Ads (728x90)


wataalam wa sekta ya kilimo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mlele wakikagua mashamba Kijiji cha  Mwamapuli Katika Bonde la ziwa Rukwa ambalo ni eneo maarufu kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali. 
 

Na Kibada Kibada –Katavi.

Halmashauri ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 868.3 sawa na asilimia ya 72 ya lengo liliowekwa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa kipindi cha mwezi julai 2013 hadi kufikia juni 2014.
 Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya  Wilaya ya Mlele Wilbrod Mayala kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ilieleza kuwa  Halmashauri ilijiwekea lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1,214,078,000/=.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa hadi kufikia kipindi hicho Halmashauri ilikuwa imefanikiwa kukusanya jumla ya kiasi cha shilingi 868,383,958.46 ambayo ni sawa na asilimia 72.

Alieleza kuwa  Mapato hayo yanatokana na vyanzo mbalimbali ambavyo ni Ruzuku ya Kawaida,Vyanzo vya ndani,Fidia ya vyanzo vingine vilivyofutwa na serikali,Pamoja na mifuko mbalimbali ya miradi ya maendeleo.

Akizungumzia matumizi alielezakuwa Halmashauri ililenga kutumia jumla ya shilingi 565,518,205.25 hata hivyo matumizi halisi  yalikuwa kiasi cha shilingi milioni 819,304,922.34 sawa na asilimia 145 hivyo kuvuka makusanyo waliyokusanya.

Akizungumzia mipango mikakati iliyowekwa kwa ajili ya kuongeza ukusanyaji wa mapato alieleza kuwa wameweka mikakati ya kufungua barabara ya Mwamapuli hadi majimoto kupitia mwamatiga ili kurahisisha usafiri na usafirishaji na kuongeza mapato ya makusanyo.

Mikakati mingine ni kukitangaza kituo cha Mwamapuli ambacho kinahusika na Masuala ya Habari za Kilimo ili kukutangaza nje ya mipaka ya Mkoa wa Katavi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kwa kueleza hali halisi ya uzalishaji wa zao la mpunga katika wilaya ya Mlele ili kukaribisha wawekezaji kuja kuwekeza zaidi katika maeneo hao ya sekta ya kilimo.

Mikakati mingine ni kupeleka maombi ya  fedha US-AID kwa mwaka huu 2014 kuombea fedha kwa ajili ya kujenga skimu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji .Post a Comment