Ads (728x90)

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akizungumza na Waandishi wa habari(pichani chini) ofisini kwake juu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Mihadarati nchini ambayo yanatarajia kufanyika Kitaifa mkoani Mbeya.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa katika kikao na Mkuu wa mkoa wa Mbeya ofisini kwake leo asubuhi.
Mkurugenzi wa Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Gloria Omar akifafanua jambo juu ya utambulisho wa dawa za kulevya
Wakili kutoka Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Charles Malamula(katikati) wakati wa taarifa ya siku ya Dawa za Kulevya nchini itakayofanyika Kitaifa mkoani Mbeya.
Mchambuzi Mkuu kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini January Ntisi akifafanua jambo katika kikao cha waandishi wa habari kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya leo asubuhi.
BAADA ya kimya  cha takribani miaka kumi tangu watu wanaodaiwa kuwa ni Vigogo wanaohusishwa na usafirishaji na uingizaji wa Dawa za Kulevya nchini majina yao kupelekwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Yusuf Makamba, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini imeendelea kusuasua kutaja majina ya Vigogo hao.
Taarifa za kuwepo kwa Vigogo 12 wa Dawa za Kulevya ziliibuliwa  Mkoani Mbeya mwaka 2014 ambapo baadhi ya watumiaji wa dawa hizo maarufu kwa jina la‘mateja’ waliodai kujihusisha na Dawa hizo waliyapeleka majina ya vigogo 12 kwa Makamba ambaye hadi anastaafu hajawahi kuyataja majina hayo.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro,juu ya taarifa za maadhimisho ya siku ya Dawa za Kulevya Nchini yanayofanyika kesho Jijini Mbeya,Mchambuzi Mkuu kutoka Tume ya Dawa za Kulevya January Ntisi alisema majina ya Vigogo hao yaliwasilishwa katika tume na yanaendelea kufanyiwa kazi kupata uthibitisho wa uhusika wao.
 ‘’Majina yalifika Tume, tuliyapokea lakini hatuwezi kuyataja, baadhi yao walishakamatwa na kesi zao zimefikishwa katika mahakama zetu na zile za nje, zipo taratibu ambazo zinaendelea kuhusiana na sheria za kimataifa juu ya suala hili,’’alisema Ntisi.
Alisema kuwa wapo ambao walitajwa majina yao ambao bado wanaendelea kutafutwa na kwamba hata hivyo udhibiti wao umekuwa ni mgumu kutokana na kuwa na mtandao mkubwa watu matajiri wenye uwezo mkubwa wa kutumia vifaa vya kisasa ikiwemo Boti ziendazo kasi.
‘’Wana mtandao mkubwa sana, wanatumia Boti ziendazo kasi, tunaendelea kuwasaka kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za kigeni, suala hili linahitaji umakini mkubwa,’’alifafanua Ntisi.
Kuhusu kuachiwa huru kwa baadhi ya watuhumiwa wa Dawa za Kulevya na vidhibiti vya dawa za kulevywa vinavyofikishwa mahakamani kupotea na kuoneka ni feki Mkurugenzi wa Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba Gloria Omar alisema kuwa taarifa zote zinazofika kwa mkemia mkuu zinafanyiwa kazi kulingana na ushahidi.
‘’Taarifa zinazoletwa kwa Mkemia Mkuu zinafanyiwa kazi kitaalamu na kuthibitishwa kulingana na ushahidi,’’alisema.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Jijini Dar es salaam Mwanaharakati wa kupigania Haki za Binadamu na Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya  Mchungaji William Mwamalanga alisema kuwa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya haina uwezo tena wa kusaidia tatizo hili na badala yake zielekezwe nguvu katika kitengo cha Jeshi la Polisi.
‘’Tume imefeli katika hili, watuhumiwa waliotajwa kuhusika na Dawa za kulevya miaka kumi iliyopita wamerejea kwa kasi na wanaedeleza biashara hizi,Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere umekuwa uchochoro wa kupitisha mihadarati,’’alibainisha.
Alisema kuwa kati ya Viwanja vya Ndege vya Kimataifa katika nchi za Afrika Mashariki uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere ndio uwanja dhaifu kuliko viwanja vyote ambapo umekuwa ukitumika kuingiza na kusafirisha Dawa za Kulevya bila udhibiti makini.
Alisema kuwa usafirishaji na uingizaji wa mihadarati  umeongezeka mara tatu kwa kipindi cha miaka kumi na kwamba idadi ya vifo na ongezeko la watumiaji limekuwa ni tishio kubwa na kwamba tume imeshindwa kudhibiti hali hiyo kwa kipindi chote tangu ianzishwe.
Kwa mujibu wa Mchungaji huyo wa Kipentekoste alisema kuwa  hadi kufikia Juni mwaka huu kulingana na utafiti uliofanywa na wanaharakati wa mapambano dhidi ya Dawa za kulevya nchini ni kwamba jumla ya vijana 6708 wamefariki kutokana na Dawa za kulevya katika Jiji la Dar es salaam pekee.
 Alisema kuwa Jiji la Mbeya jumla ya vijana 48 wamekufa ilhali katika Miji ya mipakani ya Tunduma na Kyela jumla ya vijana 104 wamefariki dunia na katika mji wa Tanga jumla ya vijana 71 wamefariki dunia ilhali Jiji la Mwanza jumla ya vijana 36 wamefariki kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Post a Comment