Ads (728x90)



Jeraha linalodaiwa kutokana na kipigo kwa watu wanaodaiwa kuwa ni askari polisi wa kituo cha Tunduma



Adamu akisaidiwa kusimama mara baada ya kuachiwa kituo cha Polisi Tunduma
Mama wa Adamu Rosa Ambakisye akiangalia jeraha la mwanaye kichwani ambalo linadaiwa kutokana na kusulubiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni askari polisi wa kituo cha Polisi Tunduma
Jamaa wakimsaidia kumlisha chakula Adam mara baada ya kutoka kituo cha Polisi Tunduma ambako anadaiwa kujeruhiwa na kusulubiwa na askari polisi.
Adamu akiwa wodini Hospitali ya Tunduma ambako anapatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni askari polisi wa Tunduma.
Jeraha katika mguu wa Shomi Mtaki mara baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi shambani kwake hivi karibuni, mtoto wa Mtaki anadaiwa kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa ni askari polisi wa kituo cha Tunduma.
Shomi Mtaki Mwandishi wa Habari wa Uhuru Publication alipovamiwa hivi karibuni shambani kwake, anayeangalia ni mwandishi wa habari wa ITV/RADIO ONE Danny Tweve ambaye alimtembelea mara baada ya kupata taarifa za uvamizi huo.

NA RIPOTA WETU,TUNDUMA


KIJANA Adam Mtaki (20) amelazwa katika hosptali ya mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba mkoa wa Mbeya,baada ya kupata kipigo na kufanyiwa mateso makali na watu wanaodaiwa kuwa  askari Polisi wa kituo cha Tunduma.

Adamu ambaye ni  mtoto wa tatu wa mwandishi wa habari wa kampuni yaUhuru Publications LTD Shomi Mtaki anayeripoti kutokea mji wa Tunduma uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baba mzazi wa kijana huyo, Shomi Mtaki alisema kuwa tukio hilo limetokea Disemba 5 majira ya saa 5.00 usiku eneo la mtaa Wasikanyika wakati Adam alipo kutana na watu wawili wanaodaiwa kua ni askari polisi waliovalia nguo za kiraia ambapo mmoja alimfahamu kwa jina moja la Shuku.

Kulingana na taarifa za Bw. Mtaki ni kwamba mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo walifika katika kituo cha polisi wakiwa wameambatana na mkewe aliyemtambulisha kwa jina la Rosa Ambakisye majira ya saa 2:00 asubuhi lakini walishindwa kuonana na kijana wao hadi majira ya saa 8:00 mchana.

Taarifa zaidi zinadai kuwa vijana wawili ambao walikuwa ni miongoni mwa mahabusu waliolala kituo cha polisi siku hiyo walidai kuwa Adam alifikishwa kituoni hapo alisikika akilia kwa maumivu kutokana na kipigo alichokuwa anapewa na kuwa hawakujua ni nani anayepigwa hadi alipolazimishwa kuingia chumba cha mahabusu kwa kutambaa kimgongo kuelekea chumba cha maabusu huku akiwa amefungwa kamba shingoni.

Anasema kuwa vijana hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao walisema kuwa Adamu alisulubiwa kwa virungu na mateke na kueleza kuwa walisikia kauli ya askari wakisema kuwa kipigo hicho kitaendelezwa hadi ndugu na wazazi wake watakapofika kituoni hapo siku inayofuata.
.
Tulipopata taarifa tulifika kituoni hapo asubuhi, tuliomba kuonana naye ili tumpe chai lakini tulishindwa hadi alipofika Ofisa mmoja wa juu kutusaidia mkewe akapata fursa ya kumpa Chai mwanaye’’alisema Bw. Mtaki. 


Akizungumzia tukio hilo baada ya kutoka na kupewa PF 3,Adamu alisema ,usiku huo alikuwa nyumbani ,lakini baadaye alipigiwa simu na mwenzake akiomba msaada baada ya kukamatwa na walinzi wa kampuni binafs kwa tuhuma za kudhaniwa kuwa ni mhalifu.

 Alisema baada ya kumtambua mwenzake kuwa ni mwenyeji wa eneo hilo aliona mlinzi mwingine akiwa na watu wawili niliowafahamu kuwa ni maskari wa kituo hicho,ambao walitumia nguvu ya kumchukua kuelekea kituoni

‘’Niliwauliza nimekosa nini?Wakasema kuwa nikifika kituoni nitajua ninachoitiwa nilitii mamlaka lakini nilipofika kituo cha Polisi nilianza kupigwa mateke hadi kwenye meza ya mapokezi”alisema akiwa wodini.

Alisema haikutosha,maaskari walimpa adhabu ya kutambaa kwa kutumia mgongo akiwa amefungwa pingu mikononi,alifungwa kamba shingoni na kuburuzwa kupelekwa kwenye chumba ambako muda wote waliendelea kumpa kipigo kwa kutumia virungu vitano.

Alisema baadaye waliongezeka askari wengine ambao hakuwatambua wakashirikiana naye kumpiga na walipoona damu inaruka kutoka kichwani na kuchafua chumba hicho ndipo walipo ridhika wakampeleka chumba cha mahabusu kwa kuvutwa na kamba aliyofungiwa shingoni.

Kwa upande wake mama mzazi alisema kuwa kitendo cha polisi wa kituo hicho kumfanyia mtoto wake kitendo hicho kinafananishwa na unyama na kukiuka haki za binadamu kwa kuwa kama kijana huyo alikuwa na makosa ilistahili afikishwe katika vyombo vya sheria ili ajibu kosa kama 
analo.
“Sioni tatizo kama mototo wangu angechukuliwa hatua kama wengine wanaokosa,lakini kitendo cha kumpiga mtoto wakati ametii amri na kufikishwa kituoni toka waliko mchukua usiku ,kinatia shaka na ni eneo la nyumbani kwetu hakijaniridhisha kabisa.

Muuguzi wa zamu alipoulizwa hali ya kijana huyo,alisema kuwa hadi alipo pelekwa katika zahanati hiyo hali yake ilikuwa mbaya,kwa sababu alikuwa amepoteza damu nyingi na alikuwa ameshonwa nyuzi 6 kisogoni.

Aliyataja majeraha mengine aliyokutwa nayo ni pamoja na alama za uvimbe wa shingoni unaoonesha kuwa alifungwa na kamba ngumu,majeraha makubwa katika eneo la magoti,viwiko vya mkono na vidonda katikati ya miguu yake.

Kwa upande wake askari anayefahamika kwa jina la Shuku alipo takiwa kuelezea jambo hilo katika kituo hicho hakuwa tayari kuonesha ushirikiano kwani alikuwa akidai ana kazi za kufanya.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya  Barakael Masaki alipoulizwa juu ya tukio hiyo alisema kuwa bado hajapelekewa taarifa kamili ya tukio lakini atalifuatilia na kulitolea maelezo baadaye.

Mapema Oktoba 10 mwaka huu usiku wa manane  baba wa kijana huyo Bw. Mtaki, akiwa  shambani kwake eneo la Mpemba alivamiwa na watu watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi ambao walimjeruhi yeye na mke wake kwa risasi na mapanga na kumpora vitu vyenye thamani ya sh.milioni Mbili.

Hata hivyo katika tukio hilo hakuna mtu aliye kamatwa wala kupatikana kwa vitu vilivyo porwa hadi leo kuhusiana na tukio hilo.

Post a Comment