Ads (728x90)

Simon Shonde, Diwani wa Iyula akionesha hisia zake za kutaka kuwawajibisha watendaji wanaokiuka taratibu za kiutumishi.
Diwani wa Halungu Samson Simkoko akielezea utaratibu aliouita mbovu wa serikali wa kuwalinda watumishi wanaoshindwa kuwajibika kwenye Halmashari.
Diwani wa Kata ya Ihanda Joel Kasebele akichangia hoja ya kutokuwa na imani kwa Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo.

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Allan Mgullah akisisitiza kutokuwa na imani na Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi limesimamia nia yake ya kumtaka Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo Zabron Lulandala kuachia nafasi yake kutokana na kile walichodai kuwa ameshindwa kuwawajibisha watendaji walioshindwa kuwatumikia wananchi.
Kauli hiyo ya Baraza la Madiwani iliibuka katika kikao cha Baraza hilo baada ya Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya  Ezekiah Kilemile kuwataka madiwani  kuangalia aina ya adhabu wanazopaswa kutoa kwa kile alichodai kuwa adhabu zingine zinaweza kuigharimu Halmashauri iwapo watumishi wataamua kuchukua hatua za kisheria.
Kilemile alisema kuwa kitendo cha kutoa adhabu au kumhamisha mtumishi kunapaswa kuzingatia taratibu za kisheria na kwamba hali hiyo itasababisha watumishi wafanye kazi kwa woga kutokana na maazimio ya Madiwani ambayo yanahatarisha ajira zao.
Mara baada ya kauli hiyo ambayo ilionesha kama vile imewasha moto Madiwani hao walisimama kwa pamoja wakitaka kutoa hoja ya kupinga kauli hiyo ya Mwakilishi wa Katibu Tawala wakidai kuwa  hana nia njema na Halmashauri hiyo.
‘’…Mfumo wa TAMISEMI unawakinga wanaokosea, watendaji wanaoharibu katika maeneo yetu wanatetewa na Mkoa, sisi ndio tunaojua utendaji wao, mfumo wa TAMISEMI ni mbovu tumechoka kuendeshwa kwa mfumo huu, tuachieni wenyewe tuchukue hatua sio kubembelezana,’’alisema Samson Simkoko Diwani wa kata ya Halungu.
Naye Diwani wa Kata ya Ihanda Joel Kasebele alidai kuwa Ofisi ya Mkoa imekuwa ni chanzo cha matatizo kwa watumishi kwa kuwa wanapowajibishwa baada ya kushinda kuwajibika ofisi hiyo imekuwa ikisimamia kuwatetea na kwamba maazimio yanayotolewa katika vikao vya Baraza la Halmashauri yanavunjwa na watendaji wa Mkoa.
Alisema kuwa iwapo Ofisi ya Katibu Tawala inaona Ofisa Utumishi huyo bado anafaa ni bora ahamishiwe kituo kingine cha kazi kwa kuwa baada ya kuazimiwa na Madiwani utendaji wake umezidi kudorora na kuwa amekuwa hatoi ushirikiano wowote kwa Madiwani.
‘’Tunaomba huyu mtu uondoke naye, hapa pamekuwa si mahala salama kwa utendaji wake, hata ukimwacha hawezi tena kuwatumikia wananchi kwa ufanisi,’’alisema Julius Simbeye Diwani wa Kata ya Nyimbili.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Allan Mgullah alisema kuwa ni vyema Ofisa Utumishi huyo angeondoka na kwamba mbali na kukosa imani naye katika utendaji  amekuwa akitoa majibu mabaya kwa madiwani na hivyo kuendelea kukosa imani naye katika kuitumikia Halmashauri hiyo.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elick Ambakisye alielezea baadhi ya mapungufu ya Ofisa Utumishi huyo ambayo yalibainika katika kikao kilichopita ni pamoja na kutowasimamia baadhi ya watendaji wa vijiji na kata ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakifanya ubadhirifu na kutumia vibaya fedha zinazokusanywa katika maeneo hayo.
Alisema miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na kutosoma mapato na matumizi ya vijiji, kutumia stakabadhi za kughushi, kutumia vibaya ruzuku ya mbolea iliyogawanywa na serikali kwa wakulima na kuwahamisha watendaji walioharibu kijiji kimoja na kuwapeleka katika vijiji vingine hali ambayo inamuondolea sifa ya uwajibikaji ndani ya Halmashauri hiyo.

Post a Comment