Ads (728x90)

Mfano wa Nyoka aina ya Chatu(picha ya mtandao) ambaye anaelezwa kuwepo katika mto unaokatiza katikati ya Jiji la Mbeya
 Picha ya (mtandaoni) ya Nyoka mkubwa aina ya Chatu akimmeza Mamba, nyoka kama huyu anaelezwa kuwepo katika mto unaokatiza katikati ya Jiji la Mbeya na kuwatia hofu wakazi wa maeneo hayo.
 

Daraja Jipya la Saba Saba- Jakaranda ambalo linapita juu ya mto Meta unaoelezwa kuwa una Nyoka mkubwa aina ya Chatu
 




Mkazi wa Jiji la Mbeya ambaye analima pembezoni mwa mto Meta unaodaiwa kuwa una Nyoka Mkubwa aina ya Chatu akielezea kuwepo kwa Nyoka huyo.






Eneo lenye msitu mzito unaodaiwa kuwa umehifadhi nyoka mkubwa aina ya Chatu ambaye anatishia wakazi wa Jiji la Mbeya.
 

Wakazi wa Jiji la Mbeya wakikatisha daraja dogo linalopitia mto Meta unaodaiwa kuwa una nyoka mkubwa aina ya Chatu.

Mto Meta unaokatiza katikati ya Jiji la Mbeya unaodaiwa kuwa umehifadhi Nyoka aina ya Chatu ambaye amekuwa tishio kwa wakazi wa Jiji la Mbeya

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya wakikatiza katika daraja linalopitia kwenye mto Meta  unaodaiwa kuwa ni hatari kwa  Nyoka aina ya Chatu wakipita kutokea upande wa Sabasaba kuelekea mtaa wa Uhindini na Jakaranda

Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Mazanda ambaye hupata riziki yake kwa kuchanja kuni eneo linalodaiwa kuwa na nyoka aina ya Chatu.

April 18 mtandao huu pamoja na mtandao Washirika Fasihi Media Inc kupitia Mkwinda Blog ulifanya utafiti na hatimaye kuibua kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya habari kwamba wakazi waishio maeneo ya katikati ya Jiji la Mbeya unapopita mto Meta  karibu kuanzia Hotel ya Rift Valley, shule ya Sekondari ya Mbeya, shule ya English Medium ya River side, shule ya sekondari Meta na shule za jirani za maeneo hayo kama Sisimba na Azimio kwamba eneo hilo linaelezwa kuwa ni hatari kutokana na kuwepo kwa mdudu mkubwa Nyoka aina ya Chatu.
Kufuatia utafiti huo wa kina uliosomwa na watu lukuki hatimaye Halmashauri ya Jiji la Mbeya imetoa tamko rasmi kuwa eneo hilo ni hatari.na kwamba watu wakazi wa Jiji la Mbeya wanapaswa kuchukua tahadhari wanapopita eneo hilo ikiwemo kutokuwa mtu mmoja.
Hata hivyo mwandishi wa Blogu hii ametembelea maeneo hayo hatari na kubaini kuwa hakuna tangazo lolote la tahadhari lililowekwa maeneo hayo zaidi ya tangazo hilo kuwepo kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kusikika katika vyombo mbalimbali vya habari.
Baadhi ya watu waliozungumza na mtandao huu wamesema kuwa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi ilipaswa kwenda mbali zaidi kwa kuweka tahadhari na ILANI katika eneo hilo hatari sanjari na kufanyika msako mkali dhidi ya mdudu huyo hatari.
''Halmashauri inataka kuona mtu ameliwa na nyoka ndipo waje kutoa msaada, wakati huu ndio wakati muafaka wa kupambana kumsaka mdudu huyo,''alisema mmoja wa wananchi aliyekutwa eneo linaloelezwa kuwa ni hatari kando ya mto huo.
Alisema kuwa taarifa za kuwepo kwa Nyoka huyo eneo hilo ni za muda mrefu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa hivyo aliiomba Halmashauri ya Jiji kuchukua hatua za dhati katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama kwa wakazi wa Jiji la Mbeya.
 Naye Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Mazanda aliyekutwa anakata kuni eneo hilo alisema kuwa taarifa za kuwepo kwa Nyoka huyo zimetishia usalama wa watu wanaopata riziki ya kuchanja kuni eneo hilo kutokana na akina mama wengi kuchanja kuni maeneo hayo na wengine kulima bustani kando ya mto.
Alisema Nyoka aina hiyo ni hatari anaweza kumeza mbuzi au mbwa na kukaa mwezi mzima bila kuonekana hadi mbwa au mbuzi aliyemmeza kuoza na anapoonekana hujitokeza wakati wa asubuhi jua linapotokeza na wakati wa jioni jua linapozama.
Baadhi ya wakazi wa Jiji waishio kando na eneo hilo wameelezea hofu yao juu ya kuwepo kwa Nyoka huyo na kusema kuwa taasisi zinazohusika zinapaswa kuchukua hatua za haraka kabla madhara makubwa hayajatokea.
Zipo taarifa zilizozagaa kwamba kuna mbuzi mmoja alikuwa amefungwa eneo hilo na kuwa kuna kijana mmoja alitumwa kwenda kumpa maji mbuzi na kuwa alipofika eneo alipofungw mbuzi huyo alikuta mbuzi anamezwa na Chatu akimalizikia miguuni.
Hata hivyo taarifa hizo ambazo bado hazijathibitishwa zinadai kuwa Nyoka huyo anakadiriwa kuwa na urefu wa takribani futi nane na amekuwa akijificha bila kuonekana katika maeneo ya Mto na daraja jipya la Jakaranda.
Aidha taarifa hizo zinasema kuwa Nyoka huyo amekuwa akiranda randa kwa kificho katika maeneo ya mto huo kuanzia Hotel ya Rift Valley,Shule ya English Medium ya Riverside, Shule ya Sekondari ya Mbeya na shule ya Sekondari ya Meta.

Post a Comment