Ads (728x90)

Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu madhehebu ya Answar Sunna wakiungana na waislamu wengine duniani katika ibada ya swala ya Idd katika Viwanja vya Kiwanja Ngoma Jijini Mbeya leo asubuhi







WAUMINI wa dini kiislamu madhehebu ya Answar Sunna mkoani Mbeya wameswali swala ya Idd leo katika Viwanja vya Kiwanja Ngoma na kuwataka Mashekhe kutotumia lugha za uchochezi zinazojenga chuki baina ya Waislamu.

Akizungumza na umati wa waislamu waliojumuika katika ibada hiyo ya kukamilisha kwa mfungo wa mtukufu wa Ramadhani, imamu aliyeswalisha swala hiyo Shekhe Ibrahimu Bombo alisema kuwa baadhi ya Mashekhe wakubwa wamekuwa wakitumia vyombo vya habari kujenga chuki kwa waislamu.

Alisema, swala la ibada ni wajibu kwa waislamu wote na kwamba yapo mambo ambayo waislamu wanatofautiana katika kufanya ibada maalumu ambayo hutokana na uelewa na kwamba jambo hilo halipaswi kuleta mgongano baina ya waislamu.

‘’Wapo  mashekhe wa taasisi fulani hujitokeza katika vyombo vya habari na kuleta kejeli dhidi ya wengine kuhusu uelewa wa mambo, hakuna mamlaka iliyo juu ya sheria inayopaswa kuwakejeli ama kuwatukana wengine, jambo hili lisipoangaliwa linaweza kuleta chuki,’’alisema Shekhe Bombo.

Alisema  uislamu unajengwa kwa umoja na mshikamano na kama yapo mambo ambayo waislamu wanapishana yanapaswa kujadiliwa kulingana na mafundisho ya dini hiyo badala ya kundi la watu fulani kujiona ni bora zaidi ya kundi jingine.

‘’Sisi sote tunafuata mafundisho ya Kitabu cha Koran na Hadithi za Mtume Muhammad (SAW) anayefuata mafundisho haya kwa dhati hawezi kukurupuka na kukejeli wengine,’’alisisitiza na kuongeza.

‘’Wanaohoji kwa nini tunaswali leo, tunasema kuwa sisi tunaswali mwezi wa Kimataifa ambao dunia nzima wanaswali,wale watakaoswali kesho hakuna anayewazuia na wala ninyi msiwakejeli ambao leo bado wamefunga na wao hawapaswi kuwakejeli ninyi ambao leo mnakula mchana,’’alisema.

Kwa upande wake Shekhe Rajab Nzunda alisema kuwa Waislamu wanapaswa kufuata na kuendeleza mafundisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo wengi waliamua kuacha maasi na kujikita katika ibada.

‘’Mwezi wa Ramadhani umetufundisha, uchamungu, hatupaswi kurejea tena katika maovu ambayo yalitakaswa na Mwezi huu,tusirejee tena kufanya madhambi, tuendeleze ibada na uchamungu tuliodumu nao kwa mwezi mzima,’’alisema Shekhe Nzunda.

Post a Comment

  1. Wallahi mtihani mkubwa,Ilobaki kuomba rehema toka kwa mola. Nauliza nini maana ya umoja ikiwa huyo anayehubiri anatangulia kusaliti kwa vitendo na kula iddi kabla ya kutangazwa na viongozi.Sasa hiyo sio uchochezi?

    ReplyDelete
  2. Idd hutangazwa kwa kuandama kwa mwezi si kwa kutangazwa na viongozi

    ReplyDelete