Ads (728x90)

Waziri  Mkuu Mizengo Pinda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Stendi mpya ya Kisasa iliyopo mkabala na uwanja wa Nane Nane Jijini Mbeya leo mchana.


Waziri Mkuu akiwapungia wananchi mara baada ya kuwasili katika eneo la Stendi mpya ya kisasa Nane Nane Jijini Mbeya leo asubuhi.

Waziri Mkuu Pinda akikata utepe kufungua maonesho ya Nane Nane yanayofanyika kikanda Jijini Mbeya leo mchana, maonesho hayo yanatarajiwa kuwa kilele chake siku ya Agosti 8.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda amezindua Stendi ya Kisasa Jijini Mbeya na kuitaka Halmashauri ya Jiji hilo kuboresha miundo mbinu ili ikidhi mahitaji ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga.
Akizungumza na wananchi waliokusanyika wakati akizinduka Stendi hiyo iliyopo mkabala na Uwanja wa Nane Nane, Waziri Mkuu alisema kuwa Stendi hiyo itakuwa na manufaa zaidi iwapo wafanyabiashara Wamachinga watapatiwa maeneo ya kufanyia biashara zao.
Alisema wafanyabiashara hao wamelazimika kukaa katika maeneo ambayo yanaonekana kuwa kero kwa wananchi wengine kutokana na ukweli kuwa wanawafuata wateja kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu hivyo iwapo wataboreshewa miundo mbinu tatizo hilo linaweza kuondoka.
Alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa maeneo ya biashara kwa wamachinga lakini hawapaswi kurundikwa mahala pamoja na kuwa hili litasaidia kuondoa msongamano na kero kwa watu wengine.
''Msiwarundike muwaweke kwa utaratibu ili wapewe huduma muhimu za maji na vyoo...tengeni fedha kwa jambo hili, ili hapa pawe mahala pa kupigiwa mfano,''alisema na kusisitiza.
Alisema kuwa ilifika mahala tatizo la Machinga hasa maeneo ya Mwanjelwa lilikuwa likimpa hofu kubwa alipokuwa akipita na gari lakini hata hivyo hofu hiyo imetoweka baada ya kujua kuwa tatizo lao ni kupatiwa maeneo muhimu ya kufanyia biashara zao.
''Wakati mwingine nilikuwa na hofu nilipokuwa napita maeneo ya Mwanjelwa..ni hofu ya kibinadamu, maana sijui nini kitatokea lakini nikijaribu kuwapungia mkono, naona nashangiliwa, nikajua kuwa hapa hakuna tatizo kama linavyosemwa, bali tatizo ni kuwaboreshea miundo mbinu na kuwatengea maeneo ya biashara,''
''Napenda niseme ukweli serikali za mitaa mmekuwa mkifanya vizuri katika utendaji nimepata uzoefu tangu nikiwa Naibu Waziri, wekeni mifumo ya kisasa katika ukusanyaji wa mapato ili muendelee kuwa na kupata hati safi katika miji na majiji yenu,''alisema.
Sanjari na kuzindua Stendi hiyo ya kisasa Waziri Mkuu pia amezindua maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayofanyika kikanda Jijini Mbeya ambayo yanahusisha mikoa sita ya Mbeya, Iringa,Rukwa, Katavi Njomba na Ruvuma na kuwataka wakulima kulima mazao ya chakula na bisahara.

Post a Comment