Ads (728x90)

MAPATO kwa mechi ya ligi ya Vodacom kati ya timu za Mbeya City ya Jijini Mbeya na Simba ya Jijini Dar es salaam yamevunja rekodi ya michezo yote iliyowahi kuchezwa nje ya Jiji la Dar es salaam kwa kuingiza kiasi cha sh. milioni 105.

Mechi iliyowahi kuingiza kiasi kikubwa cha mapato katika uwanja huo ni ile iliyochezwa kati ya Timu ya Mbeya City na Yanga ya Dar es salaam katika uwanja huo mwaka jana na kuingiza kiasi cha sh. milioni 100.Katika mechi hiyo ya jana ambayo timu hizo zilitoka sare ya goli 1-1,jumla ya tiketi 21,000 ziliuzwa ambapo tiketi moja iliuzwa kwa sh.5,000 hata hivyo tiketi hizo ziliisha mapema na kusababisha baadhi ya mashabiki waliohitaji kushuhudia mchezo huo kubaki nje ya uwanja.

Mbali na mashabiki waliokosa tiketi kushindwa kuingia uwanjani, mwandishi wa habari hizio alishuhudia umati wa mashabiki ambao walikuwa na tiketi mkononi kuendelea kubaki nje hadi kipindi cha kwanza kinamalizika kutokana na msururu mrefu wa kuingia uwanjani.

Wapenzi wa soka walianza kukata tiketi  majira ya saa 2:00 asubuhi na kuanza kuingia uwanjani saa 4:30 ambapo hata hivyo msururu  mrefu wa wapenzi waliohitaji kuiona mechi hiyo ilisababisha kushindwa kuingia uwanjani kwa wakati.

Katika hatua nyingine baadhi ya watu walipata fursa ya kujiongezea kipato kwa kununua vitabu vya tiketi za mechi hiyo na baadaye kuziuza kwa bei ya sh.8,000 hadi sh.10,000 badala ya bei ya kawaida iliyopangwa na TFF ya sh. 5,000 kwa kila tiketi.

Mbali na tiketi hizo kuuzwa kwa bei ya juu bado kuna baadhi ya tiketi zilionekana kutokidhi viwango ambapo mwandishi wa habari hizi alishuhudia mmoja wa wasemaji wa timu ya Mbeya City Freddy Jackson akiwa na tiketi zisizopigwa mhuri na kusema kuwa tiketi hizo zimeghushiwa kwa nia ya kuhujumu mapato ya mchezo huo.

Akizungumza mapato ya mchezo huo Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mbeya Elias Mwanjala alisema kuwa  jumla ya tiketi 21,000 ziliuzwa na kumalizika na kuingiza mapato jumla ya sh. milioni 105.

Katika mapato hayo kila timu ilipata kitita cha sh. milioni 25.3 ambapo sh.milioni 12.8 zilibaki kwa ajili ya uwanja,sh.milioni 7.7 kwa ajili ya maandalizi na sh. milioni 7.7 kwa ajili ya kamati ya ligi ilhali sh. milioni 3.8 zilikuwa ni kwa ajili ya chama cha mpira wa miguu TFF.

Post a Comment