Ads (728x90)

Maafannde wa Jeshi la Magereza Prison ya Mbeya leo jioni imeendeleza ubabe wa kushinda mechi za mzunguko wa pili wa Ligi ya Vodacom kwa kuwabugiza maafanbde wenzao timu ya JKT Ruvu mabao 6-0.
Mchezo huo ambao ulipigwa katika dimba la Sokoine huku huku ukihudhuriwa na watazamaji wachache na  mvua ikinyensha na kutotesha uwanja huo ulitoa fursa kwa timu ya Prison kufanya vyema katika uwanja wake wa nyumbani.
Katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo Timu ya JKT Ruvu iliwachabanga Maafande wa Prison mabao 3-1 hali ambayo ilisababisha mashabiki kuja juu na kusababisha aliyekuwa kocha wa timu hiyo Jumanne Chale kutimuliwa katika timu hiyo.
Prison ikiwa chini ya kocha wake David Mwamwaja walianza kuhesabu karamu hiyo ya magoli dakika ya 20 na Omega Seme ambapo alipiga shuti hafifu lililomkuta golikipa wa JKT Ruvu Shaaban Dihile aliyeudaka na kumponyoka na kisha kutinga wavuni.
Goli la pili  lilifungwa na Nurdin Choma dakika ya 29 baada ya piga nikupige katika lango la JKT ambapo dakika 34 mchezaji wa Prison Lugano Mwangama aliipatia timu yake goli la tatu kwa shuti iliyopigwa kutokea upande wa kushoto na kumuacha golikipa Dihile akichupa bila mafanikio na mpira kutinga wavuni.
Karamu ya magoli katika kipindi cha kwanza ilihitimishwa dakika ya 44 ambapo mchezaji wa timu ya Prison Peter Michael aliipatia timu yake goli la nne alilofunga kwa kichwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya JKT Ruvu kufanya mabadiliko ambapo golikipa Dihile alipumzika na nafasi yake kuchukuliwa na Sadikc Maksi.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweeza kuisaidi timu ya JKT Ruvu ambapo golikipa Maksi alionekana kung'aa dakika chache za mwanzo wa kipindi cha pili na baadaye dakika ya 70 mchezaji wa timu ya Prison aliiandikia timu yake bao la tano lililotokana na shuti kali iliyomuacha kipa Maksi akichupa golini bila mafanikio.
Baada ya kuingia kwa goli hilo kocha msaidizi wa timu ya JKT Ruvu Nelson Haule alifanya mnabadiliko mengine kwa kumtoa mchezaji Amos Magisa na kumuingiza Karage Mgunda, hata hivyo hakukuwa na mafanikio yoyote kwa timu hiyo ambapo wachezaji wa JKT RUVU walionekana kushindwa kuutawala mchezo kutokana na kuteleza uwanjani na kuanguka kila walipolikaribia lango la timu ya Prison.
Karamu ya magoli kwa siku ya leo ilihitimishwa na mchezaji Peter Michael ambaye alifunga bao la 6 dakika ya 82 baada ya mashambulizi yaliyotokea katika lango la JKT lililosababisha wachezaji wa timu hiyo kupoteana na kumfanya Michael apate fursa ya kufunga bao hilo kiurahisi.

Hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa Prison ilitoka kifua mbele kwa mabao 6-0 ambapo katika hatua nyingine ubao wa magoli katika uwanja huo ulisomeka magoli 5 1-0 kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hakukuwa na ubao wa magoli zaidi ya 6 katika uwanja huo wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Post a Comment