Ads (728x90)

Baadhi ya waendesha Bodaboda wakiwa wamevaa Helmet zilizoziba masikio ambazo zimelalamikiwa kuwa zimekuwa chanzo cha ajali kutokana na waendesha bodaboda hao kutosikia honi za magari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya Kiserikali inayoshughulikia Kumaliza Umaskini,Majanga na Mazingira (APEC) Bw. Reespius Timanywa akiwahutubia maelfu ya waendesha Bodaboda waliohudhuria siku ya Bodaboda nchini.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dkt. Michael Kadeghe (katikati) akimeueleza  jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya APEC iliyotoa mafunzo kwa waendesha Bodaboda nchini Bw. Respius Timanywa (kulia) huku Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe akifuatilia kwa makini mazungumzo hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Bodaboda yaliyofanyika Kitaifa wilayani Mbozi mkoani Mbeya.
Waziri wa Uchukuzi Dkt Harrison Mwakyembe akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi    isiyo ya kiserikali ya APEC iliyoandaa mafunzo kwa waendesha Bodaboda wa mikoa 6 nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya APEC Respius Timanywa akimuongoza Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe katika maadhimisho ya siku ya Bodaboda yaliyofanyika Kitaifa wilayani Mbozi mkoani Mbeya.
Waendesha bodaboda wakiserebuka katika maadhimisho ya siku ya boda boda nchini

Baadhi ya viongozi wa chama na serikali wilayani Mbozi wakiwa katika maadhimisho ya siku ya Boda boda nchini yaliyofanyika mjini Vwawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya.

Baadhi ya waendesha Boda boda waliopata mafunzo wakiwa katika maadhimisho ya siku.

Na Ripota Wetu, Mbozi 
WAENDESHA boda boda nchini wamedai kuwa kofia ngumu zinazoingizwa nchini kwa ajili ya watumiaji hazina ubora kutokana na kuziba masikio na hivyo kuwafanya watumiaji kutosikia honi za magari wanapokuwa barabarani na hivyo kuchangia ajali.
Imeelezwa kuwa kofia hizo maarufu kwa jina la ‘Helmet’ zimekuwa chanzo cha ajali za barabarani badala ya kuzuia kutokana na kuzibwa masikioni na kwamba ili kupunguza ajali kofia hizo ziboreshwe ili ziwasaidie waendesha bodaboda.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Boda boda katika kilele cha mafunzo kwa waendesha bodaboda nchini yaliyofanyika Kitaifa katika wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kupunguza Umaskini na majanga na kuhifandhi Mazingira APEC Bw. Respicius Timanywa alisema kofia za waendesha  boda boda hazina Viwango.
Alisema mazingira ya uendeshaji wa Boda boda yanataka usikivu na umakini kwa kusikiliza honi za magari na kwamba iwapo zitaendelea kuingizwa kofia zinazoziba masikio kuna hatari ya ongezeko la ajali nyingi za Pikipiki nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Uchuzi Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo aliwatahadharisha waendesha Piki piki nchini kuzingatia sheria za usalama wa barabarani ili kuepusha vifo na majeruhi wanaotokana na uendeshaji usiozingatia sheria za usalama barabarani.
Dkt Mwakyembe alisema kuwa takwimu za vifo na ajali za waendesha boda boda zimekuwa zikiongezeka ambapo kwa mwaka 2012 kati ya ajali 127 watu 66 walipoteza maisha  kwa nchi nzima ambapo katika mkoa wa Mbeya kati ya ajali 77 waliopoteza maisha ni watu 37.
Aidha Dkt Mwakyembe alisema kuwa serikali itapitia kwa kina kero zinazosababisha ucheleweshaji wa leseni kwa waendesha bodaboda ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa kina matatizo yatokanayo na ushuru unaotozwa na Halmashauri za Wilaya ambazo zimekuwa kero kwa waendesha bodaboda.
‘’Mkiona kuna ushuru usiofaa nijulisheni, zipo kodi zingine za maonezi kwa wananchi tutazifuatilia ili kuondoa kero hizo,’’alisema Dkt. Mwakyembe.
Alisema ushuru wote unaosababisha kero kwa wananchi utaangaliwa upya kwa nia ya kuisaidia jamii itekeleze wajibu wake bila kikwazo chochote cha utendaji katika kukuza uchumi wan chi.
Kadhalika Dkt. Mwakyembe aliitaka mamlaka ya Mapato kutochelewesha leseni kwa waendesha Bodaboda ili kupunguza msururu unaosababisha waendesha boda boda kuchelewa kupata leseni.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw.Barakael Masaki alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la ajali kwa mkoa wa Mbeya kati ya Januari hadi Novemba 2013 ambapo jumla ya watu 66 walipoteza maisha na watu 96 walijeruhiwa.
Maadhimisho hayo ya mafunzo ya waendesha boda boda nchini yamehusisha jumla ya waendesha bodaboda 30,000 ambapo kati yao kuna wanawake 2600 kutoka mikoa 6 ya Dar es salaam,Tanga,Morogoro,Simiyu,Shinyanga,Ruvuma na Mbeya.

Post a Comment