Ads (728x90)






CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jijini Mbeya kimetoa onyo kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutotumia jina lao kwa propaganda za kuvuta wananchi kwenye mikutano yao na kwamba wakiendelea kufanya hivyo chama hicho kitaanzisha vurugu katika mikutano ya CCM.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hotel ya Mbeya Peak jana Mwenyekiti wa CHADEMA Jiji la Mbeya Bw.John Mwambigija alisema kuwa CCM imekuwa ikiwalaghai wananchi  kwamba kuna vigogo wa CHADEMA waliojiunga na CCM ili kujaza watu kwenye mikutano yao.

Alisema kuwa katika mkutano wa Agosti 8 uliohutubiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM)  Taifa Bw. Abdallah Bulembo ilitangazwa kuwa kuna vigogo wa CHADEMA waliojiunga na CCM ambao ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee CHADEMA Bw.Ambindwile Mwantondo na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana BAVICHA Bw. Frank Fumbo.

Bw. Mwambigija alisema kuwa katika chama chao hakuna viongozi wenye majina hayo na kwamba walichokifanya CCM ni kutumia jina la CHADEMA kujipa umaarufu ambao umepotea katika jimbo la Mbeya na kuongeza kuwa iwapo CCM itaendeleza propaganda hizo chafu, watavuruga mikutano yao.

''Sisi hatutumii jina la CCM kunadi chama chetu, wao wanawalaghai wananchi kwa kutumia jina la Chama chetu,uvumilivu umefika mwisho, wakiendelea tunatumia vijana wetu kuvuruga mikutano yao,''alisema, Bw. Mwambigija.

Alimtambulisha Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA kuwa ni Bw. Edward Mwakagenda na Mwenyekiti wa BAVICHA kuwa ni Lule Mwashamba na kukukanusha idadi ya wanachama 360 wanaotajwa kujiunga na CCM katika mkutano huo.

‘’Hakuna mwanachama yoyote aliyejiunga na CCM tangu tumalize uchaguzi wa Udiwani Kata ya Iyela ambao tulishinda kwa kishindo, wanachokifanya CCM ni propaganda ambazo zimepitwa na wakati,wakiendelea hatutavumilia, tutavamia mikutano yao na kuvuruga’’alisisitiza Bw. Mwambigija.

Alisema CHADEMA haijapoteza mwanachama yoyote na kwamba sasa kimejipanga kufanya mikutano ya hadhara kaunzia Agosti 18 ambapo Mbunge wa Arusha, Godbless Lema,ambaye ataambatana na wabunge wenzie Tundu Lissu na Halima Mdee watafanya mikutano katika Jiji la Mbeya,Mlowo, Tunduma, Tukuyu, Kyela, Chunya na Ileje katika operesheni maalumu ya ‘M4C’ ‘CHADEMA ni msingi.’

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Bw.Mwakagenda alisema kuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee na kuwa katika baraza lake hakuna mtu anayeitwa Mwantondo.

Post a Comment