Ads (728x90)

Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya Mjini John Mwambigija akielezea azma yao ya kutangaza mkutano wa UKAWA unaotarajia kufanyika Mei 22
Katibu Mwenezi wa CHADEMA Mbeya Mjini Baraka Mwakyabula akitoa msimamo wa UKAWA kuhusu kuwa na gari la (PA) juu ya mkutano wa UKAWA jijini Mbeya Mei 22

 

Baadhi ya waandishi wa Habari waliokuwepo kwenye kikao hicho


Katibu wa Chama Cha Wananchi CUF  Zacharia Mwidunda akizungumzia mkutano wa UKAWA utakaofanyika Mei 22, utakaohutubiwa na Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahimu Lipumba

Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA) Mbeya imekumbana na kikwazo kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya baada ya kudai kuwa wamezuiwa kutangaza ujio wa mkutano wa hadhara utakaohutubiwa na viongozi wa Kitaifa Jijini Mbeya MEI 22.
UKAWA wamedai kukumbana na vikwazo hivyo katika ofisi ya Ofisa Utamaduni wa Jiji ambaye alikataa kupokea hela kwa ajili ya kupita na matangazo barabarani maarufu kama PA kwa nia ya kuwajulisha wananchi mkutano wa UKAWA.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa Habari kwenye Hotel ya Mbeya Peak leo mchana Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya mjini John Mwambigija alisema kuwa pamoja na kupata vikwazo hivyo wao watazunguka na gari la matangazo kote mjini huku wakisindikizwa na Blue Guard wao ambao watalinda vurugu zozote zitakazosababisha wao wasifanye matangazo hayo.
''Tumefuata taratibu kihalali tumeenda Ofisi za Ofisa Utamaduni kulipia matangazo kama yanavyofanyika matangazo mengine Jijini, Ofisa Utamaduni amekataa hela yetu na kutunyima kuwajulisha wananchi juu ya Mkutano wetu, sisi tutafanya mkutano kama tulivyopanga, tutasindikizwa na Blue Guard wetu katika gari nyuma,''alisema Mwambigija.
Katika taarifa yake juu ya mkutano huo  Mwambigija alisema kuwa viongozi wa Kitaifa wa UKAWA wakiongozwa na Profesa Ibrahimu Lipumba watafanya mkutano katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe ambapo pia atakuwepo Said Mohamed(Makamu Mwenyekiti CHADEMA (Zanzibar) Danda Juju wa NCCR Mageuzi na Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi(SUGU).
Aidha alisema kuwa ili kuepuka mamluki wanaopandikizwa katika mikutano hiyo na kuweka mabango, wao UKAWA hawatakuwa na bango hata moja hivyo mamluki yoyote atakayejitokeza na bango atashughulikiwa ipasavyo.
''Tumepata taarifa mamluki wa (chama kimoja cha siasa) wamejipanga kuwa na mabango sisi hatutakuwa na mabango, tunawaonya watakaokuja na mabango wasimlamu mtu kwa yale yatakayowapata" alionya Mwambigija.
Mkutano huo na waandishi wa habari uliwahusisha pia viongozi wa CUF, na NCCR Mageuzi ambao walisisitiza kuwa mkutano huo umelenga kuwazindua wananchi waidai Tanganyika yao ambayo imepotezwa kwa maslahi ya wachache.
''Mkutano wetu una nia ya kuwazindua wananchi waidai Tanganyika yetu na kuhitaji serikali tatu,nia yetu ni kufanya mkutano wa amani na utulivu pamoja na kunyimwa kibali cha Maandamano na Jeshi la polisi,''alisema Zacharia Mwidunda Katibu wa CUF Mbeya mjini.
Kwa upande wake Katibu wa NCCR Mageuzi Mbeya mjini George Mbogela alisema kuwa wameamua kuunganisha nguvu kujenga umoja na mshikamano ili kudai uhuru wa maoni ya wananchi yaliyotolewa juu ya uhitaji wa serikali tatu usihodhiwe na chama tawala.
''Tumeamua kwa pamoja kutetea Utanganyika wetu, tumedhamiria kuwakumbusha wananchi juu ya mtazamo wa UKAWA kuhitaji kuwepo kwa serikali tatu,''alisema Mbogela.

Post a Comment