Ads (728x90)



Mkuu wa wilaya ya Momba Abihudi Saideya akisisitiza jambo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Momba. 
Diwani wa Viti Maalum kata ya Ivuna Colletha Mwaselela aliyeibua hoja ya kushambuliwa kwa Ufuta na wadudu wa ajabu.
Kaimu Ofisa Kilimo wa wilaya ya Momba Henry Kiondo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba Anton Mwantona. 
Shamba la Ufuta

FUNZA wa ajabu wenye maumbile madogo mchanganyiko wa rangi, nyekundu, nyeusi na kijani wamevamia na kushambulia kwa kasi zao la Ufuta katika vijiji vilivyopo Tarafa ya Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya.
Vijiji vilivyoathiriwa na janga hilo na majina ya kata zake kwenye mabano ni Mkongo,Usoche, Senga na Muuyu(Kamsamba),Vijiji vya Mkulwe,Namsinde na Itelesya(Mkulwe) na vijiji vya Ivuna, Ifumbula,Samang’ombe na Mkomba(Ivuna).
Kwa mujibu wa wakulima wa zao hilo walidai kuwa wadudu hao wenye ukubwa mithili ya mchanga wanafanana na viwavi wanapokuwa wadogo na baadaye huwa kama Panzi wadogo ambao hukaa ndani ya maua ya Ufuta kabla ya kupasuka.
Wadudu hao wamedaiwa kushambulia mazao hayo kwa kipindi cha miaka miwili mfulululizo ambapo awali wakulima wa vijiji hivyo walizoea kulima bila  kutumia mbolea wala dawa za kuulia wadudu.
Mmoja wa wakulima wa zao hilo ambaye ni Diwani wa Viti maalumu kata ya Ivuna Colletha  Mwaselela alisema kuwa yeye aliwekeza kwenye shamba lenye  hekari 15 kiasi cha sh.  milioni 3.5 na  matarajio yake ni kupata debe 400 ambazo angeuza kwa sh. Milioni 18 lakini alivuna jumla ya debe 62 alizopata kiasi cha sh. Milioni 2.8.
Naye Diwani wa Kata ya Kamsamba Hezrone Sapali alisema kuwa yeye alilima kiasi cha hekari 11 ambazo aliwekeza kiasi cha sh. Milioni 1 kwa matarajio ya kupata jumla ya sh. milioni 4 lakini alivuna kiasi cha debe 52 alizouza sh. milioni 1.
Mkulima mwingine ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkulwe Mathew Chikoti alisema kuwa yeye alilima jumla ya hekari 10, lakini alivuna hekari 5 tu na zingine zilishambuliwa na wadudu na hivyo kujikuta akipata hasara na kuwa aliwekeza jumla ya sh. 1.5 na matokeo yake alipata chini ya matarajio kiasi cha  sh.milioni 1.
Kwa upande wake mkulima mkazi wa kijiji cha Karungu kata ya Ivuna Gervas Zyembele alisema kuwa alilima jumla ya hekari 48 ambazo alitarajia kuvuna kiasi cha gunia 100 ambazo angeuza jumla ya sh. milioni 35 lakini amevuna debe 48 ambazo ameza jumla ya sh.milioni 1.4.
Zyembele aliiomba serikali kutembelea kwa wakulima kujua matatizo yaliyosababisha zao hilo kushambuliwa na wadudu hao.
Kaimu Ofisa Kilimo wilaya ya Momba  Henry Kiondo alisema kuwa tatizo hilo limetokana na wakulima wengi kutojua mchanganyiko wa dawa za kuulia wadudu na kuwa eneo hilo walizoea kulima bila kutumia dawa wala mbolea.
Alisema kuwa dawa za zao la ufuta ni ghali na kuwa wakulima wengi hawamudu kununua dawa na kwamba ni vyema wakulima wakafuata ushauri wa kilimo bora cha ufuta ikiwa ni pamoja na kutolima kwenye maeneo yenye maji mengi.
Mkuu wa Wilaya ya Momba Abihudi Saideya alisema kuwa hajapata rasmi taarifa hizo na kuwa  hata hivyo amewataka watendaji wa Idara ya Kilimo kufuatilia tatizo hilo na kutoa elimu kwa wakulima ili tatizo hilo lisijirudie katika msimu ujao.


Post a Comment