Ads (728x90)

Add caption

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Elick Ambakisye katikati akisisitiza jambo katika kikao cha Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Levisson Chillewa

Nyumba hii ambayo imepangishwa kwa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Selfina iliyopo mtaa wa Shimoni, ni kati ya nyumba tatu ambazo zimepangishwa na Halmashauri hiyo kwa miaka 30 lakini mapato yake hayajulikani

Hii ni Bar katika Nyumba inayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ambayo mapato yake yanadaiwa kutafunwa na wajanja

MAMILIONI ya fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi yanayotokana na pango la nyumba 3 za halmashauri hiyo yanadaiwa kutafunwa na wajanja kwa takribani miaka 30, huku baadhi ya watendaji wakidaiwa kuficha vyanzo vya mapato hayo kwa nia ya kujinufaisha.

Fedha hizo ambazo zinatokana na miradi ya nyumba tatu za halmashauri hiyo tangu mwaka 1983 ambavyo ni vitega uchumi vilivyopo mjini Vwawa vimepangishwa kwa watu binafsi huku mapato yake yakidaiwa kuishia mikononi mwa baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo.

Imedaiwa kuwa baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa wakichukua kodi katika nyumba tatu za halmashauri hiyo bila kuziwasilisha ofisini huku wengine wakijimilikisha nyumba hizo na kufahamika kwa wapangaji kama ni wamiliki wa nyumba hizo.

Nyumba  hizo zimepangishwa watu na taasisi binafsi za Tanganyika Famers Association(TFA) Chama Cha Akiba na Mikopo lililopo karibu na soko la Vwawa na nyumba ya kulala wageni ya Mbozi Development Council(MDC) ambazo tangu zilipopangishwa mwaka 1983 hakuna mapato yaliyoingizwa kwenye halmashauri hiyo.

Aidha mwandishi wa gazeti hili alitembelea nyumba hizo na kuwauliza baadhi ya wapangaji kujua ni nani wanayemlipa kodi ya nyumba na kuwataja baadhi ya watu ambao wanadaiwa kuwa ni watumishi wa halmashauri hiyo(majina tunayo) kwamba ndio ambao huwalipa kodi hiyo kwa miaka yote.

Hoja hiyo iliibuliwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na Diwani wa kata ya Ihanda Bw. Joel Kasebele katika maswali ya papo kwa papo kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Levison Chilewa ambaye alitakiwa kutoa ufafanuzi juu ya mahala zinapokwenda fedha za pango za nyumba hizo.

‘’Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupata ufafanuzi juu ya mapato ya fedha zinazotokana na nyumba tatu zinazomilikiwa na Halmashauri yetu, zinakwenda wapi, nyumba hizo ni za Halmashauri mapato yake yanafanya kazi gani?,’’aliuliza Bw. Kasebele.

Katika majibu yake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Chilewa alisema kuwa hajui fedha za nyumba hizo zinakokwenda na kwamba tangu ameingie hapo miaka saba iliyopita hajawahi kupewa taarifa kuhusu mapato ya nyumba hizo na kwamba hata hivyo ofisi yake imewaandikia barua wapangaji ili kujua mkataba wa upangaji wa nyumba hizo.

‘’Lazima niseme ukweli hili jambo nimelikuta, sijui lolote kuhusu mapato ya nyumba hizo, tangu nimefika miaka saba sasa sijapewa mrejesho wowote kuhusu nyumba hizo’’, alisema Bw. Chilewa.

Kufuatia majibu hayo baadhi ya madiwani walisimama ili kupata ufafanuzi zaidi na kuhoji sababu za ofisi ya halmashauri hiyo kuachia mapato ya nyumba hizo kwa takribani miaka 30 bila kufuatiliwa.

Alisema kuwa siku za nyuma hakukuwa na kumbukumbu wala taratibu zozote za vyanzo vya mapato kutoka kwa uongozi uliopita na kwamba nyumba hizo zimeibuliwa hivi karibuni ambapo jitihada zinafanyika ili kujua mikataba ya wapangaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Elick Ambakisye alisema kuwa kikao cha baraza la Madiwani kimeiagiza ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuandaa taarifa sahihi ya kina juu ya vyanzo vingine vya mapato ambavyo fedha zake zinaingia mifukoni mwa wachache.

Post a Comment