Ads (728x90)

Gari la Polisi maarufu kama Washa Washa ambalo ni mkakati mpya wa Jeshi la Polisi kukabiliana na Uhalifu


Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi nchini Rashid Omar akielezea changamoto inazokumbana nazo Jeshi la Polisi nchini katika utendaji wake.



Mweka hazina wa Chama Cha Waandishi wa habari mkoa wa Mbeya Brandy Nelson akielezea namna ambavyo Jeshi la Polisi limekuwa kero katika utendaji wake wa kila siku hususani kuhusu vitendo vya rushwa kwa askari wa usalama barabarani


Katibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mbeya Emanuel Lengwa akifafanua jambo juu ya umuhimu wa Jeshi la Polisi kushirikisha Jamii katika kukabiliana na vitendo vya Uhalifu

Washiriki wa Mkutano wa siku moja uliolihusisha Viongozi wa Jeshi la Polisi na wadau Jijini  Mbeya.


Washiriki wa mkutano ulioitishwa na Jeshi la Polisi wakifuatilia kwa makini maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro(hayupo pichani)




Na Bloga Wetu
JESHI la polisi limejipanga kutumia njia mpya ya ukamataji salama kwa kutumia maji ya upupu badala ya kutumia virungu na mkong’oto ili kuwanasa  wahalifu wanaokabiliwa na makosa mbalimbali ya jinai.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi nchini Rashid Omar alipokuwa akielezea mikakati ya jeshi hilo katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika kikao cha Siku ya Polisi kilichofanyika Jijini Mbeya jana.
Bw. Omar alisema kuwa jeshi la polisi limejitahidi kwa kila njia kukabiliana na kuzuia vitendo vya uhalifu ambapo limeamua kutumia njia mpya ya ukamataji salama kwa kumwagia maji ya upupu badala ya mkong’oto.
‘’Tumeamua kutumia utaratibu mpya wa ukamataji salama badala ya kupiga sasa tunamwagia maji ya upupu, njia hii ni nyepesi kwetu kuwanasa wahalifu, hata wakinawa maji tutawanasa tu, ‘’alisema.
Aidha alisema Tanzania ni moja ya nchi zinazokabiliwa na ongezeko kubwa la tishio la Uhalifu na  wizi wa kimtandao ambapo ili kukabiliana na changamoto hizo kuna haja ya kuweka utaratibu wa kuwa na daftari la wakaazi kwa Tanzania Bara na Visiwani.
Alisema utaratibu wa kuwepo kwa daftari la wakaazi utasaidia kuratibu aina ya watu wanaoishi katika jamii na kwamba matukio ya uhalifu na uvamizi wa Westgate uliotokea nchini Kenya ni aina ya uvamizi unaopaswa kuchukuliwa tahadhari mapema.
 Bw. Rashid Omar alisema kuwa pamoja Jeshi hilo linachangamoto kubwa katika utendaji wake kutokana na uwiano askari mmoja kuhudumia raia 1200 ilhali takwimu za Kimataifa ni askari mmoja kuhudumia raia 500.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alilitaka Jeshi la polisi kuacha kufanya kazi kwa mazoea kutokana na lawama nyingi zinazoelekezwa kwa jeshi hilo hususani kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu, kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ubambikizaji wa kesi.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi linapaswa kufanya kazi kwa weledi na umakini mkubwa hususani katika kipindi hiki ambacho baadhi ya wananchi wamekuwa hawataki kuheshimu utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani.

Post a Comment