Ads (728x90)

-CHUNYA-

Baadhi ya wakazi wa Chunya mkoani Mbeya wakiwa katika makundi kujadili Rasimu ya Katiba Mpya
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Chunya wakiwa katika mjadala wa Rasimu ya Katiba Mpya
WACHANGIAJI katika rasimu ya Katiba mpya wilayani Chunya mkoani Mbeya wamependeleza kuwa Mwenge wa Uhuru, uwekwe makumbusho na uwe ni sehemu ya Nembo za Taifa badala ya kuiingizia gharama  serikali kwa kukimbizwa kila mwaka.

Wakichangia katika mkutano wa kuchangia Rasimu ya Katiba mpya ulioitishwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Kituo cha Msaada wa Kisheria na Unasihi(CHULECU) katika mji mdogo wa Mkwajuni wilayani humo, wajumbe wa mkutano huo walipendekeza kuwa mwenge huo uwekwe katika Jumba la Makumbusho ya Taifa ili iwe kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

‘’Tunaomba mwenge wa Uhuru uwekwe makumbusho ya Taifa, kila mwaka unakimbizwa ukiwa na ujumbe ambao mwisho wake hauna utekelezaji, unagharimu fedha nyingi za walipa kodi, matunda yake hayaonekani,’’alisema Bw.Bahati Komba mkazi wa kata ya Mbuyuni.

Alisema kuwa hata hivyo pamoja na mwenge huo kuitwa ni Mwenge wa Uhuru tafsiri yake imepotoshwa kwa kuwa uliwashwa mwaka 1961 wakati Tanganyika ilipopata Uhuru wake na kwamba badala yake mwenge huo unawakilisha pande mbili za Tanganyika na Zanzibar.

‘’Tuwekwe wazi kuwa huu ni Mwenge wa Uhuru wa Tanganyika mwaka jana uliwashwa Zanzibar ambako  Uhuru wao ni mwaka 1964, kama tumeamua uwe ni mwenge wa pande zote basi uitwe Mwenge wa Taifa na uwe ni sehemu ya nembo za Taifa,’’alisema Bw. Komba.

Alisema kati ya alama za Taifa ambazo ni Bendera na Wimbo wa Taifa Mwenge nao uwe ni sehemu ya alama hizo ambao utahifadhiwa katika makumbusho na kuenziwa kama zinavoenziwa kumbukumbu zingine za nchi yetu.

Alisisitiza kuwa dhana ya Mwenge huo ni kuleta amani pasipo na matumaini kuondoa chuki pale penye dharau lakini hata hivyo pamoja na ujumbe mzuri wa Mwenge hakuna matokeo wala mabadiliko yoyote yaliyotokea mara baada ya Mwenge huo kumaliza mbio zake hivyo ni vyema ukapumzishwa na ukawekwa katika historia.

Naye Bi. Margreth Sigereti mkazi wa kijiji cha Mkwajuni alisema kuwa iwapo kuna haja ya kuendelea kuwa na Mwenge huo basi uwekwe Mwenge bandia ambao hauhitaji gharama za mafuta na kwamba gharama kubwa za mafuta ya mwenge zielekezwe kwenye huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na miundombinu.

Bi. Sigereti alisema kuwa miradi mingi iliyowekwa mawe ya msingi na mwenge imekufa na haijaendelezwa hadi sasa na kwamba inawezekana dhana ya Mwenge inatumika kwa ajili ya watu kujinufaisha kutokana na kuanzisha miradi hewa ambayo haina tija kwa wananchi.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Mangala aliyejitambulisha kwa jina la Justasi Wihege alisema kuwa watendaji wabovu ndio wanaosababisha Mwenge wa Uhuru uonekane haina manufaa kwa wananchi na kwamba ni muhimu kwa watendaji wabovu kumulikwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kuweka nidhamu ya utumishi bora.

Naye Bw. Festo Mambwe mkazi wa kijiji cha Mkwajuni alisema kuwa, kumekuwa na dhana ya vitisho juu ya Mwenge wa Uhuru kiasi cha kuupa hadhi kubwa ambayo inawajengea hofu watendaji ilhali ukweli ni kuwa mwenge huo unatumia fedha nyingi za walipa kodi bila matokeo ya matumizi ya mbio za Mwenge kuwekwa bayana.

Wachangiaji hao walishauri kuwa iwapo serikali itaona ni lazima kuwepo kwa mbio za Mwenge, kuwekwe uwazi wa matumizi yake ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji ya miradi mbalimbali iliyofunguliwa na mbio za Mwenge kote nchini na gharama zilizotumika.

xxxxMJINI MBEYA WANAHABARI NAO WALIPATA FURSA YA KUKETI PAMOJA NA KUJADILI RASIMU YA KATIBA MPYA KAMA INAVYOONEKANA PICHANI

Wanahabari Mbeya wakinyoosha mikono kuafikiana jambo na kupitisha uamuzi wa kuondolewa kwa vifungu juu ya Uhuru wa kupata na kutoa habari baada ya kujadili kwa kina Rasimu ya Katiba mpya kwenye vifungu ambavyo vinanyanyasa utendaji kazi wa wanahabari nchini

Post a Comment