Ads (728x90)

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya Hilda Ngoye akiwa katika picha na wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalangwa wilayani Chunya

Wanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari Chalangwa wilayani Chunya.
  
WANAFUNZI wa kike wa shule za Sekondari mkoani Mbeya wametakiwa kutokubali zawadi za ‘’Chipsi Kuku na Soda’’ kutoka kwa watu wasiowafahamu kwa kuwa zawadi hizo zimelenga kuwaharibia maisha na masomo yao.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Hilda Ngoye katika ziara yake ya wilaya za Chunya, Momba, Mbozi,Mbeya na Mbarali akitathmini maendeleo ya akina mama na watoto kwenye shughuli za ujasiriamali.
Mbunge huyo alisema kuwa akina mama ndiyo walezi wakuu wa familia hivyo wanapaswa kutumia nafasi waliyonayo kusimamia watoto wa kike ambao wamekuwa wakipata majaribu katika kipindi chao cha ujana na kusababisha kudanganywa na kupata ujauzito kwa zawadi za Chipsi Kuku na Soda.
‘’Akina mama mkisimamia vyema familia matatizo ya mimba mashuleni yatatoweka, wanafunzi wanadanganywa, msikubali zawadi za Chipsi Kuku na Soda, mtaharibikiwa,’’alisema huku akielekeza macho yake kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalangwa iliyopo wilayani Chunya.
Alisisitiza kuwa tatizo la mimba mashuleni limekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya watoto wa kike jambo ambalo likisimamiwa vyema kwa ushirikiano wa wazazi, walimu na wanafunzi linaweza kutoweka.
Aidha aliwataka wanafunzi hao kuwa na wivu wa maendeleo ya kimasomo na kutokubali vishawishi vitakavyosababisha wao kushindwa katika masomo.
Awali akielezea matatizo yaliyopo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Chalangwa, Makamu Mkuu wa Shule hiyo  Morris Mbwilo alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2013-14 jumla ya watoto saba wa wameishia njiani kwa kupata ujauzito.
Alisema kuwa mwaka 2013 jumla ya watoto watano walipata ujauzito shuleni na kushindwa kuendelea na masomo ambapo pia hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu watoto wawili wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na ujauzito.

Post a Comment