Ads (728x90)MHADHIRI wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari nchini Dotto Kuhenga amesema imefika wakati kwa watumiaji wa mitandao ya Kijamii maarufu kwa jina la Blogers watambuliwe kama wanahabari kutokana na mchango mkubwa wanaoutoa katika tasnia ya habari kufuatia kwa kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano duniani.
Mwalimu Kuhenga aliyasema hayo wakati akitoa mhadhara mbele ya wamiliki na waandishi wa mitandao ya Kijamii nchini katika mafunzo ya siku mbili kwa 'Blogers' yaliyoadaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA jijini Dar es salaam hivi karibuni.
Alisema teknolojia ndiyo inayoendesha tasnia ya habari kwa sasa kutokana na Media House nyingi kuwa na vyanzo kutoka kwenye mitandao ya kijamii ya FaceBook, Twitter na Blog.
Alisema ushiriki wa wapokeaji wa habari umewawezesha waendeshaji wa Blog na Twitter kuwa wanahabari hivyo ni muhimu kwa sasa kuwezeshwa kwa kupewa nyenzo za kufanyia kazi kama wanahabari kamili.
Mhadhiri huyo wa Shule Kuu ya Uandishi wa habari nchini alisema mabadiliko ya Demokrasia na Utandawazi yameleta maendeleo makubwa katika teknolojia ya mawasiliano nchini ikiwa ni pamoja na kukua kwa Uhuru wa habari na teknolojia hiyo nchini.
Alisema hata hivyo pamoja na kutambuliwa kwa Blogers kama wanahabari ni muhimu wakapata nyenzo za kufanyia kazi kwa kufuata maadili ya taaluma ya habari ili kuepuka migongano ndani ya jamii.
Alibainisha kuwa waendesha mitandao ya kijamii wanapaswa kufuata miiko ya taaluma ya habari kama inavyotakiwa na wanahabari na kwamba iwapo watatumia vibaya Uhuru wa uendeshaji wa mitandao ya kijamii nchini watakuwa wanafanya makosa kama wakosaji wengine katika taaluma ya habari.
Kwa upande wake mwakilishi wa Baraza la Habari nchini (MCT)Bi. Pili Mtambalike alisema kuwa Mitandao ya Kijamii imepata uhuru mkubwa wa utoaji wa taarifa katika jamii na kwamba kwa kuwa ni sehemu ya vyanzo vya habari ni muhimu ikatumika vyema ili kuepuka kutoa taarifa zinazoweza kusababisha madhara na hata kufikishwa mahakamani.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA Profesa John Nkoma alisema kuwa waendeshaji wa mitandao ya Kijamii wanapaswa kujiunga ili kuwa na Umoja wao wenye nguvu na kwamba Mamlaka ya Mawasiliano itawaunga mkono kutokana na kutambua mchango mkubwa wa waendeshaji wa mitandao ya kijamii.
Awali Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy alisema kuwa  Mamlaka ya Mawasiliano imeamua kuwakutanisha waendeshaji wa mitandao ya Kijamii nchini ikiwa ni hatua ya awali kutambua umuhimu wa kazi zao katika kukua kwa maendeleo ya Kiuchumi,kijamii na kisiasa nchini.
Alisema ni muhimu kwa waendeshaji wa mitandao ya kijamii ambao kwa muda mrefu wamekuwa ni vyanzo vikuu vya habari nchini kutambuliwa na kuthaminiwa ili kujenga ushirikiano katika kukuwa kwa muktadha wa mawasiliano na teknolojia ya habari na mawasiliano nchini.

Bi. Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari (MCT)
Bi. Pili Mtambalike(MCT) na Mkuu wa Mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy wakateta jambo wakatiwa mafunzo kwa Blogers nchini
Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari nchini Dotto Kuhenga akielezea umuhimu wa Blogers katika vyanzo vya habari kwa Media House nchini


Mkuu wa Biashara na Masoko wa mtandao wa Kijamii wa Jamii Forums Mike Mushi akielezea umuhimu wa mitandao ya Kijamii katika kuongeza kipato na uchumi wa nchi.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano TCRA Profesa John Nkoma akifafanua jambo wakati wa mafunzo kwa waendeshaji wa mitandao ya kijamii nchini.

Mkurugenzi wa Jamii Forums Maxene Melo akifafanua jambo wakati wa mafunzo kwa Blogers

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari nchini Dotto Kuhenga(katikati)na Mkuu wa Biashara na Masoko wa Jamii Forums wakifuatilia jambo wakati wa mafunzo kwa Blogers nchini

Bloger Othuman Michuzi akikabidhiwa cheti na Mkurugenzi wa TCRA Profesa John Nkoma kwa kutambua mchango wa maendeleo ya tasnia ya habari nchini

Baadhi ya Blogers katika picha ya pamoja


Bloger Jeff Msangi akipokea cheti kutoka kwa Mkurugenzi wa TCRA Prof John Nkoma ikiwa ni kutambua mchango wa waendeshaji wa mitandao ya Kijamii(Blogers) kwa maendeleo ya tasnia ya Habari nchini.

Post a Comment