Ads (728x90)

Wachezaji wa timu ya Mbeya City wakiingia uwanjani kwa ajili ya mechi ya timu ya Coastal Union leo jioni
Wapenzi wa mpira wakiwania tiketi nje ya uwanja wa Sokoine kwa ajili ya mechi kati ya Mbeya City na Coastal Union,timu hizo zilitoka sare ya 1-1
Kikosi cha timu ya Coastal Union ya Tanga ambacho kimeminyana na Mbeya City na kutoka sare ya bao 1-1


Wachezaji wa timu za Mbeya City  Deus Kaseke na Othman Tamim wa timu ya Coastal Union wakiwania mpira wakati wa mechi ya ligi Kuu katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine leo jioni
Patashika langoni mwa timu ya Coastal Union
Goli likiwa limetinga wavuni mwa goli la Coastal Union baada ya mchezaji wa timu ya Mbeya City Mwagane Yeya kupachika bao hilo kwa njia ya kichwa.
Kocha wa timu ya  Coastal Union  Hemed Moroco akielezea mchezo wa timu yake na Mbeya City
Msalaba Mwekundu wakimtoa nje ya uwanja golikipa wa timu ya Coastal Union ambaye amekuwa akianguka mara kadhaa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ameshikwa na musuli
Golikipa wa timu ya Coatal Union Hassan Shaabanakiwa amelala chini baada ya kupata maumivu ya musuli
Waamuzi wa Mchezo kati ya Mbeya City na Coastal Union, washika kibendera Hamis Chang'walu, Mashaka Mwandemba,Refarii Oden Mbanga na Omar Kambangwa wakiwa na makepteni wa timu za Coastal Union  Jery Santo na Hassan Mwasapili wa Mbeya City
MCHUANO wa ligi kuu umeendelea leo katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine Jijini ambapo wenyeji Mbeya City waliwakaribisha Coastal Union ya Tanga na kuilazimisha kutoka sare ya bao 1-1.

Mchezo huo umeanza kwa kuviaziana ambapo timu ya Coastal Union ndiyo ilikuwa ya kwanza kuliona lango la timu ya Mbeya City dakika ya saba ya mchezo baada ya mchezaji wa timu ya Coastal Union Haruna Moshi Boban kuwatoka walinzi wa Mbeya City, Anton Matogolo,Alex Seth na Steven Mazanda  na kujipatia bao kwa mkwaju hafifu uliompita golikipa wa timu ya Mbeya City David Baruani.

Goli hilo liliamsha hoihoi kwa washabiki wachache wa timu ya Coastal Union ambao walikuwa wakiburudisha uwanja kwa ngoma yao ya Mdumange.

Baada ya goli hilo wachezaji wa timu ya Coastal Union walionesha kupoteza muda ambapo kila mpira ulipofika katika goli lao golikipa wa timu hiyo Hassan Shaaban alikuwa akiuchezea chezea kwa muda mrefu bila kuupiga hali ambayo iliibua malalamiko kwa washabiki ambao walianza kumzomea.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Coastal Union walitoka kifua mbele kwa bao 1-0,ambapo hata hivyo Golikipa wa Coastal Union Shaaban alitoka nje ya uwanja baada ya maumivu ya musuli na badala yake kuingia Said Libawa.

Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi makali yaliyofanywa na timu ya Mbeya City na hivyo kulazimisha kona tatu zilizoelekezwa kwa timu ya Coastal ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda.

 Mchezo huo ambao ulitawaliwa na kipyenga cha mara kwa mara kutoka kwa refarii Oden Mbanga wa Dar es salaam aliyesaidiwa na washika vibendera Hamis Chang'walu na Omar Kambangwa kutokana na rafu za hapa na pale.

Mashambulizi katika lango la timu ya Coastal yalizaa matunda katika dakika za lala salama ambapo katika dakika ya 89 wachezaji wa timu ya Mbeya City walionana vizuri na kusababisha goli la kusawazishwa lililofungwa kwa njia ya kichwa na mchezaji wa timu ya Mbeya City Mwagane Yeya aliyeingia katika kipindi cha pili.

Hata hivyo dakika chache baadaye refarii ametoa kadi nyekundu kwa wachezaji wawili wa timu ya Coastal na Mbeya City ambao walionekana kubishana uwanjani ambao ni Marcus Ndeheli na Richard Peter na baadaye zikiwa zimesalia sekunde kadhaa kumalizika kwa mchezo Haruna Moshi naye alipewa kadi nyekundu kwa kumtolea lugha ya matusi mshika kibendera Hamis Chang'walu.

Hadi Kipyenga cha mwisho kinapulizwa timu zilikuwa sare ya bao 1-1.

Post a Comment