Ads (728x90)ZAIDI ya sh. milioni 300 fedha zinazotokana na mradi wa vibanda 120 vya chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya zinadaiwa kutafunwa na kuingizwa katika akaunti za watu binafsi.

Taarifa za ndani ya chama hicho zinadai kuwa vibanda hivyo ni kati ya miradi mikubwa ya chama katika kata hiyo ambapo uanzishwaji wake ulilenga kukiongezea kipato chama ili kukabiliana na wimbi la upinzani lililoshamiri katika jimbo la Mbozi Magharibi.

Vibanda hivyo ambavyo viko jirani kabisa na kituo cha Polisi cha Tunduma karibu na mpaka wa Tunduma na nchi jirani ya Zambia vinadaiwa kulenga kukipatia chama hicho mamilioni ya fedha ambapo hata hivyo fedha zilizotokana na uzabuni wa vibanda hivyo zinadaiwa kutafunwa na watu wachache.

Utata uliogubikwa kuhusu fedha za uzabuni wa vibanda hivyo umeelezwa kuwa umetokana na viongozi wa chama hicho ngazi ya kata kuwatoza wafanyabiashara waliohitaji vibanda hivyo kiasi cha sh. 100,000 kwa kila mmoja ambapo hata hivyo fedha zilizotokana na zabuni hiyo zinadaiwa kuingizwa katika akaunti za watu binafsi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari hii ni kwamba jumla ya wafanyabiashara 120 walijitokeza kuomba vibanda hivyo na kulipia kiasi cha sh. 100, 000 kwa kila mmoja na hivyo kuingiza kiasi cha sh. milioni 12 ambazo hazijulikani matumizi yake hadi sasa.

Aidha mara baada ya wafanyabiashara 120 kukubaliwa uzabuni wao kila mmoja alitakiwa kutoa kiasi cha sh. milioni 3 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vibanda hivyo ambapo zilikusanywa kiasi cha sh. milioni 360 zilizopaswa  kuingizwa katika akaunti ya chama.

 Mwandishi wa habari hizi alishuhudia hali ya vibanda hivyo vilivyoanza Mwezi Machi 2012 ambao ulitarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka huu ambapo hata hivyo hadi sasa vibanda hivyo kwa sasa vinatumiwa kama hifadhi ya wavuta bangi na sehemu ya kujisaidia haja kubwa na ndogo kwa wapita njia.

Gazeti hili lilishuhudia vyumba hivyo vikiwa vimetapakaa vinyesi na vipisi vya sigara ambapo ujenzi huo ambao umegharimu kiasi kikubwa cha fedha hauna gharama za ujenzi(BOQ), Ramani wala mkataba wa ujenzi hali ambayo inazidi kuongeza maswali juu ya matumizi halali ya fedha za mradi huo.

Kadhalika uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa katika harakati zote za ujenzi hakukuwa na uthibitisho wowote wa risiti ambazo zingepaswa kuwasilishwa katika vikao vya mapato na matumizi ya chama ilhali fedha zilizopatikana kwa ajili ya gharama za ujenzi ziliingizwa katika akaunti za watu binafsi.

Akaunti zilizokuwa zikitumiwa kuingiza fedha hizo ni pamoja na akaunti yenye namba 615250658 ya NMB tawi la Tunduma ambayo Mei 5, 2012 ziliingizwa kiasi cha sh. milioni 20  na akaunti nyingine yenye namba  615500155 ambayo ilitumika kuingizwa fedha kiasi cha sh. milioni 30 kati ya Mei 11 hadi Mei 16.

Kulingana na taarifa za ndani ya chama hicho zinadai kuwa akaunti hizo ni za watu binafsi na kwamba fedha hizo kiasi cha milioni 50 hazijulikani matumizi haye hadi sasa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM kata ya Tunduma Bw. Daniel Mwashiuya alisema kuwa fedha zilizokuwa zikikusanywa kwa ajili ya ujenzi hazikuingizwa katika akaunti ya chama bali zilikuwa zikipitiliza kwa mkandarasi kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa vibanda hivyo.

Naye Katibu wa CCM Kata ya Tunduma Bw. Hemed Steven alisema kuwa mradi huo wa vibanda 120 ulitarajiwa kugharimu kiasi cha sh. milioni 270 ambapo kila mpangaji alilipia sh. milioni 3 fedha ambazo amelipwa  mkandarasi kampuni ya Wazawa Company Group.

Hata hivyo  kauli ya Katibu wa chama  Bw. Steven inapingana na makusanyo halisi ya fedha za wapangaji na kwamba kiasi hicho cha fedha sh. milioni 270 alizotaja kumlipa  mkandarasi hakilingani na fedha halisi za malipo ya wapangaji 120 ya jumla ya sh. milioni 3 kwa kila mmoja ambazo ni sawa na sh. milioni 360 ambazo ni  pungufu kwa sh. milioni 90.
Baadhi ya Vibanda amb avyo ni sehemu ya mradi wa CCM kata ya Tunduma ambao fedha zake zinadaiwa kutafunwaPost a Comment