Ads (728x90)


Mtoto Anna Mwakyoma anayedaiwa kutelekezwa na baba yake kilabu cha pombe za Kienyeji.


-Adaiwa kuelekea kwenye machimbo ya dhahabu


MSICHANA Anna Mwakyoma(13) mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Majengo iliyopo wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ametelekezwa katika kilabu cha Pombe za kienyeji  na baba yake mzazi aliyemtaja kwa jina la Fred Mwakyoma.

Tukio hilo la unyanyasaji limetokea huku kukiwa na mkakati wa kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na taasisi mbalimbali kikiwemo Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA limetokea mwishoni mwa wiki baada ya mwandishi wa habari hizi aliyekuwa akifuatilia vitendo vya ukatili wa kijinsia kufika wilayani humo.

Akisimulia mkasa huo katika ofisi ya Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani hapa Binti huyo ambaye alikuwa ameambatana na Ofisa wa polisi kutoka Kitengo cha Dawati la jinsia Majuto Khalfani, alisema kuwa alifika wilayani humo na baba yake wakitokea Sumbawanga kupitia mkoani Mbeya.

Alisema baba yake ambaye ametengana na mama yake mzazi aliyemtaja kwa jina la Asha Mwanandeje mkazi wa Majengo mjini Sumbawanga alimfuata na kuondoka naye kwa madai kuwa alitaka kumkutanisha na kaka yake ambaye wameachana miaka mingi.

‘’Baba alinifuata Sumbawanga, akasema nije naye Mbeya nionane na kaka John, sikuonana na kaka tukapanda gari kuja huku Chunya, tangu aliponiacha hapa kilabuni sijamuona tena,’’alisimulia kwa masikitiko msichana huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa chini ya uangalizi wa Dawati la Jinsia la Polisi wilayani Chunya.

Aliendelea kusimulia kuwa awali alikutana na baba yake akiwa darasa la kwanza walipokuwa wakiishi mjini Tunduma lakini baadaye ulitokea ugomvi ambao ulisababisha baba na mama yake watengane na yeye kwenda kuishi na mama yake mjini Sumbawanga.

Alisema kuwa kwa kipindi chote ambacho alikuwa akiishi na mama yake mjini Sumbawanga hajawahi kukutana na baba yake hadi alipofika hivi karibuni na kumtaka waondoke pamoja kuelekea Mbeya.

‘’Alipokuja mama alikuwa yupo kwenye biashara zake za kuuza mpunga alinichukua alfajiri tukapanda Basi hadi Mbeya, hata mama sikumuaga,’’alisema msichana huyo.

Akizungumza mazingira ya kupatikana kwa mtoto huyo Ofisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Chunya Bi. Macrina Mayage alisema kuwa kwa mujibu wa maelezo ya msichana huyo baba yake alimtorosha kutoka kwa mama yake ambapo walipofika Mbeya waliondoka naye hadi Chunya na kumtelekeza bila msaada wowote na yeye kutokomea kusikojulikana.

Alisema hadi sasa msichana huyo amehifadhiwa katika kituo cha Polisi wilayani Chunya kitengo cha Dawati la Jinsia wakijaribu kutafuta mawasiliano katika shule aliyokuwa akisoma mjini Sumbawanga.

Naye Ofisa wa polisi kutoka Dawati la Jinsia wilayani humo Bi. Majuto Khalfani alisema kuwa msichana huyo alikabidhiwa kwao kutoka kwa mama mmoja ambaye aliletwa na vijana katika eneo lake la biashara za pombe za kienyeji usiku wa manane.

Kwa mujibu wa Bi. Khalfani ni kwamba, msichana huyo aliachwa stendi na baba yake kuanzia mchana hadi saa sita za usiku ndipo alipoingia katika eneo la pombe za kienyeji ambako alikutana na mama huyo ambaye alimhifadhi nyumbani kwake hadi asubuhi alipompeleka kituo cha Polisi.

''Hatujui alipo baba yake hadi sasa,hatujapata taarifa za ajali au kifo, tumeenda hospitali ya wilaya hatujaona majeruhi au mtu yoyote aliyeripotiwa kufariki dunia, inawezekana ameelekea kwenye machimbo ya dhahabu na kumtelekeza mwanaye, kitendo alichokifanya hakifai katika jamii,''alisema Bi. Khalfani.

Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kimekuwa mstari wa mbele kupinga ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake na watoto na kulazimika kuwatuma baadhi ya waandishi wa habari kufuatilia na hatimaye kuibua matukio ya aina hii maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TAMWA Bi. Valerie Msoka ni kwamba matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika maeneo ya pembezoni hayaripotiwi katika vyombo vya habari hivyo kutoa fursa kuendelea kwa matukio hayo bila kuchukuliwa hatua za kisheria.Post a Comment