Ads (728x90)

Katika hali isiyo ya kawaida mtu mmoja ambaye hakufahamika jina lake alionekana karibu na Rais wa Marekani Barack Obama akijishughulisha na kutafsiri lugha ya alama kwa watu maalumu VIZIWI na baadaye kubainika kuwa mtarjumani huyo hakuwa akitafsiri lugha hiyo kama inavyofahamika dunia nzima wakati wa ibada ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela.

Mtarjumani huyo ambaye alipea ridhaa ya kuwa karibu na Rais wa Marekani ambaye amekuwa akiambatana na ulinzi wa hali ya juu kila aendako ameushanga za ulimwengu kwa namna ambavyo alipata fursa hiyo ya kuwa na Rais Obama ilhali si mweledi wa kazi hiyo.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo ya kiusalama kwa viongozi wamedai kuwa jambo hilo ni hatari kwa kuwa upo iuwezekano wa mtu yoyote kujifanya ni mweledi wa lugha ya alama na akawa karibu na kiongozi wa nchi kisha akaleta madhara kwa kiongozi huyo.

''Inashangaza...hawa watu wanaojifanya ni watu wa usalama walikuwa wapi hadi huyu mtu anakaa karibu na Viongozi na kujifanya anatafsiri lugha ya alama bila kufahamu lugha hiyo,''alisema mstaafu mmoja wa Usalama wa Taifa ambaye hakupenda kutajwa jina lake kutokana na maadili ya kazi hiyo.
Mkalimani Feki akifanya vitu vyake karibu kabisa na Rais Barack Obama.

Picha mbalimbali za mtarjumani Feki alipokuwa mkabala na Rais Obama wakati akihutubia dunia katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela


Alisema kuwa upekuzi wa kiusalama huanzia kujua sifa ya mtu kabla ya kupewa kazi kubwa kama hiyo na kwamba inavyoonekana jamaa huyo hakupekuliwa wala hajulikani vyema taaluma yake jambo ambalo ni hatari kwa Taifa lolote lile.

''Huyu jamaa alikuwa anatafsiri upuuzi na ujinga mtupu, hakuwa anatafsiri chochote zaidi ya kunyoosha nyoosha vidole kwa mbwembwe, sijui alikuwa na maana gani kuwepo karibu na vongozi wakuu wa nchi, mara nyingine inaweza kusababisha madhara, umakini unatakiwa katika jambo la aina hii,''alisema.

Kwa upande wake Mkalimani wa Ishara kutoka Chama cha Viziwi nchini Afrika Kusini(Deaf SA) Delphin Hulngwane alisema kuwa mtarjumani huyo hakuwa akitafsiri chochote zaidi ya upuuzi tu na kwamba kila alichokuwa akikifanya kilikuwa katika makosa na kuwa kwa kuonesha kuwa hakuwa anajua lolote katika lugha maalumu ya alama alishindwa hata kusema neno Ahsante.

Wakati hali hiyo ikitokea imeelezwa kuwa Serikali nchini Afrika Kusini inamtafuta mkalimani huyo ambaye hakufahamika vyema ni wapi alikotokea ingawa inadaiwa alikuwa na Pasi zilizotolewa kwa ajili ya usalama wa eneo hilo la Uwanja wa Soccer City ambako alikuwa akitafsiri alama za viongozi waliokuwa wakita salamu za Rambirambi wakati wa ibada ya kumuaga Hayati Nelson Mandela siku ya Jumanne.

Inaelezwa kuwa tukio hilo kwa jamaa huyo si la kwanza na kwamba kuna wakati alishawahi kufanya hivyo hivyo kwenye sherehe moja ya chama kinachotawala nchi hiyo ANC ambapo Rais Jacob Zuma alikuwa akihutubia.

Post a Comment