Ads (728x90)

Mwamuzi wa mchezo kati ya Lipuli ya Iringa na  Kimondo ya Mbozi Mbeya Cleaner Kabara akitolewa nje ya uwanja huku baadhi ya mashabiki wakimzonga kwa ajili ya kutaka kumpiga

Mwamuzi Kabara akiwa katika wakati mgumu akizongwa na mashabiki katika mchezo baina ya Lipuli na Kimondo jana jioni

Wachezaji wa Lipuli baada ya mechi na Kimondo jana jioni uwanja wa Samora

Waamuzi wakitoka nje ya uwanja wakati wa mapumziko







Benchi la Timu ya Lipuli

Benchi la timu ya Kimondo






MCHUANO wa ligi daraja la kwanza imeendelea mwishoni mwa wiki kwa sare ya Bao 1-1 katika uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa kwa kuzikutanisha timu mbili za Lipuli ya mjini humo na Kimondo SSC ya wilayani Mbozi mkoani Mbeya.
Mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani mkali ulimalizika kwa mwamuzi wa kati  wa mchezo huo Cleaner Kabara kutoka jijini Dar es salaam kutolewa nje huku akirushiwa mawe na mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa timu ya Lipuli kwa kile kilichodaiwa kuwa alikuwa anafanya upebdeleo.
Lipuli ambayo ilikuwa ikicheza katika uwanja wake wa nyumbani iliingia dimbani kwa nia ya kulipiza kisasi baada aya kuchabangwa magoli 2-0 na timu hiyo katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa katika uwanja wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya.
Timu ya Lipuli ilikuwa ya kwanza kuliona lango la timu ya Kimondo dakika ya  tatu ya mchezo bao lililofungwa na mchezaji Abdallah Said baada ya kuwatoka walinzi wa timu ya Kimondo na kumalizia kwa shuti kali lililomuacha golikipa wa timu ya Kimondo Abraham Simasiku akichupa bila mafanikio.
Mara baada ya kufungwa goli hilo Kimondo walianza kuishambulia Lipuli kama nyuki hatimaye dakika 9 baadaye mshambuliaji Asifiwe Lwinga aliyevalia jezi nambari 14 mgongoni aliwatoka walinzi watatu wa timu ya Lipuli na kuambaa ambaa na mpira golini mwa timu hiyo baadaye akakwatuliwa na mchezaji wa timu ya Lipuli George Mbelwa aliyevalia jezi nambari 2.
Mwamuzi wa mchezo huo Kabara alilazimika kutoa penati kwa timu ya Kimondo kufuatia mchezo mbaya aliyechezewa Asifiwe ambapo mnamo dakika ya 12 Baraka Mtafya wa Kimondo aliipatia timu yake bao la kusawazisha kwa shuti lililoingia pembeni mwa goli na kumuacha golikipa wa Lipuli Green Pour akichupa bila mafanikio.
Baada ya Kimondo kusawazisha goli hilo mchezo huo ulianza kutawaliwa na rafu za hapa na pale na kusababisha mwamuzi na washika vibendera  kuwa na wakati mgumu kutoa uamuzi kutokana mashabiki waliokuwa karibu na uwanja kutoa maneno ya vitisho.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilitoka uwanjani zikiwa zimefungana bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa mbwembwe zaidi za rafu za hapa na pale na kulazimika mwamuzi kusimamisha mchezo mara kadhaa na kutoa mipira ya faulo ambayo hata hivyo ililalamikiwa na wachezaji wa timu ya Lipuli ambao ndio walioonekana kucheza faulo zaidi.
Dakika ya 52 Golikipa wa timu ya Kimondo Abraham Simasiku alipigwa kipepsi na mchezaji wa timu ya Lipuli George Mbelwa na baadaye kuwaumiza wachezaji wengine wawili wa timu ya Kimondo ambao ni Casmir Frank na Joshua Omar ambapo Omar alilazimika kutoka nje ya uwanja na kuingia Guna Benedict.
Dakika chache baadaye Golikipa Simasiku alizidiwa na maumivu ya jicho baada ya kupigwa kipepsi na Mbelwa wa Lilpuli na kulazimika kutoka nje ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Emmanuel Othman.
Hali ya mchezo iliendelea kuwa na dosari kwa kipindi hicho hali iliyomfanya mwamuzi kutoa jumla ya kadi tano za njano ambapo tano kati ya kadi hizo alizitoa kwa wachezaji wa timu ya Lipuli.
Kipyenga cha kumaliza mchezo kilipopulizwa na mwamuzi wa mchezo huo wachezaji wa timu ya Lipuli walimzonga mwamuzi huyo na kuanza kumsukuma huku na huko hali iliyosababisha baadhi ya wasamaria wema kuingia uwanjani kumuokoa mwamuzi huyo huku baadhi ya mashabiki wakirusha mawe.
Dakika chache baadaye gari la kikosi cha kutuliza ghasia FFU liliingia uwanjani kwa mbwembwe na kuwatawanja baadhi ya mashabiki waliokuwa wanasababisha vurugu katika mchezo huo.
Kwa mchezo huo timu ya Lipuli imefikisha pointi 14 kwa michezo 10 ilhali timu ya Kimondo imefikisha jumla ya pointi 11 kwa michezo 10 Burkina Faso ya Moro pointi 11 kwa michezo 10.
Lipuli:Green Pour,Stone Peter,Saimon Nsajigwa,Joram Nasson,Hassan Matitu,Samwel Chitete,Meshack Mwaitelile,Innocent Boniface,George Mbelwa,Nonole Mabena na Abdallah Mativila.
Kimondo:Abraham Simasiku/Emmanuel Othman,Baraka Mtafya,Gefrey Mlawa,Amirson Mohamed,Patrick Mwamengo,Daud Mwaipaya,Mashaka Mwakyoma,Geofrey Mwashiuya,Kasmir Mwamboka, Asifiwe Lwinga,Joshua Omar/Guna Benedict.

Post a Comment