Wachezaji wa timu ya Kimondo wakicheza kufurahia ushindi mara baada ya kupata bao la pili |
Na Danny Tweve wa Indaba Blog
Ligi
daraja la kwanza imeendelea kuchanua katika viwanja mbalimbali nchini ambapo
katika uwanja wa CCM Vwawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya wenyeji Kimondo wamejiongezea pointi tatu muhimu baada ya kuisasambua timu Mkamba Rangers ya Morogoro mabao 4-0.
Katika
mchezo huo uliojaa ufundi na mashambulizi ya kasi, ulimalizika kwa wenyeji
kuweka kibindoni pointi tatu, huku wageni wakiondoka vichwa chini.
Katika
michezo mingine majimaji iliutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wakati ambapo Burkina Faso ya Morogoro
ilisafiria nyota ya Kurugenzi Mufindi kwa kufungana bao 1-1.
Kimondo
ambayo katika mchezo uliopita ilitoka suluhu ya kutofungana na Burkina Faso
ilionyesha dalili za ushindi tangu mchezo kuanza baada ya mashambulizi kadhaa
ya kosa kosa kuliandama lango la Mkamba.
Bao
la kwanza la Kimondo lilipatikana mnamo dakika ya 32 kupitia kwa Christopher
Kasekwa baada ya kuunganisha mpira wavuni uliopigwa kwenye adhabu ndogo.
Bao
la Pili la Kimondo liliwekwa wavuni kupitia kwa
Charles Hiza mnamo dakika ya 39
ambaye aliunganisha wavuni mpira uliotokea wingi ya kushoto kwa Christopher
Kasekwa.
Hadi
mapumziko kimondo ilikuwa mbele ya bao
2, na kipindi cha pili mchezo uliendelea kwa timu ya Mkamba rangers kujaribu
bahati yao lakini hali iliendelea kuwa tete kwa upande wao kwani mnamo dakika
ya 87 Geofrey Mlawa aliipatia timu ya Kimondo bao la tatu.
Bao
hilo lilitokana na piga nikupige iliyojitokeza langoni mwa Mkamba baada ya
shambulizi lililofanywa na safu ya ushambuliaji ya Kimondo kufuatia gonga baina
ya Charles Hiza, Geofrey Mlawa na Godfrey Magetha na kupiga hodi kwenye lango la Mkamba huku
kipa wake Noel Steven Mkachage akionekana kushindwa kumudu kutokana na ufupi.
Bao la nne liliwekwa kimiani na mshambuliaji hatari Bryson Mponzi
dakika moja baada ya bao la tatu baada ya kuanzisha shambulio lililombambatiza
mlinzi wa Mkamba Thabit Kameta na hivyo mpira huo kumfikia mfungaji ambaye
alimchambua kipa wa Mkamba na kuhesabu bao hilo.
Ingawa
bao la tano liliwekwa wavuni dakika ya 90 mwamuzi alipiga filimbi kuwa kipa wa
mkamba alikuwa amesukumwa na hivyo mchezo kumalizika huku timu ya Kimondo ikitoka na ushindi
wa bao 4 –0 dhidi ya Mkamba ya Morogoro.
Baada
ya mchezo viongozi wa Mkamba walionekana kulaumiana na wachezaji na
Mwalimu wake Amri Ibrahimu alipohojiwa kama ana maoni yoyote
juu ya mchezo huo alisema nafasi ya kuzungumza amemwachia msaidizi wake Mohamed
Mgalike na meneja wa Timu Gaudence Mnyangao ambao walikataa kuzungumzia mchezo
huo licha ya kukiri kuwa wamezidiwa.(stori na picha kwa hisani ya Indaba Blog)
Post a Comment