Ads (728x90)Mkuu wa Wilaya ya Momba Abihudi Saideya akiandika namba ya usajili  katika mtumbwi wa uvuvi wakati wa uzinduzi wa Ziwa Rukwa ambalo lilifungwa kwa miezi 6 kutokana na uharibifu wa mazingira.
Uoto wa asili umerejea baada ya Ziwa kufungwa kwa miezi 6

Wavuvi wakikokota Mtumbwi kuelekea Ziwani baada ya kusajiliwa kwa matumizi halali ya uvuvi ziwani humo
ZANA za uvuvi haramu zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 69 zimenaswa na kutekekezwa kwa kipindi cha miezi sita cha kufungwa kwa Ziwa Rukwa wakati wa operesheni maalumu iliyokuwa ikifanywa kuzuiwa wavuvi haramu Wilayani Momba Mkoani Mbeya.
Ziwa Rukwa lilifungwa kwa miezi sita kutokana na tangazo maalumu lililohusisisha wilaya jirani za Chunya mkoani Mbeya na Mlele wilayani Sumbawanga ambapo zilikubaliana kwa pamoja kulinusuru ziwa hilo lililokumbwa na uharibifu wa mazingira, uvuvi haramu na kusababisha kupungua kwa samaki ziwani humo.
Katika taarifa iliyosomwa wakati wa kufunguliwa kwa Ziwa hilo kwenye kilele cha Siku za Serikali za Mitaa kilichofanyika kijiji cha Samang’ombe ufukweni mwa ziwa hilo, Ofisa Uvuvi Ali Libenanga alisema kuwa kwa kipindi cha miezi sita ya kufungwa kwa ziwa hilo doria mbalimbali zilifanyika na kufanikiwa kukamata wavuvi haramu wenye zana za uvuvi zenye thamani ya sh. Milioni 69.9.
Libengana ambaye alisoma taarifa hiyo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Momba Abihudi Saideya kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri Antony Mwantona alisema kuwa kwa kipindi cha kati ya Januari na Mei katika forodha tofauti za wilayani humo zilikamatwa nyavu na baruti zilizohusisha uvuvi haramu.
Alisema nyavu hizo ziliteketezwa  Machi 5 ambapo jitihada za kuendelea kuhifadhi ziwa hilo zilitekelezwa kwa kuwahusisha wananchi wa maeneo hayo kwa kuweka mikutano ya hadhara kwa nia ya kulitunza Ziwa hilo pamoja na fukwe zake.
Miongoni mwa zana zilizokamatwa na kuteketezwa ni pamoja na mitumbwi, nyavu,na baruti katika forodha nane  za Mtakuja,Nunka,Uwanja wa Ndege,Mchangani,Chafundika,Masuche zilizopo wilayani Momba mkoani Mbeya na wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Kufuatia kufunguliwa kwa Ziwa hilo Libenanga alisema halmashauri imeamua kulifanya Ziwa hilo kuwa ni chanzo kikuu cha Mapato na kuwa wavuvi wote wanaovua ziwani humo watapaswa kuwa na leseni ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kusajili vyombo vyao  vya  uvuvi.
‘’Kila mvuvi anapaswa kuwa na leseni ya uvuvi itakayotolewa kila mwaka, kwa sh.16,000,chombo kinasajliwa mara moja kwa sh.16,000,matumizi ya leseni ni ya mwaka mmoja,’’alisema Libenanga.
Akizungumza wakati wa kufunguliwa kwa Ziwa hilo Mkuu wa Wilaya ya Momba Saideya alisema kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kulitunxza Ziwa hilo ambalo limekuwa ni sehemu ya chanzo cha mapato cha Halmashauri ya wilaya hiyo.
Aliwataka wananchi kudhibiti  mifugo yao ili isiingie ovyo ziwani na kutunza vyanzo vyake ili kutoathiri uchumi wa wakazi wa maeneo yanayolizunguzuka hivyo ni vyema kila mwananchi akawa mlinzi wa kuhifadhi uoto wa asili ambao umeanza  kuwa kivutio pembezoni mwa ziwa hilo.

Post a Comment