo wetu ni mdogo,’’alisema Rais.
Alifafanua kuwa mwelekeo wa uchumi wan chi yetu ndio unaotoa tafsiri na kwamba hata hivyo serikali iko tayari kukaa chini na wafanyakazi kwa nia ya kuzungumza nao kuangalia kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kuweka punguzo la kodi.
Kadhalika alisema kuwa imeamua kuubeba mzigo kw amalipo ya pensheni ya wafanyakazi nyuma ya mwaka 1999 ambao wakati sheria hii inaanza serikali ilikuwa bado haijaanza kuwajibika juu malipo ya pensheni za wastaafu wa serikali.
‘’Kabla ya mwaka 1999 pensheni za wafanyakazi zilikuwa bado hazijaanza kukusanywa,lakini serikali italazimika kuchangia waliotakiwa kuchangiwa kabla ya mwaka huo, tutachangia kwa miaka kumi, mwaka huu tutachangia sh. Bilioni 50,’’alisema na kuongeza.
‘’Hakuna mfanyakazi yoyote wa serikali aliyestaafu atakayeshindwa kulipwa mafao yake,’’alifafanua.
Pia Rais Kikwete aliwaonya waajiri kutowalazimisha wafanyakazi kujiunga kwenye mifuko ya kijamii kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kuwalazimisha kuingia katika mifuko ambayo haina tija kwa maslahi yao.
‘’Waajiri acheni tabia za kuwalazimisha wafanyakazi wajiunge kwenye mifuko Fulani yenye maslahi zenu,hiyo sio tabia nzuri, waacheni wafanyakazi waamue wenyewe,’’
Katika kuhakikisha serikali inafuatilia kwa karibu masuala ya wafanyakazi Rais Kikwete alisema kuwa serikali imeweka utaratibu wa kukutana na viongozi wa wafanyakazi kwa mwaka mara tatu ambapo katika mazungumzo hujadili mustakabali wa wafanyakazi na maslahi yao.
‘’Wanaozungumza hawagombani, tutaendelea kuzungumza na kukutana mara tatu kwa mwaka ili kujadili matatizo yanayoikumba sekta ya wafanyakazi nchini,’’alisema .
Alisema kuwa serikali itaunda chombo chini ya Ofisi ya Rais kuangalia sekta sita kwa wakati tofauti kama vile kilimo, biashara, viwanda na mambo mengine yanayoigusa jamii.
Pia alisema kuwa serikali imedhamiria kuongeza ajira kupitia fursa za uwekezaji ambapo katika programu hii ajira 195,000 ambapo kati ya hizo 142,000 inatokana na miradi ya maendeleo na 56,000 kupitia sekta ya umma na kwamba bado kuna fursa ya kuongeza ajira 600,000.
Alisema kuwa viongozi wa ngazi za serikali katika maeneo ya mikoa na wilaya wanatakiwa kuwa wepesi kutenga maeneo ya kuwasaidia vijana ambapo pia kila atakayekopeshwa anatakiwa kusimamiwa vizuri.
Aidha Rais Kikwete fursa hiyo ya maadhimisho ya Mei Mosi kusisitiza suala la amani na utulivu wa nchi na kuwaonya wanaotumia masuala ya udini na ukabila kuacha mara moja kwani wanaweza kuliingiza Taifa katika maangamizi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
‘’Ndugu zangu chuki hizi za udini zimetoka wapi, haya mambo yalipoanza wala hapajulikani, masuala ya mauaji  ya viongozi wa kidini, migogoro ya uchinjaji, hii imeanzia wapi, kabla ya hapa hatukuwahi kusikia hali hii,’’alisisitiza.
Alisema kuwa mifumo iliyopo kuhusu suala la uchinjaji imeanza tangu enzi za kale na kwamba ijapokuwa haijawahi kutungiwa sheria lakini haijawahi kutokea kuwagawa Watanzania.
Alisema hali inapobadilika inaonekana na kwamba jambo la muhimu ni kushikilia yanayojenga badala yanayosababisha chuki na fitina miongoni mwa Watanzania.
‘’Amani inapovunjika si rahisi kurejea tena hatupaswi kuichezea, tusiwasikilize wanaotaka  kutupeleka pabaya, vita vya dini havina mshindi, kila mtu anaamini akifia dini yake atakaa kulia kwa Bwana,’’alisema.
Aliwataja viongozi wa dini kuketi pamoja na kuangalia namna ya kuondoa matatizo hayo ambayo yanaweza kuliingiza Taifa katika majanga, ‘’ tumekaa na viongozi wa kiislamu na kikristo tumeulizana tumepata jibu, mwelekeo uliokuwepo ulikuwa ni mbaya ambao hauna maslahi kwa Wakristo wala kwa waislamu,’’alisema.

Post a Comment