Ads (728x90)


‘’Kila kiongozi huja na mabadiliko yake ili kukamilisha ufanisi wake wa kazi, Malinzi kaja na safu yake kwa mtazamo alionao, nimevunja mkataba na Timu ya Taifa, sijutii uamuzi wake kwa kuwa ndivyo alivyoona inafaa, nimepokea kwa mikono miwili,mabadiliko haya,’’Ndivyo alivyoeleza   kocha Mdenish Kim Poulsen aliyelazimika kuvunja mkataba wake wa kuifundisha timu ya Taifa kutokana na mtazamo wa Rais wa sasa wa TFF Jamal Malinzi.

Aliyekuwa Kocha wa Stars Kim Poulsen
Rais wa TFF Jamal Malinzi
Rais Mstaafu wa TFF Leodgar Tenga
Kutokana na mtiririko wa mambo mengi yaliyojiri kabla ya uteuzi katika mchakato wa kuwania kiti cha Urais wa chama Cha Mpira wa Miguu nchini TFF yapo mengi ya kujifunza juu ya mustalabali wa soka la Tanzania na aina ya viongozi wanaokalia kiti hicho.
Malinzi anakuwa ni Rais wa Pili tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Soka nchini TFF baada ya kile kilichokuwa chama cha Mpira wa miguu nchini FAT.
Matumaini ya soka la Tanzania hutegemea zaidi mtazamo wa kiongozi aliye madarakani ingawa kiongozi huyo hafanyi kazi kama yeye bali hufanya kwa niaba ya taasisi nzima, bali uamuzi wa juu wa kiongozi ndio unaoonekana kuheshimiwa zaidi.
Inawezekana kwa kujua kuwa uamuzi unaotolewa hutokana na maamuzi ya jopo la viongozi wa TFF ndio hasa imekuwa sababu ya kubadilisha safu ya uongozi wa juu ili kumrahisishia utendaji Rais Malinzi katika maamuzi yake.
Sipendi kusema mengi yaliyosemwa hapo awali juu ya ‘Interest’ iliyooneshwa na kiongozi huyu hadi ikatafsiriwa kuwepo kwa ubaguzi na hata kueleza kuwa kuna ukabila unaingizwa katika soka la Tanzania, bali kinachoendelea kutendeka kinaonesha dira ya kutumbukia mtaroni kwa soka letu.
Ipo hoja miongoni mwa wadau wa soka wakielezea mtazamo wao juu ya Malinzi kama kweli ana uchungu na soka la nchi yetu ama anachokifanya ni njia ya kujijengea hadhi na heshima binafsi kutokana na maamuzi anayoyafanya ndani ta soka la nchi yetu.
Tunaweza kusema Malinzi ana  uchungu sana na soka la nchi yetu hata kuamua kukatisha mkataba wa Kim Poulsen nyuma ya miezi minane na hata kulazimika  kutoa fedha zake za mfukoni, ingawa si muhimu kujua atazirudishaje fedha hizo mfukoni mwake kwa kipindi cha uongozi wake, ‘’hapa tuiachie TAKUKURU ifanye kazi yake’’.
Ninavyokumbuka Poulsen aliingia nchini akitokea Denmark mwaka 2010 akifundisha vijana wa chini ya miaka 17 Serengeti Boys na wale wa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes  na baadaye kuwa kocha wa timu ya Taifa akirithi mikoba ya mtangulizi wake Mdenish mwenzie Jan Poulsen.
Poulsen amedumu katika Timu ya Taifa tangu Mei 14 2012 na kukamilisha safari ya siku 645 tangu aanze kuifundisha Stars akizidiwa na mtangulizi wake Jan aliyedumu na Stars kwa takribani siku 730 ambapo baadaye hakuongezewa mkataba mwingine na TFF kuendelea kuifundisha Stars.
Tutaendelea kubanwa na historia ya soka la nchi yetu kufundishwa na makocha wakigeni huku kila kocha aliyepata kuifundisha timu ya Taifa akiondoka na historia ya aina yake kutokana na mtazamo wa viongozi waliopo madarakani.
Yapo mengi ya kujiuliza juu ya mabadiliko anayoyafanya Malinzi kuanzia pale alipoamua kupangua safu ya viongozi wa juu wa TFF ambapo kwa hatua hiyo hoja nyingi zinaibuliwa kwa kile kilichoelezwa kuwa anaendeleza ukabila ijapo alikanusha taarifa hizo kuwa yeye anafuata watendaji bora hafuati kabila la mtu.
Ijapokuwa ni mapema kuelezea mustakabali wa soka la nchi yetu kwa siku 100 za Malinzi bali ni muhimu kuweka angalizo kwa namna ambavyo ameanza kwa kasi ya kujenga chuki kwa watendaji waliomtangulia katika uongozi wake…!!
‘’Wacha Niseme Ya Moyoni Mwangu juu ya Mtazamo Wangu Na Mustakabali wa Soka Letu Nchini’’Alamsiki!!!

Post a Comment